Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maida Hamad Abdallah
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:- Kwa kipindi kirefu suala la watumishi hewa limekuwa likiathiri sana uchumi wa Taifa na kwa kuwa waliohusika wengi wao ni maafisa na watumishi wa Serikali. Je, Serikali inasema nini juu ya wale waliohusika kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa njia hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa wanavyojitahidi na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kuhusiana na kadhia hii au suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza. Katika uhakiki unaondelea kuchukuliwa hadi tarehe aliyoitaja Mheshimiwa Waziri ni hasara kiasi gani Serikali imepata hadi kufikia tarehe hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; pamoja na mikakati ambayo Serikali imekuwa ikichukua kuhusiana na watumishi pamoja na maafisa waliohusika na swala hili. Serikali itambue kwamba kuna udhoroteshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa inakwama pamoja na ukosefu wa madawa pamoja na ufinyu wa bajeti uliokuwa unajitokeza.
Je, Serikali inaweza kukubaliana na mimi kwamba pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa kwa watumishi kwamba iwepo adhabu ya kurudisha fedha ambazo walizipoteza?
Name
Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mara nyingi tumekuwa tukitoa takwimu mwezi hadi mwezi endapo watumishi hao hewa wasingeondolewa kwa mwezi husika wangeisababishia hasara kiasi gani? Niseme tu kwamba hadi sasa tumeshaondoa watumishi hewa 19,629 ambao endapo wangeendelea kubaki katika orodha ya malipo ya mshahara kwa mwezi husika mmoja wangeisababishia Serikali hasara ya shilingi 19,749,737,180, hiyo ni kama wangebaki kwa mwezi mmoja husika bila kuondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nitoe labda takwimu ya Halmashauri mojawapo. Ningeweza kutaja kwa ujumla wake maana yake tuliomba takwimu lakini sijapiga mahesabu kwa jumla kwa haraka. Nikianzia na Kinondoni tangu ambavyo wameondoa watumishi hewa waliondoa watumishi hewa 107 na kwa kiasi cha fedha ambacho walilipwa watumishi hao ni shilingi bilioni 1.279. Nikija kuchukua kwa Halmashauri ya Kishapu watumishi 73 wamelipwa shilingi milioni 543. Kwa hiyo, ambacho naweza kusema ni kwamba endapo wangeendelea kubaki kwa kweli ni gharama kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili ni mikakati gani ambayo Serikali inachukua kuhakikisha kwamba pamoja na watumishi hawa hewa kuondolewa basi wanarejesha fedha. Nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kama nilivyotoa takwimu kwa wale ambao tayari mashauri yao yamefikishwa mahakamani wametakiwa pia aidha kulipa faini lakini pamoja kurejesha fedha na endapo watashindwa kufanya vyote viwili basi watapata kifungo jela. Na kesi mbalimbali zimekuwa zikiendelea; tayari kesi 38 zilishamalizika mahakamani, tayari kuna majalada mengine ya uchunguzi 126 yanaendelea, lakini vilevile bado tunaendelea kuhakikisha kwamba tunakamilisha na wote walioshiriki basi wanafikishwa katika vyombo vya kisheria.
Name
Venance Methusalah Mwamoto
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:- Kwa kipindi kirefu suala la watumishi hewa limekuwa likiathiri sana uchumi wa Taifa na kwa kuwa waliohusika wengi wao ni maafisa na watumishi wa Serikali. Je, Serikali inasema nini juu ya wale waliohusika kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa njia hiyo?
Supplementary Question 2
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize swali moja la nyongeza.
Pamoja na kufanya kazi nzuri ya kupatikana kwa wafanyakazi hewa ambao takribani wataokoa zaidi ya shilingi bilioni kumi na Serikali inapaswa ijazie hizo nafasi kutokana na watumishi wengine. Lakini walio wengi ni wale wanavyuo ambao sasa wanakwenda kuanza vyuo, lakini mpaka leo tunavyozungumza hawajapata mikopo wanahangaika. Je, kuendelea kutokuwapa mikopo hatuoni kwamba tunaweza tukazalisha hewa nyingine zaidi? Sasa Serikali iseme mpango mzima kwa nini mpaka leo mikopo ya wanafunzi baadhi hawajapata?
Name
Eng. Stella Martin Manyanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa katika nyakati tofauti tofauti ni kwamba kimsingi fedha kwa ajili ya mikopo kwa awamu hii zilishatolewa jumla ya shilingi bilioni 80 na tayari bajeti yake ipo sawa. Suala lililokuwa limetuchelewesha lilikuwa ni suala la uhakiki kwa misingi kwamba watu wanaohitaji mikopo sio wote watakaoweza kupata kwa sababu fedha ambayo inatolewa ni kwa ajili ya watu wale ambao hasa wana uhitaji wa kupita wenzao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hivyo nina maana kwamba tumeangalia mikopo tu, lakini Serikali kupitia Wizara ina majukumu mengine makubwa sana ya kuangalia mfano tumeona vijana wetu wengi walikuwa wanakaa katika maeneo ambayo walikuwa wakijipangia wenyewe, mabweni yalikuwa yanakuwa hayapo, vitendea kazi vingine vilikuwa viepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyoangalia katika utoaji wa elimu tunaangalia Nyanja zote na haswa katika kuona kwamba elimu inatolewa kwa kiwango kinachostahili na kwa haki inayostahili mwanafunzi kuipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo wale wote ambao wanastahili kupata mikopo kutokana na uhitaji uliopimwa, mikopo yao itapatikana, lakini hata hivyo lazima tuzingatie kwamba mikopo hiyo inamfikia mlengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini ndani ya wiki hii tutakuwa tumefikia mahali pazuri zaidi. Ahsante
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved