Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Suala la Mpango Miji ni jema na mtu aliyepimiwa ardhi na kupata hati ya eneo lake huweza kutumia hati hiyo kukopa kirahisi lakini gharama za kupima ardhi ni kubwa sana kiasi kwamba wananchi walio wengi wanashindwa kupima maeneo yao. Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kupunguza gharama za upimaji ardhi ili wananchi wengi zaidi waweze kupima maeneo yao na kuyaongezea thamani?
Supplementary Question 1
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naitwa Waitara, jina hili inabidi ulifahamu, jina rahisi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ameandika mwenyewe hapa kwamba gharama za upimaji ni shilingi 300,000 lakini mimi niliwaita hawa wahusika nikataka wanipimie eneo langu ambalo halifiki ekari mbili, wakafanya tathmini na wakaniambia natakiwa nilipe shilingi milioni tano, kwa hiyo nikapiga mahesabu wananchi wangu ambao wananizunguka pale Kivule na maeneo mengine wanawezaje kumudu hizo gharama kubwa za kupimiwa maeneo yao?
Kwa hiyo naomba kwanza anisaidie, gharama nilizopewa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ni milioni tano kwa eneo langu chini ya ekari mbili, yeye anasema hekta moja ni shilingi 300,000, na nini kauli yake sasa kwa maana ya maelekezo nchi nzima juu ya hili la upimaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika maelezo yake Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba mimi nimeuliza swali langu ni hatua gani za dharura kwa sasa kwa sababu migogoro mingi ya ardhi iliyopo nchi nzima ni kwa sababu maeneo hayo kwa sehemu kubwa hayajapimwa na ikiwemo Dar es Salaam na watu wanasogeza mawe, kunakuwa na ugomvi mkubwa na kuna kesi nyingi katika mabaraza ya ardhi. Sasa nikataka mkakati wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anasema wana mpango wa kusogeza huduma, sasa naomba anisaidie, huu mpango walionao kuna bajeti yoyote ambayo imetengwa? Kwa sababu wakisema halmashauri inunue vifaa hivi ambavyo yeye mwenyewe amesema ni gharama, kama Waziri anakiri kwamba gharama ya vifaa vya upimaji wa ardhi ni kubwa Halmashauri ambayo haina fedha na imeomba fedha kutoka kwenye Bunge hili na Serikali hawajapeleka mpaka leo, hali ni mbaya, wao Serikali kwa maana ya hii Wizara wanasaidia nini katika mpango wa dharura kwa sasa ili huduma hizi ziweze kupatikana katika maeneo husika? Ahsante.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza maswali mawili, jambo la kwanza amesema, nimetaja kwamba gharama za upimaji ni 300,000 kwa hekta. Naomba niseme hizo ndizo gharama sahihi ambazo tulipitisha hapa kwenye kikao baada ya kupunguzwa ile awali iliyokuwa shilingi 800,000 na Bunge hili lilipitisha baada ya Mheshimiwa Waziri kuleta katika bajeti yake na kuomba ipunguzwe. Sasa kama Manispaa inatozo lingine tofauti na wewe ni mmojawapo katika Manispaa hiyo, ni vizuri pia kujua kwa sababu officially tunachojua na kiko katika maandishi ni shilingi 300,000 lakini kama Halmashauri huwa wana mipango yao kule kutegemeana na Baraza lenyewe la Madiwani wameridhia nini katika lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu kuna mambo mengine ambayo yanafanyika ndani ya Halmashauri kutegemeana na mamlaka walizonazo, lakini katika rate offial zilizoko ni shilingi 300,000 kwa hekta moja na ni shilingi 300,000 hiyo hiyo kwa kiwanja kimoja. Sasa pengine itabidi tuwasiliane kuweza kujua kwanini wanatoza shilingi milioni tano kwasababu zipi za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ameongelea habari ya harakati zipi za dharura ambazo tunazifanya ili kupunguza hilo na ni bajeti gani imetengwa. Naomba niseme; bajeti tuliyopitisha hapa Wizara ilileta bajeti ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya kununua vifaa hivyo na tayari mchakato wa kununua umeshaanza na kwa sababu uko chini ya Benki ya Dunia ambao ndio wafadhili, mchakato ndani ya Wizara tumeshamaliza, tunachosubiri tu ni ile no objection kutoka Benki ya Dunia, wakishapitisha sisi hatuna tatizo kwasababu tayari ipo na tulisema itakwenda katika kanda zote nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, harakati za dharura ambazo tunafanya sisi ndiyo katika hizo lakini bado tulishasema kuna makampuni zaidi ya 58 ambayo yapo na Halmashauri inaweza kuyatumia, Wizara imesharidhia yafanye kazi hiyo ili kuondokana na tatizo hili. Kama Wizara tunafanya kazi ya urasimishaji katika maeneo ambayo hayako vizuri, kwahiyo hilo naweza kujibu kuwa ndizo hasa harakati zetu tunazofanya kuhakikisha tatizo hilo linaondoka.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved