Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Primary Question

MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:- Majibu ya Serikali ya Swali Na.1 la tarehe 6 Septemba, 2016 yanapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli aliyoitoa wakati akiwa kwenye kampeni katika Jimbo la Solwa:- (a) Je, kwa nini Serikali inapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais? (b) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya?

Supplementary Question 1

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nashukuru sana kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri yenye matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Solwa na hasa Hospitali yetu ya Wilaya katika Kata hii ya Salamagazi, Makao Makuu ya Wilaya yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali hii imechukua muda mrefu, sasa imefika miaka karibu sita na nguvu ya Halmashauri yetu ilifika mahali ikawa haiwezekani kuikamilisha; na kwa kuwa tumeomba fedha hizi kwa muda mrefu; na kwa kuwa Serikali sasa imeahidi kulikamilisha: Je, fedha tunazozihitaji tunaweza tukazipata zote katika bajeti hii inayokuja ya 2017/2018? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri, Jafo mdogo wangu, namwamini, naiamini Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, yeye mwenyewe na Serikali yake yote kwa ujumla, anaweza akawa tayari kuja kutembelea hospitali hii akajionea hatua na nguvu ya Halmashauri yetu tuliyoiweka na kwa nini tunaomba fedha hizo ili Hospitali yetu ya Wilaya iweze kukamilika na kutoa huduma kwa wananchi wetu wa Jimbo la Solwa?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Ahmed kwa sababu amekuwa akizungumzia sana hospitali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme wazi kwamba nami nilifika katika Mkoa wa Shinyanga, nimebaini changamoto zinazoukabili mkoa huu, hasa ukiangalia kwanza pale tuna Hospitali ya Mkoa, lakini ukiangalia katika eneo hili la Shinyanga Vijijini hakuna hospitali ambayo itaweza ku-accommodate idadi kubwa sana ya watu. Kwa hiyo, kinachotokea ni kwamba, wagonjwa wengi sana wanakwenda pale katika hospitali ile. Kwa hiyo, ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika mpango huu wa bajeti ya mwaka huu wa fedha tutahakikisha kwamba, zile shughuli za awali za kuhakikisha kwamba hospitali inasimama, tutajikita nazo hizo. Naomba nimtoe hofu kabisa, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo. Leo hii asubuhi nilikuwa nafanya mawasiliano na Mkurugenzi kule Shinyanga Vijijini kuona jinsi gani wanajipanga na kuwapa agizo na sisi huku Serikali Kuu tuweke nguvu ya pamoja ili wananchi wa eneo hili waweze kupata huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kiujumla ni kwamba Serikali itajitahidi kwa kadri iwezekanavyo; na katika mchakato wa bajeti nami nitatoa kipaumbele sana kwa sababu nimefika eneo lile, nimebaini changamoto na Mheshimiwa Mbunge muda mrefu alikuwa analipigia kelele eneo hili, lakini kwa bahati nzuri ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo wananchi wana imani kubwa katika hilo na kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameahidi, lazima litekelezwe. Ni jukumu letu sisi Serikali kuhakikisha tunafanya, tusimwangushe Mheshimiwa Rais, ahadi ile iweze kutekelezeka na wananchi wapate huduma ya afya iliyo bora.

Name

Saumu Heri Sakala

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:- Majibu ya Serikali ya Swali Na.1 la tarehe 6 Septemba, 2016 yanapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli aliyoitoa wakati akiwa kwenye kampeni katika Jimbo la Solwa:- (a) Je, kwa nini Serikali inapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais? (b) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya?

Supplementary Question 2

MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la kuuliza.
Katika Kijiji cha Ushongo kilichopo Wilaya ya Pangani, wakazi wake wamejitahidi kujenga jengo la zahanati kadri ya walivyoweza hadi kufikia kiwango cha lenta, lakini kulikuwa na ahadi kuwa Serikali itamalizia jengo hilo pamoja na kuleta huduma muhimu ikiwemo wahudumu pamoja na dawa, mpaka sasa Serikali bado haijatimiza ahadi hiyo ikiwa ni takriban miaka mitatu sasa. Sasa Serikali itatimiza lini ahadi yake hiyo, hasa ukizingatia kijiji hicho hakina huduma ya usafiri wa umma? Wanatumia boda boda na gari za kukodi. Nashukuru sana.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tumesikia suala hili, ndiyo maana hapa katikati tulizungumza kwamba tunafanya tathmini ya maeneo yote kwa majengo ambayo yamejengwa hayajakamilika na katika upande wa zahanati, tuna takribani zahanati 1,358 ambazo ukiangalia tuna bajeti siyo chini ya shilingi bilioni 78 kuweza kumaliza shughuli hizi zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba tulifanya assessment ile ili tuweze kujua nini tunatakiwa tukipange katika mpango wa bajeti tuweze kuondoa haya maboma na kujali juhudi kubwa zilizofanywa na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Saumu na Waheshimiwa Wabunge wote, katika suala zima la magofu ambayo hayajakamilika yale ya zahanati na vituo vya afya sambamba na hospitali zetu za wilaya, tunaweka mpango mkakati kabambe ambapo tutawaomba Waheshimiwa Wabunge katika mchakato wa bajeti mtuunge mkono ilimradi tuweze kuondoa hivi viporo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini tukifanikiwa hata kwa asilimia 60 kwa hivyo viporo ambavyo vipo site huko, tutakuwa tumewezesha kwa kiwango kikubwa kuwapatia wananchi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania afya bora na miundombinu ya ujenzi wa zahanati. Ahsante.