Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Askari Magereza katika Mji wa Tarime wamekuwa wakilalamika kuwepo kwa mlundikano wa mahabusu ndani ya Gereza la Mji wa Tarime. Hii inatokana na mlundikano wa kesi ndani ya Mahakama ya Wilaya kwa kigezo cha upelelezi kutokamilika:- (a) Je, kwa nini kesi zenye vigezo vya dhamana watuhumiwa wasipewe dhamana ili kupunguza mlundikano wa mahabusu na gharama kwa Serikali? (b) Je, nini mkakati mahususi wa Serikali katika kuhakikisha Jeshi la Polisi linamaliza upelelezi kwa wakati ili kuweza kupunguza mlundikano? (c) Je, ni hatua gani zinachukuliwa kwa Askari Polisi ambao wanawabambikia kesi wananchi na kupoteza nguvu kazi za Taifa kwa kuwafanya wananchi waishi Gerezani?

Supplementary Question 1

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya Tarime Mjini yanafanana kabisa na Gereza la Bariadi Mjini, msongamano wa wafungwa. Naomba niulize kuwa Mheshimiwa Waziri alifika katika Gereza la Bariadi Mjini, hali halisi aliiona jinsi ambavyo wamesongamana hawa watu na Gereza hili linatumika kwa Wilaya zote tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inajenga Gereza ambalo lina hadhi ya Kimkoa? Kwa sababu kesi nyingine zinasababishwa na Jeshi la Polisi kuwabambikizia watu kesi, wakiwemo Madiwani wa Wilaya ya Itilima, Wenyeviti wa Vijiji, Kiongozi Naibu Katibu Mkuu CHADEMA ambaye alishikiliwa takriban siku 12 bila sababu za msingi akiwa na vijana…

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea pendekezo ama ombi la Serikali kuangalia upya mazingira ya Gereza la Bariadi, nami nilifika, kuna mambo ya kufanyia kazi pale na sisi kama Wizara tume-earmark kwamba kuna jambo la kufanyika ukianzia na nafasi yenyewe ya Gereza, lakini pia na ngome/kuta kwa ajili ya Gereza. Kwa hiyo, hilo tumelipokea.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, sisi ni viongozi. Mimi nimetembelea Magereza, nimeongea na wafungwa na mahabusu. Wale watu ukifika katika mikoa yote nilikotembelea ni mmoja tu ambaye nilipomwuliza kama umefanya kosa ama hukufanya akasema nimefanya. Wengine wote ukiwasikiliza, kama una fursa ya kuwatoa, unaweza ukawatoa dakika hiyo hiyo, wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nimekuja kupeleleza baada ya hapo, napeleleza mmoja mmoja; ukipeleleza mmoja mmoja utakuta makosa aliyofanya ni ya kupindukia. Kwa maana hiyo, tunapokuwa tunasemea kwa ujumla wake kwamba Polisi wanabambika kesi, nadhani tuwaamini kwamba wale ni Watanzania ambao wanafanya kazi kwa kiapo. Kama kuna jambo la mtu mmoja mmoja, hayo ndiyo kama viongozi tuyafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie kule Magerezani, chukueni muda Waheshimiwa Wabunge; ninyi ni viongozi, nendeni mkawasikilize. Ukiwasikiliza wote unaweza ukadhania Gereza hilo limeshika malaika, lakini ukifuatilia undani wake utaona mambo mabaya waliyoyafanya katika familia nyingine ambayo wanastahili kwa kweli kuwa katika maeneo hayo.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Askari Magereza katika Mji wa Tarime wamekuwa wakilalamika kuwepo kwa mlundikano wa mahabusu ndani ya Gereza la Mji wa Tarime. Hii inatokana na mlundikano wa kesi ndani ya Mahakama ya Wilaya kwa kigezo cha upelelezi kutokamilika:- (a) Je, kwa nini kesi zenye vigezo vya dhamana watuhumiwa wasipewe dhamana ili kupunguza mlundikano wa mahabusu na gharama kwa Serikali? (b) Je, nini mkakati mahususi wa Serikali katika kuhakikisha Jeshi la Polisi linamaliza upelelezi kwa wakati ili kuweza kupunguza mlundikano? (c) Je, ni hatua gani zinachukuliwa kwa Askari Polisi ambao wanawabambikia kesi wananchi na kupoteza nguvu kazi za Taifa kwa kuwafanya wananchi waishi Gerezani?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kiukweli majibu ya Mheshimiwa Waziri yapo kiujumla zaidi na inasikitisha kwa sababu tunapokuwa tunatoa maswali yetu tunatarajia mwende sehemu husika kujua uhalisia wa sehemu husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mahabusu waliopo Gereza la Tarime, zaidi ya asilimia 65 ni kesi au makosa ambayo yanatakiwa yapewe dhamana; na kwa kuwa kesi nyingi ni kesi za kisiasa za kubambikwa na nyingine ni kesi za watoto chini ya miaka 15; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alikuja Tarime na hakupata muda wa kuingia Gerezani, ningependa sasa leo mtuambie ni lini Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkurugenzi wa Mashtaka watakuja Tarime kuangalia hali halisi ya mahabusu walioko Gereza la Tarime ili waweze kuondoa zile kesi ambazo jana Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba nyingine ni za juice, ili Watanzania warudi uraiani na wafanye kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kuna msongamano mkubwa sana kwenye Gereza la Tarime, capacity yake ilikuwa ni watu 260 wakiwa wamezidi sana. Sasa hivi ni zaidi ya watu 600; na kwa kuwa ukitokea mlipuko wa magonjwa tutapoteza Watanzania wengi waliopo kwenye lile Gereza; na kwa kuwa gereza lile linahudumia Wilaya ya Rorya na Tarime: ni lini sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi mtajenga gereza katika Wilaya ya Rorya, mtajenga Mahakama ya Wilaya kule Rorya ili wale Watanzania wa Rorya waweze kushtakiwa kule na kuhudhuria kesi zao kule ili kuondoa msongamano ambao upo katika Gereza la Tarime?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwape pole timu yangu ya Magereza (Tanzania Prisons) kwa kushindwa jana kwa figisu za Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda zilipocheza na Ndanda. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mkuu na Wizara ya Katiba na Sheria tutalifanyia kazi jambo hilo; huo ni wajibu wetu na tumekuwa tukifanya hivyo. Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria ameshafika Mkoa wa Geita, ameshafika Mkoa wa Mwanza, Mkoa wa Kagera na anakuwa na Ofisi ya DPP na anakuwa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani. Nikubaliane nalo, hilo tutafanya, ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba wale ambao kwa kweli wanaweza wakapata namna ya kwenda nje waende nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitofautiane na Mheshimiwa Mbunge kwenye takwimu, anasema asilimia 75 ya kesi ni za Wanasiasa. Natofautiana naye kwa sababu amesema asilimia 75 ni za wanasiasa na wakati ule ule ni za watoto. Huwezi ukawa na asilimia 75 ya wanasiasa na watoto. Kwa hiyo, kwenye hilo siyo kweli na kama kuna issue specific ya kesi ya mtu mmoja mmoja, Waheshimiwa Wabunge ninyi ni Viongozi, tusaidiane kupeana taarifa ili tuweze kufanya intervention inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kujenga gereza Rorya hata Mheshimiwa Mbunge wa Rorya amelisema mara nyingi na ameongelea matatizo wanayopata wananchi wake. Ni kweli wanapata shida kwa sababu mashahidi wanatakiwa kutoka Rorya na ni gharama hata kwa Serikali kuwatoa watu Wilaya nyingine kwenda kutoa ushahidi katika Wilaya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo tumelipokea na kama Serikali tunachukua hatua kwa Wilaya zote mpya ambazo zimeanzishwa, ambazo bado hazina huduma hizo za Mahakama pamoja na Magereza, kuhakikisha kwamba tunawapunguzia usumbufu wananchi na sheria iweze kuchukua mkondo wake kwa wakati.