Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Msitu wa Shagayu ndio wenye vyanzo vingi vya mito katika Jimbo la Mlalo, msitu huu uliungua takribani hekari 49 mwaka 2012:- Je, ni lini Serikali itapanda miti katika eneo lililoungua ili kulinda vyanzo vya maji?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, japo hayaridhishi sana, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa miti ya asili huwa ukuaji wake siyo wa kasi na wameshaanza kupanda miti katika hizi hekta 11, kwa nini wasione umuhimu wa kumalizia hizi hekta 38 ili ku-cover eneo hili la msitu kwa sababu msitu huu una vyanzo zaidi ya vinne vya mito ambayo inatiririsha maji kuelekea katika mbuga ya Mkomazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mvua za mwaka jana, zilisababisha uharibifu mkubwa kutokana na maporomoko yaliyosababisha uoto wa msitu kupotea, hivyo kusababisha uharibifu mkubwa katika barabara za Kata ya Shagayu, Mbaramo na Sunga. Je, Wizara haioni sasa kuna umuhimu wa kipekee wa kuwaunga mkono wakazi wa maeneo haya ili kuweza kuboresha miundombinu hii ya barabara iweze kusaidia hata wakati mwingine wanapakuwa na dharura za moto waweze kufika katika eneo husika kwa haraka zaidi?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kutambua kwamba misitu inachangia kiasi kikubwa au ndiyo msingi kwa kweli wa kuweza kuboresha vyanzo vya mito. Ana mito minne, na kwamba yote minne chanzo chake kikubwa ni misitu hii tunayoizungumzia.
Kwa hiyo, kwa kutambua hivyo nampongeza lakini nataka elimu hiyo pia aweze kuifikisha kwa wananchi kwenye eneo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali kwa nini sasa tusipande miti kwenye lile eneo ambalo lina hekta 38 tulizosema tuache miti ikue kwa utaratibu wa asilia. Kwanza, nimfahamishe tu kwamba, mimea ikiwemo hiyo miti kwa kawaida huwa kuna mimea ambayo ni rafiki kukua pamoja na mimea mingine si rafiki kukua kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo lake siyo baya lakini tunapaswa kufanya kwanza utafiti wa kitaalam, na nitafanya utaratibu wa kufika kwenye eneo lile na wataalam ili tuweze kuona miti iliyopo ni miti gani inayotakiwa kukua asilia, halafu tuone kama kuna miti rafiki inayoweza kupandwa ilimradi tusichague miti ambayo itaathiri ile miti ambayo inatakiwa kukua asilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, uwepo wa barabara ambazo zinasaidia kutumika wakati wa dharura za moto na matumizi mengine ambayo ni rafiki kwa utunzaji wa misitu.
Kwanza ni dhahiri kwamba hiyo pia ni interest yetu pia sisi kama Serikali, lazima tuwe na barabara ambazo zinaweza kutusaidia wakati wa dharura kama moto utatokea, na kuwa ni jukumu letu kushirikiana na wananchi, na mamlaka za Wilaya zilizopo kuweza kuhakikisha kwamba barabara hizi zinatengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la kuangalia hali ya kibajeti, lakini pamoja na hayo katika safari hiyo nitakayokwenda nitakwenda pia kuangalia hali ya barabara na kuweza kuona namna gani tunaweza kuweka kwenye mipango yetu.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Msitu wa Shagayu ndio wenye vyanzo vingi vya mito katika Jimbo la Mlalo, msitu huu uliungua takribani hekari 49 mwaka 2012:- Je, ni lini Serikali itapanda miti katika eneo lililoungua ili kulinda vyanzo vya maji?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Kwa miaka mingi sana nchi yetu imekuwa ikihamasisha sana utalii kupitia Mbuga zetu za Wanyama, Mlima wetu na Mapori yetu, lakini nchi ina vivutio vingi sana. Sasa nauliza; je, Wizara ina mpango gani wa kujenga makumbusho ili vizazi vyetu viweze kujionea jinsi Machifu wetu kwa mfano Mirambo, Mkwawa, kule Kilimanjaro, Mshumbue Marialle ambao walifanya vitu vingi na kuna vitu vingi vya asili vinavyoweza kuvutia utalii, kule Kusini, Wilaya ya Kilwa ni Wilaya ya zamani sana elfu moja mia nane na kitu, lakini vivutio vyote hivi havizungumzwi.
Je, Wizara ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inajenga makumbusho ili vivutio hivi viweze kuwa kwa faida ya watoto wetu kwa kujifunza na vilevile kutuingizia fedha kutokana na watalii kutoka nje?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze kwa kuweza kutupa hamasa sisi Serikali, hasa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kuongeza jitihada kwenye Sekta hii ya Utalii. Ni kweli na nipende tu kusisitiza kwamba, majukumu manne makubwa ya Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na utalii wenyewe ni misitu, wanyamapori na malikale.
Makumbusho anayozungumzia Mheshimiwa Mbunge yanaangukia kwenye sehemu ya malikale na imo kwenye sera zetu kwamba tunapaswa kuboresha makumbusho maeneo yote ya kihistoria popote pale yalipo ili tuweze kuyatangaza na kuweza kuwafanya watalii waweze kuyafikia pamoja na kutupatia pesa, lakini pia kuweza kutangaza utamaduni wa Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya kwa sasa tumeanza kuorodhesha katika ngazi ya Wizara, pia hivi karibuni tunasambaza barua kwa Halmashauri za Wilaya zote ili waweze kutuambia kwa sababu wao wanafahamu vizuri maeneo hayo halafu tutakwenda kuyakagua kuona kama yatakidhi vigezo vya kuweza kuyafanya kuwa ni maeneo ya utalii.

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Msitu wa Shagayu ndio wenye vyanzo vingi vya mito katika Jimbo la Mlalo, msitu huu uliungua takribani hekari 49 mwaka 2012:- Je, ni lini Serikali itapanda miti katika eneo lililoungua ili kulinda vyanzo vya maji?

Supplementary Question 3

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, upandaji wa miti ndiyo hasa unaoleta uoto wa asili; Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wananchi wa Lushoto katika upandaji wa miti hasa maeneo ya msitu wa Magamba, Mazumbai ili kurudisha uoto wa asili uliotoweka?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea wazo lake na kwa kweli ni msisitizo kwa kile ambacho Serikali inakifanya, lakini na yeye sasa nimwombe arudi kule kwa wananchi aanze kuwashawishi kwa kuwaelewesha kwanza umuhimu wa misitu, lakini pia kuwafanya wajipange kwa ajili ya kupanda miti ili kuungana na jitihada za Serikali ambazo tayari zipo kwenye mipango.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishatoa maelekezo kwa Wilaya na Mikoa yote kwamba kila Wilaya inalazimika kupanda miti 1,500,000. Kabla ya msimu wa kuanza kupanda kila Wilaya, sasa inawajibika kuhakikisha kwamba inaandaa mbegu, vitalu na kuhakikisha kwamba miche ya kupanda kila eneo inapatikana. Kwa sasa hivi sisi Wizara tunahakikisha tunawapelekea maelekezo ya kila eneo miti gani inayoota na inayoweza ku-survive bila matatizo. Kwa hiyo, kila Wilaya wanalo jukumu hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ndani ya Wizara ya Maliasili pamoja na hii Ofisi ya Mazingira kwa maana ya Ofisi ya Makamu wa Rais, tutaendelea kusaidia pale inapobidi lakini ni mkakati wa kila Wilaya na Mkoa kuhakikisha kwamba kila Wilaya inapanda miti hiyo kwa mwaka inapofikia kipindi husika.