Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Primary Question
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:- Serikali ilielekeza nguvu zake katika kutangaza vivutio vya utalii na wawekezaji kuja Kanda ya Kusini ili kupunguza msongamano wa utalii Kaskazini mwa Tanzania:- (a) Je, ni kwa kiasi gani Serikali imeyatangaza maporomoko ya Kalambo ambayo ni ya pili Afrika baada ya yale ya Victoria kuwa kivutio cha utalii? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Hifadhi ya Msitu wa Kalambo pamoja na maporomoko haya yanakuwa chini yake kupitia Shirika lake la TANAPA?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali ambayo kimsingi sijaridhika sana, naomba kwanza niifahamishe Serikali kwamba maporomoko ya Kalambo ni ya pili Afrika yakifuatiwa na maporomoko ya Victoria. Kwa hiyo, yana unyeti na upekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuifahamisha Serikali, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mazungumzo yalikuwa yameshaanza kati ya Halmashauri ya Kalambo na TANAPA wakijua umuhimu wa maporomoko haya. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuhakikisha kwamba anayasukuma mazungumzo haya na ili maporomoko ya Kalambo yapandishwe hadhi na kuchukuliwa na TANAPA? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa maporomoko ya Kalambo yapo mpakani mwa Tanzania na Zambia na wenzetu wa upande wa Zambia wamekuwa wakiyatumia na kuyatangaza maporomoko haya na wakinufaika pamoja na kwamba scenery nzuri iko upande wa Tanzania. Je, Serikali iko tayari kuweka mkakati mahsusi kuhakikisha kwamba maporomoko haya yanafanyiwa promotion ya pekee?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza la mazungumzo yaliyokwishafanyika awali kati ya TANAPA na Halmashauri ya Wilaya inayohusika lakini akihusianisha na umuhimu wa maporomoko haya yakiwa ni ya pili kwa ukubwa na umaarufu katika Afrika, napenda niungane naye kusema kwamba mazungumzo yakianza ni sharti yakamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe pia kuhusu kuwa maporomoko haya ni ya pili kwa ukubwa na umaarufu Afrika, Wizara inayo taarifa hiyo. Hata hivyo, nimfahamishe tu kwamba, tukisema bado yatasimamiwa chini ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) haimaanishi kwamba tunayashusha hadhi wala haimaanishi kwamba tutapunguza kasi na nguvu ya kuyatangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa nimesema kwamba suala hili ni kwa mujibu wa sheria, Hifadhi za Taifa zina tafsiri yake kama ambavyo nimesema hapo awali na kwamba misitu ama maporomoko haya ambayo yapo ndani ya msitu tuliouzungumzia kwa mujibu wa sheria iliyopo sasa hivi yenyewe hayawezi kuwa Hifadhi ya Taifa kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikubaliane na Mbunge kwamba nakwenda kufanya rejea ya mazungumzo yaliyokwishafanyika kwamba nini kilizungumzwa, tuliamua nini hapo nyuma ili kutotoka nje ya mazungumzo, lakini kwa sasa hivi mpaka nitakapokwenda kuona mazungumzo hayo msimamo ni kwamba, Hifadhi za Taifa zitabaki kuwa Hifadhi za Taifa na misitu itabaki kuwa misitu na itasimamiwa kwa sheria zinazohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kuweza kufanya promotion ya pekee, hili nakubaliana nalo moja kwa moja na namwomba Mheshimiwa Mbunge nikitoka hapa hebu tukutane, inawezekana ana maoni mazuri zaidi kuliko hiki ambacho Serikali imefanya. Nakiri kabisa siyo tu kwa maporomoko haya bali kwa ujumla wake kutangaza vivutio vya utalii ni jukumu la Serikali na kwamba tunapaswa kuboresha namna ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote ili tuweze kufanya vizuri zaidi ili vivutio vyetu viweze kufikiwa na watalii kwa wingi na kuongeza pato la Taifa.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved