Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Primary Question

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Wananchi waliojenga nyumba katika maeneo ambayo hayajapimwa wanapopata kesi hasa kwenye Mahakama ya Wilaya wanatakiwa kutoa Hati au Ofa lakini kwa kukosa nyaraka hizo ndugu au jamaa wanakosa kudhaminiwa:- Je, Serikali haioni kuwa iko haja ya kupandisha thamani ya makazi ya wananchi hao?

Supplementary Question 1

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo bado hayajaridhisha sana kwa sababu maeneo mengi wananchi bado wanajenga kiholela. Wakishajenga kiholela baadaye ndiyo Serikali inajua kuwa hawa wamejenga kiholela wanaanza kuja kuwasumbua, kunakuwa hakuna barabara hata watu wakiugua kwa mfano akinamama wajawazito jinsi ya kutoka maeneo yale kwenda hospitalini inakuwa shida kwa vile usafiri hauingii katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaona jambo hili kuwa wananchi wanajenga kiholela na baadaye inakuwa shida na tabu, lini sasa itaweka mipango mikakati ya kuhakikisha inapima kwanza halafu inawagawia wananchi viwanja ili waweze kupata maeneo mazuri na yenye kupitika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa Manispaa ya Mpanda kuna migogoro mingi sana ya ardhi na nilishamwambia Waziri aje Mpanda kuona jinsi wananchi wanavyopata tabu. Je, ni lini sasa mimi na yeye tutaongozana kwenda Mpanda ili aende akatatue matatizo ya wananchi wa Mpanda?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameanza kwa maelezo na kusema kwamba Serikali inaacha watu wanajenga holela na baadaye inakuja kuwabomolea, lini itaweka mpango mkakati wa kupima ardhi yote? Kama Wizara tayari tumekwishaanza zoezi hili na tulilitambulisha pia wakati wa bajeti na tumeanza na Mkoa wa Morogoro katika zile Wilaya tatu za Ulanga, Kilombero na Malinyi. Huko ndipo tulipoanzia na uzoefu mzuri utaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hii haizuii Halmashauri kufanya mipango yake ya upimaji wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao. Kwa sababu kama itaachiwa Wizara peke yake haiwezi kupima kwa wakati na ikamaliza kwa nchi nzima hii. Ndiyo maana kama Halmashauri tunacho kitengo/idara yetu, mipango miji wako pale ambapo wanatakiwa pia kuangalia namna ya upangaji miji. Ndiyo maana sasa hivi tuna miji zaidi ya 33 ambayo wameandaa mipango yao kabambe ili kuweka miji salama. Vilevile ujenzi unafanyika kule kwenye Halmashauri zetu, kwa hiyo kama Halmashauri tunapaswa pia kulisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai tu kwamba zoezi hili tunapaswa wote kushirikiana kuweza kuangalia watu wanawezaje kuendeleza makazi yao vizuri na kwa kuzingatia sheria kwa sababu tuko nao karibu zaidi katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo, tunalichukua kama changamoto, lakini bado tunalirejesha kama changamoto pia kwenye Halmashauri zetu kuweza kusimamia matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao na kama mipango haijapangwa basi iweze kupangwa. Wataalam wa Wizara yangu wapo wanaweza wakasaidia kikanda kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuwaondolea wananchi hawa kero ambayo wanaipata pale ambapo wanabomolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ameongelea migogoro ya Mpanda na alitutaka twende. Nadhani tulizungumza kwamba migogoro iliyopo ni mingi na kama Wizara tumeipokea. Juzi wakati tunajibu swali hapa tumesema tunayo timu maalum inayoandaa tathmini ya ile migogoro. Kwa sababu unapofunga safari huwezi kwenda kufanya kazi ya mgogoro mmoja halafu ukarudi. Tunataka unapokwenda mahali uende ukaipitia migogoro yote iliyopo lakini pia uwe umeshapata ABCs za ile migogoro na chanzo chake, ukifika kule unatoa ufumbuzi wa kudumu na siyo kwenda tena halafu kurudi mara nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, zoezi hili la kwenda kwenye maeneo baada ya muda si mrefu tutawatembelea na tutafika kwa sababu timu inayoandaa tathmini ya ile migogoro na kuweka mapendekezo na kupitia zile taarifa za zamani za tume mbalimbali ili tuweze kuzifanyia kazi, karibu inakamilisha kazi yake na ikikamilika utaona tutafika na niko tayari kufika kwenye eneo lake.