Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Richard Phillip Mbogo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Primary Question
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:- Halmashauri ya Nsimbo imekuwa ikipokea wahamiaji toka mikoa mbalimbali ambao ni wakulima na wafugaji na kusababisha kukosa maeneo yenye rutuba. Je, ni lini Serikali itaongeza maeneo ya vijiji vilivyotangazwa mwaka 1974?
Supplementary Question 1
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kwanza naomba niseme, mimi nikiwa ni Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, nina masikitiko makubwa sana kuhusiana na uongozi wa Wilaya na Mkoa kwamba katika kutekeleza majukumu yao, hawaangalii haki za msingi. Tarehe 24 wamefanya operation ya kuondoa watu kwenye Hifadhi ya Kijiji ambao walipewa na uongozi wa Kijiji kwa kuwachomea nyumba, mvua zinanyesha, wanakosa pa kulala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii imekuwa ni tofauti na kauli ya Mheshimiwa Makamu wa Rais aliyotoa mwaka 2016 kwamba endapo watu wako katika maeneo ya hifadhi, wanatakiwa watafutiwe maeneo mengine na ndiyo wapelekwe. Kutokana na hilo, naomba kuuliza, je, Wizara husika iko tayari kuwafuta machozi wananchi wa Kitongoji cha Kamini, Kaumba katika Kijiji cha Katambike, Kata ya Ugala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ilitolewa taarifa hapa kwamba imeundwa tume ambayo inashirikisha Wizara karibu tatu kushughulikia kero za migogoro ya ardhi. Sasa tunaomba majibu ya hiyo tume, yamefikia wapi?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkoa ilifanya uchomaji wa nyumba kwa sababu hii taarifa kwetu sisi ni mpya, ni ngeni, naomba tulichukue hili kwanza kwa ujumla wake kwa sababu jambo hili maana yake ni haki za binadamu ambao saa nyingine wameathirika. Kwa hiyo, kama Ofisi ya TAMISEMI tunasema kwamba habari hii kwanza tumeipata, tutaifanyia kazi kwanza, lakini suala zima la ulipaji wa fidia kwa wale walioathirika kwa Wizara yenye dhamana kwa sababu jambo hili, sijajua, ni jambo mtambuka. Je, iliyohusika ni Wizara ya Maliasili na Utalii au Ofisi ya Rais - TAMISEMI?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimesema jambo hili kwanza lazima lifanyiwe tafiti ya kina kujua nini kilichojiri kule katika eneo hilo. Pia kuna suala zima la kikosi kazi kilichoundwa na Wizara takriban nne, je, kimefikia wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kazi ile inaendelea hivi sasa, tukijua kwamba tuna changamoto kubwa sana nchini mwetu. Leo hii mikoa mbalimbali, ukiangalia Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani na karibu katika maeneo yote kuna tatizo hilo kubwa sana. Ninaamini kabisa kikosi hicho kinaendelea na kazi hiyo na pindi taarifa hiyo itakapokuwa imekamilika ambapo aliyehitaji jambo hilo lifanyike ni Waziri Mkuu mwenyewe, basi tutapata taarifa rasmi ya Kiserikali kuhusiana na jambo hili linavyoshughulikiwa katika maeneo mbalimbali, lakini kujua ukubwa wake maana yake tunataka kuokoa Taifa hili kwa sababu sasa hivi janga la mauaji limekuwa kubwa sana, na huu ndiyo suluhu ya jambo hili kwa sababu kila eneo sasa hivi lina shida kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Richard Mbogo naomba tuvute subira tu, taarifa hii ikikamilika itatolewa rasmi hapa katika Bunge letu.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa majibu yake mazuri, lakini nilipenda tu kuongeza jibu kwa hoja ya msingi aliyokuwa ameuliza kwenye swali la nyongeza kwamba ile Kamati iliyoundwa mpaka sasa hivi imefanya kazi wapi na wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ile Kamati mpaka sasa imeshakwenda mikoa minne; imekwenda Geita, Kagera, Morogoro na Tabora. Wakimaliza hapo, wanaelekea Kaskazini. Kwa hiyo, ile Kamati tayari imeshaanza kazi yake, lakini pia sisi ndani ya Wizara tumeshaanza kazi hiyo katika kufuatilia. Ni juzi tu nilikuwa Kusini na Waziri wangu alikuwa Kaskazini. Kwa hiyo, tunaendelea na kazi hiyo.
Name
Julius Kalanga Laizer
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Primary Question
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:- Halmashauri ya Nsimbo imekuwa ikipokea wahamiaji toka mikoa mbalimbali ambao ni wakulima na wafugaji na kusababisha kukosa maeneo yenye rutuba. Je, ni lini Serikali itaongeza maeneo ya vijiji vilivyotangazwa mwaka 1974?
Supplementary Question 2
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna Kamati Maalum iliyoundwa kwa ajili ya kushughulikia matatizo hayo na wakati huo huo Kamati inavyoendelea na kazi yake, Serikali imeendelea kuwaondoa wafugaji na kutaifisha mifugo yao, je, haioni ni wakati muafaka wa kusubiri Kamati hiyo imalize kazi yake ili waje na suluhu ya kudumu juu ya jambo hili?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema, Kamati iko site, lakini sijajua kwa sababu wakati mwingine kuna case by case.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine haya mambo yanatofautiana mazingira kwa mazingira; na kwa sababu katika maeneo mbalimbali tuna Wakuu wetu wa Mikoa ambao wapo; na ni viongozi Wakuu wa Kamati za Ulinzi na Usalama wa Mikoa hiyo, hali kadhalika na Wakuu wa Wilaya, mambo haya wakati Kamati inafanya kazi wao watapima uzito wa maeneo haya na kuona jinsi gani ya kufanya ili utaratibu uende vizuri. Lengo kubwa ni kumsaidia Mtanzania katika mazingira yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kwa sababu tuna Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na Kamati inaendelea kufanya kazi, nawaomba Wakuu wa Wilaya kuratibu mambo haya katika maeneo yetu na mikoa yetu. Jambo kubwa ni kuwalinda wananchi wetu waweze kuishi kwa usalama ili kujenga uchumi wa nchi yetu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved