Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Oliver Daniel Semuguruka
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:- Mkoa wa Kagera umezungukwa na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda na mipaka ya nchi hizo imekuwa adhabu kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera, kwani hali ya usalama wa raia na mali zao umekuwa mashakani kutokana na kuvamiwa na majambazi toka nje ya Tanzania wakishirikiana na baadhi ya Watanzania wasio na uzalendo na Taifa lao. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuimarisha ulinzi katika mipaka hiyo ili wananchi wa Mkoa wa Kagera waweze kuishi kwa amani na utulivu?
Supplementary Question 1
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Jeshi la Polisi lina uhaba wa vitendea kazi vya kisasa kuweza kudhibiti matukio ya uhalifu; je, Serikali ina mpango gani kutoa vifaa vya kisasa zaidi kwa askari wetu waliopo katika maeneo ya mipakani?
Swali langu la pili; ili askari aweze kufanya kazi zake na kudhibiti matukio ya uhalifu kwa ufanisi ni muhimu akawa na mazingira rafiki kuanzia nyumbani.
Je, ni lini Serikali itatekeleza kwa vitendo ahadi ya kujenga makazi ya hadhi ya askari wa Jeshi la Polisi katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera?
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa na concern ya hali ya usalama katika mpaka wa Kagera, lakini naomba tu nimthibitishie kwamba, si Jeshi la Polisi ama Serikali kupitia Jeshi la Polisi kwa kutambua umuhimu na unyeti wa maeneo ya nchi yetu yaliyoko mipakani ikiwemo Kagera huwa kwa kawaida inatoa kipaumbele katika ugawaji wa vifaa katika maeneo hayo hususan vitendea kazi ikiwemo silaha, magari na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni kwamba, kwa Mkoa wa Kagera pekee tunahakikisha kwamba tunawapatia Askari wetu walioko mipakani silaha za kutosha lakini silaha nzito ili kuweza kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu ambao mara nyingi wamekuwa wakisababisha ukosefu wa amani katika mikoa yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hakuna hata Kituo kimoja cha Polisi katika mipaka ya nchi yetu ambacho hakina gari mpaka sasa hivi tunavyozungumza. Kwa hiyo, ni kuonesha kwamba tunatoa nguvu kubwa sana na kipaumbele katika maeneo ambayo yapo mpakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili ni kweli kuna matatizo ya makazi, sio tu Kagera lakini katika mikoa mbalimbali nchi nzima na ndiyo maana tumekuwa tukizungumza hapa kuna mipango ya Serikali ya ujenzi nyumba 4,136 ambayo mpaka sasa hivi tunasubiri approval kutoka Hazina ili mradi ule uanze kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kagera, kuna ujenzi wa nyumba 12 ambazo tunaendelea nazo hatua kwa hatua kadri ya pesa zitakazopatikana tumalize katika eneo la Buyekera ambalo litasaidia kupunguza makali ya matatizo ya makazi kwa askari wetu.
Name
Alex Raphael Gashaza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Primary Question
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:- Mkoa wa Kagera umezungukwa na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda na mipaka ya nchi hizo imekuwa adhabu kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera, kwani hali ya usalama wa raia na mali zao umekuwa mashakani kutokana na kuvamiwa na majambazi toka nje ya Tanzania wakishirikiana na baadhi ya Watanzania wasio na uzalendo na Taifa lao. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuimarisha ulinzi katika mipaka hiyo ili wananchi wa Mkoa wa Kagera waweze kuishi kwa amani na utulivu?
Supplementary Question 2
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ni majibu ya Serikali. Lakini kwa kuzingatia kwamba Ngara ni miongoni mwa Wilaya za Mkoa wa Kagera, Wilaya inayopakana na nchi mbili, Rwanda na Burundi imekuwa ni waathirika wakubwa sana wa hali ya usalama katika eneo hilo. Sasa swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanzisha Kanda Maalum ya kipolisi kwa Wilaya hii ya Ngara ambayo kwa muda mrefu wamekuwa ni waathirika wa hali ya usalama? Ahsante.
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa tukiangalia maeneo ambayo yamekuwa na changamoto kubwa sana za kiusalama nchini mwetu na maamuzi ya kuongeza Wilaya katika maeneo hayo yanatokana na wingi wa matukio ya uhalifu. Ngara ni moja kati ya sehemu ambayo kuna matukio ya uhalifu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, hasa kutokana na kupakana na nchi jirani. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge atuachie hili tunalifanyia kazi na baadaye pale ambapo hatua itakapofikiwa, tutamjulisha.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved