Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Primary Question

MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:- Ujenzi wa Maabara za Shule za Sekondari Wilaya ya Serengeti umeshakamilika kwa kiwango kikubwa lakini maabara hizo zimebaki kuwa makazi ya popo:- Je, ni lini Serikali italeta vifaa vya maabara kama ilivyoahidi?

Supplementary Question 1

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Serengeti kwa kujitahidi kukamilisha vyumba vya maabara kwa asilimia 81.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wamekamilisha kwa asilimia 81, Mheshimiwa Naibu Waziri uko hapa na umekuja pale Jimbo la Serengeti na umeona hali ilivyo; kwa kuwa wananchi hawa wamejitahidi kwa hali hii. Je, Serikali kupitia hizi fedha za P4R mko tayari kukamilisha hivi vyumba 12 ambayo ni sawa na asilimia 19? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa ujenzi wa maabara ulipaswa pia kuendana na upungufu wa vyumba vya madarasa: Je, kupitia hizi pesa za P4R, mko tayari kupeleka sehemu ya fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa?
Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niwapongeze kwa kazi kubwa waliyoifanya; na kama kuna deficit ya vyumba 12, niseme kwamba Serikali tutashirikiana, siyo na watu wa Serengeti peke yake, isipokuwa jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunapata maabara katika kila sekondari zetu zilizokamilika. Ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge nilikwambia hiyo juhudi iendelee, lakini Serikali na sisi tutatia nguvu yetu kuhakikisha maeneo yote yale ya Serengeti yanapata maabara kama tulivyokusudia.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimezungumza hapa kwamba tumetenga karibu shilingi bilioni 16. Lengo ni kwamba zile maabara ambazo wananchi wamejitolea kwa nguvu kubwa kuzijenga, lazima ziwe na hivyo vifaa. Kuanzia mwezi Machi mpaka mwisho wa mwaka hapa tutajikuta tumekamilisha suala zima la maabara siyo Serengeti, lakini katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, suala zima la ujenzi wa vyumba vya madarasa, ni kweli. Tuna changamoto ya vyumba vya madarasa katika maeneo mbalimbali ikiwepo kwako Serengeti, nami nakupongeza sana, nilikuwa nawe siku ile. Tutajitahidi.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka huu ukiangalia katika michakato mbalimbali, tulikuwa na madarasa ambayo yapo katika program ya P4R ambayo tumejenga kwa kiwango kikubwa katika nchi yetu, lakini tulikuwa na madarasa ambayo tulikuwa tunayajenga kwa mpango wa MES II lakini kuna mipango mingine mbalimbali ambayo takriban shilingi bilioni 29 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vingi vya madarasa, zaidi ya vyumba 3,000.
Mheshimiwa Spika, katika harakati hizi, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo maeneo ya Serengeti, lakini nchi nzima kwa ujumla kwa hii mipango mipana ya Serikali ili tuondoe changamoto ya madarasa. Lengo kubwa ni wanafunzi wetu wapate maeneo mazuri ya kusomea.


WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Jafo kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imeshanunua vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 kwa ajili ya maabara zote nchini zilizokamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaanza zoezi la usambazaji wa vifaa hivyo. Kwa hiyo, natoa tu wito kwa Waheshimiwa Wabunge ambao katika maeneo yao maabara hazijakamilika, waendelee kuzikamilisha kwa sababu utaratibu wa Serikali ni kwamba tutakuwa tunapeleka vifaa pale ambapo maabara zimekamilika.