Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Jimbo la Tabora Mjini katika maeneo ya Kata za Uyui, Misha, Itetemia, Ntalikwa, Kabila, Mtendeni, Ifucha, Itonjanda na baadhi ya vijiji vya Kata ya Tumbi vina shida sana ya upatikanaji wa maji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji?
Supplementary Question 1
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwa kuwa huu mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria unaonekana unaendelea kusuasua na hauna uhakika exactly lini utaanza na wananchi wa Tabora wanaendelea kuteseka kwa shida ya maji na sisi pale Tabora Mjini tuna bwawa kubwa la Igombe ambalo lina-access ya maji kwa maana ya lita za ujazo ambazo Serikali kama itaweka mpango mkakati wa kusambaza maji yale ya Igombe na kwa unafuu, Wananchi wa Tabora Mjini watapata nafuu ya tatizo la maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba yale maji ya Igombe yaweze kusambazwa kwa bei nafuu kuliko kusubiri huo mradi wa Ziwa victoria ambao haujulikani utaanza lini? Hilo la kwanza
Swali la pili, moja ya tatizo lingine linalosababisha ile Mamlaka ya Maji (TUWASA) Tabora inapata matatizo katika uendeshaji wake ni pamoja na kutolipa deni ambalo Mamlaka ya Uendeshaji ya Maji - TUWASA pale Tabora inaidai Serikali kwa muda mrefu zaidi ya shilingi bilioni 2.3 ambazo zinadaiwa hasa kwenye taasisi zetu za majeshi pamoja na taasisi zingine za Serikali.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha TUWASAwanalipwa pesa hizo ili Tabora iweze kupata maji ambayo yatakuwa ni ya uhakika? Ahsante.
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka tuweke kumbukumbu sawa. Katika mradi huu wa Tabora-Sikonge ambao katika bajeti yetu mwaka huu nadhani tulipitisha pamoja hapa. Tulitenga takribani shilingi bilioni 29 ukiangalia kitabu cha maendeleo lakini kwa juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali kupitia ufadhili kutoka India ndiyo maana nimesema ile figure zaidi ya shilingi bilioni 500 ambayo Serikali imeshaweka commitment hiyo. Hivi sasa mchakato wa manunuzi upo katika hatua mbalimbali na lengo la mradi huu kati ya mwezi Aprili mpaka mwezi Mei mradi huu utakuwa umeanza, kwa hiyo, ndugu yangu, mtani wangu, Mnyamwezi wa Tabora naomba ondoa hofu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala zima la jinsi gani tutumie bwawa la Igombe, wataalam wetu wameshaanza kufanya tathmini pale. Takribani ule mradi utagharimu shilingi bilioni 1.5 na hili ndiyo maana tumeona kwamba jambo hili kama Ofisi ya Rais - TAMISEMI lakini na kushirikiana na wenzetu ambao ni Wizara mama wa Wizara hiyo tutaangalia jinsi gani tutafanya kwa pamoja katika mchakato wa pamoja wakati tunasubiri mradi mkubwa wa maji wa hizo shilingi bilioni 500, jinsi gani tutafanya hizo back up strategy ya mradi mwingine huu mdogo katika bwawa la Igombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo lengo letu kama Serikali ni kuweza kutatua shida ya maji katika Mkoa wa Tabora na ndiyo maana nimesema mradi huu siyo Tabora peke yake, kuna watu wa Tinde pale, kuna watu wa Kahama, kuna watu wa Shinyanga mradi huu utakuja kujibu matatizo ya watu wote wa ukanda ule. Niseme, Wasukuma na Wanyamwezi wa eneo hilo mmepata bahati kubwa sana kwa Serikali kuwaona kwa jicho la karibu kuwatengea takribani shilingi bilioni 580.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo, suala zima la bili ya maji; suala la bili ya maji ni kwamba tumetoa maelekezo mbalimbali hapa kwamba bili ya maji kupitia Waziri wa Maji ameshatoa maelezo mbalimbali, sasa naomba niziase taasisi mbalimbali; kila taasisi inayodaiwa deni la maji liweze kulipa deni la maji siyo Tabora peke yake lakini katika maeneo yote ya nchi hii, kama taasisi inayodaiwa na maji, miradi hii ya maji au hizi mamlaka za maji zitashindwa kutupatia maji kwasababu watu wanashindwa kulipa bili za maji.
Name
Shabani Omari Shekilindi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lushoto
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Jimbo la Tabora Mjini katika maeneo ya Kata za Uyui, Misha, Itetemia, Ntalikwa, Kabila, Mtendeni, Ifucha, Itonjanda na baadhi ya vijiji vya Kata ya Tumbi vina shida sana ya upatikanaji wa maji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji?
Supplementary Question 2
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa maji ni kilio cha muda mrefu sana hasa katika Jimbo la Lushoto na ukizingatia Jimbo la Lushoto lina mto mkubwa sana unaitwa Kibohelo, lakini unakuta Lushoto mto ule hautumiki unamwaga tu maji kuelekea bondeni Mombo bila kutumika maeneo yote.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha maji yale yanaenda hasa katika vijiji vya Dochi, Ngulwi, Miegelo, Kwekanga pamoja na Gare?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shekilindi anafahamu si muda mrefu sana nilitokea katika Jimbo lake na Jimbo la ndugu yangu Shangazi na kwa bahati nzuri hapa kuna mwalimu wangu hapa kutoka huko huko Lushoto amekuja hapa leo na hili naomba niwahakikishie ni kwamba ni commitment ya Serikali kuangalia jinsi gani tutatumia fursa zote zilizokuwepo kutatua tatizo la maji. Na katika Mpango wa Maji wa Awamu ya Pili, Waziri wa Maji amezungumza hapa mara kadhaa, lengo letu ni kwamba kutumia hizi fursa zilizokuwepo nikwambie ndugu yangu Shekilindi kwa sauti eneo lile nilivyofika kule Lushoto niwaagize wataalam wetu wa maji katika Halmashauri ile waanze michakato ya awali suala zima tufanyeje sasa matumizi halisi ya mto ule uweze kutumika vizuri kwa ajili ya wakazi wa Lushoto.
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Jimbo la Tabora Mjini katika maeneo ya Kata za Uyui, Misha, Itetemia, Ntalikwa, Kabila, Mtendeni, Ifucha, Itonjanda na baadhi ya vijiji vya Kata ya Tumbi vina shida sana ya upatikanaji wa maji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji?
Supplementary Question 3
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa matatizo ya maji ya Tabora ni sawa sawa na matatizo ya maji ya Mkoa wa Kagera hasa Bukoba Mjini. Kwa sasa hivi ukame umechukua muda mrefu mito mingi imekauka. Je, ni lini Serikali itatuweka kwenye Mpango wa Ziwa Victoria angalau hizi kata zilizoko karibu na Bukoba Mjini zipate maji?
Name
Eng. Gerson Hosea Lwenge
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anazungumza kuhusu maji ya Ziwa Victoria kupelekwa Kata za Mjini Bukoba. Hivi sasa Serikali imejenga mradi mkubwa sana wa kutoa maji Ziwa Victoria kusambaza katika Mji wa Bukoba. Tatizo lililopo tu ni kwamba baadhi ya maeneo yako juu. Kwa hiyo, Serikali itaweka pump za kuweza kupandisha maji zaidi kwenye yale maeneo ambayo yako juu kuliko yale ya chini ili tuweze kuona kwamba wananchi wetu wa Manispaa ya Bukoba watapata maji ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kazi ambayo inaendelea na kila mwaka tumeweka fedha kila Halmashauri na tumetoa mwongozo kwamba kwa kulingana na fedha ambazo zipo tumetenga kwenye Bajeti yetu kila halmashauri ianze kufanya manunuzi ili kusudi maeneo yale ambayo hayakuwa yamefikiwa maji yaweze kufikiwa maji kulingana na malengo ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunataka maeneo yote ya mijini tufikishe maji kwa 95% ikifika mwaka 2020; kwa hiyo Wabunge ni sehemu ya Baraza la Madiwani, tuwe karibu sana katika mipango ya maendeleo ya sekta maji kuhakikisha wananchi wetu wanapata maji.