Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Marwa Ryoba Chacha
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Primary Question
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:- Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na uvamizi wa tembo kutoka Hifadhi ya Serengeti na kupelekea vifo na uharibu wa mashamba katika Wilaya ya Serengeti na maeneo jirani:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kunusuru maisha na mali za Watanzania waishio Serengeti? (b) Je, Serikali ina mpango wa kutathimini upya fidia inayotolewa kwani haiendani na uhalisia wa uharibifu wa mali na upotevu wa maisha ya watu?
Supplementary Question 1
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba kutokana na uhifadhi unaofanywa na wananchi wa Serengeti umesababisha tembo kuongezeka kwa wingi sana.
Mheshimiwa Spika, kwa sensa ambayo imefanyika 2006, kulikua na tembo 3000 na kwa sensa ambayo imefanyika mwaka 2014 tembo wako 7000 na wengi wamehamia maeneo ya West – Serengeti sasa kwa kuwa tembo wameongezeka imekua sasa ni laana kwa wananchi wa Serengeti.
Mheshimiwa Spika, swali, kwa vyote hivi ambavyo Waziri amesema ni ukweli hakuna hata kimoja ambacho kimetekelezwa. Sasa swali kwa Waziri, la kwanza; tungetamani Wanaserengeti kila Kata iwe na game post ambayo game post itakua na gari, itakua na Maaskari na silaha. Je, Wizara iko tayari kujenga game post kwa kila Kata, ziko Kata 10 zinazozunguka hifadhi, mko tayari kutujengea game post na kila game post na askari wake wanalinda mipaka ya Kata husika dhidi ya tembo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nimepitia Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sheria Na. 5 ya Mwaka 2009, kuna kifuta machozi hakuna fidia. Na kifuta machozi kama tembo ameua mtu ni shilingi 1,000,000/= na kama wewe umeua tembo ni 25,000,000/=. Swali, kati ya tembo na mtu nani wa thamani?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Serikali katika hatua ya kwanza kabisa inampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia jitihada za Serikali katika uhifadhi. Takwimu za ongezeko la tembo ni faraja kwa Taifa hili kwa sababu kila mmoja wetu anafahamu faida za uwepo wa wanyamapori na faida za uhifadhi katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la hatua zilizochukuliwa napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ni wiki mbili tu zilizopita nilikuwa Serengeti na haya niliyoyasema hapa sikuyaandika tu kutoka kwenye karatasi isipokuwa nimeshuhudia yakiwa yametekelezwa katika hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali lake la uanzishwaji wa game posts katika kila Kata hili ni wazo jema, unapotaka kuanzisha jambo ambalo ni jipya ni lazima kujipa fursa kwanza ya kufanya utafiti uliokamilika uweze kujiridhisha juu ya umuhimu na uwezekano na ukaangalia kila aina ya jambo ambalo ni la umuhimu kabla ya kutekeleza mpango wowote unaoufikiria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunalipokea, tutalifanyia kazi na itakapoonekana kwamba ni jambo ambalo ni vema tukalitekeleza basi Serikali italitekeleza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kifuta machozi kuwa kidogo, katika jibu langu la msingi nimeeleza pale mwishoni kwamba Serikali inatambua juu ya changamoto ya kwamba kifuta jasho au kifuta machozi vyote kwa pamoja hivi kila kila kimoja havitoshi, yeye ameangalia tu upande wa maisha lakini pia hata kwenye mali, mali zinazoharibiwa wakati mwingine ukiweka ulinganifu wa kiasi cha mali kilichopotea na kiwango kile kinacholipwa mara nyingi kinakuwa ni kidogo.
Mheshimiwa Spika, lakini nimesema kwenye jibu la msingi kwamba Serikali inachukua hatua ya kupitia viwango hivyo na upitiaji wa Kanuni utakapoonekana kwamba, iko haja ya kuweza kufanya mabadiliko basi tunaweza kufanya mabidiliko hayo kwa mujibu wa sheria.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kutoa majibu ya nyongeza baada ya majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, ningependa sana niwapongeze wananchi wa Serengeti kwa moyo wao na juhudi zao katika kuhifadhi wanyamapori, ninaamini kabisa kama wananchi wa Serengeti wangekuwa hawahifadhi wanyama wale walioko pale ingekuwa vigumu sana kwa pori lile kuwa zuri na pori ambalo lina kiwango cha pili kwa ubora dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu ambao wanaua tembo ni majangili siyo wananchi wa Serengeti na ndiyo maana watu ambao wanawaua wale tembo kama wanaua kwa makusudi kama ambavyo inatokea mara kwa mara ndiyo maana wanachajiwa fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, lakini malipo haya hayalinganishi binadamu na wanyama. Lengo ni kuhakikisha kwamba watu wenye nia mbaya hawauwi wanyama bila sababu, lakini pia ni kuhakikisha kwamba Serikali inashirikiana na wananchi katika kuomboleza matukio ambayo yanaweza kutokea kwa wanyama kuwaua wananchi.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:- Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na uvamizi wa tembo kutoka Hifadhi ya Serengeti na kupelekea vifo na uharibu wa mashamba katika Wilaya ya Serengeti na maeneo jirani:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kunusuru maisha na mali za Watanzania waishio Serengeti? (b) Je, Serikali ina mpango wa kutathimini upya fidia inayotolewa kwani haiendani na uhalisia wa uharibifu wa mali na upotevu wa maisha ya watu?
Supplementary Question 2
MHE. ESHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, wananchi ambao wanazungukwa na hifadhi kwa Mkoa wa Mara, Tarime, Serengeti, Bunda Mjini na Bunda, wamekuwa wavumilivu sana. Hivi tunavyozungumza hakuna mwaka ambao tembo hawatoki kwenye hifadhi na kuja kwenye vijiji, nazungumzia kwenye Jimbo langu, Kijiji cha Serengeti, Tamau, Kunzugu, Bukole, Mihale, Nyamatoke na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tulienda na Mheshimiwa Jenista, akajionea mwenyewe tembo wanavyoharibu mazao ya wananchi, lakini bado fidia ni ndogo, shilingi 100,000/= mtu anaandaa shamba kwa milioni 10. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Utalii na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu…..
MHE. ESTER A. BULAYA: Komeni basi, kelele niongee!
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jenista wamepeleka magari mawili na askari sita kuhakikisha yale mazao ya wananchi yanalimwa. Tunaposema ni lini Serikali mtatafuta ufumbuzi wa kudumu ili hao wananchi waepukane na njaa wakati wana uwezo wa kulima na lini ufumbuzi wa kudumu utapatikana badala ya kupeleka magari na askari kwa ajili tu ya kulinda mazao ambayo yako shambani?
Name
Prof. Jumanne Abdallah Maghembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Answer
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya ziada ya kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alikuwa kule na alitoa ahadi, alijionea mwenyewe na kutoa ahadi kwamba Serikali itafanya juhudi ya kupeleka magari na askari wa ziada ili kuhahakikisha kwamba tembo hawaharibu mazao ya wananchi. Ni wiki moja na nusu sasa magari yale yako kule yanafanya kazi na tunaamini kabisa kwamba hii ni hatua ya kwanza ya Serikali kulishughulikia jambo hili kwa hatua za kudumu.
Mheshimiwa Spika, tumeanza pia kutumia ndege ambazo hazina rubani, tumeanza majaribio katika Wilaya ya Serengeti na Wilaya ya Bunda ili kuzitumia ndege hizi kuwatisha tembo na kuwaondoa katika maeneo ambayo wako karibu na mashamba ya watu na tunategemea kwamba jambo hili litatatuliwa kwa kudumu kwa kutumia utaratibu huo wa teknolojia.