Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA Aliuliza:- Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ni hifadhi ya kipekee hapa nchini, Afrika na dunia kwa ujumla; hifadhi hii ina vivutio vya kipekee pamoja na kuwa na matumizi mseto (multiple land use) ambapo wanyama na mifugo inachungwa pamoja; kutokana na upekee huo hifadhi hii imetambuliwa na kuwekwa kwenye maajabu saba ya dunia chini ya Shirika la Uhifadhi Dunia (UNESCO). Je, Serikali ina mpango gani endelevu wa kuhakikisha hadhi ya hifadhi hii inabaki kwenye ubora wake kwa ajili ya vizazi vya leo na vijavyo na pia kwa uchumi wa Taifa letu?

Supplementary Question 1

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini Serikali inaruhusu na kutoa vibali kujengwa kwa hoteli za kitalii kuzunguka rim ya Ngorongoro Crater hali inayoharibu mandhari ya Ngorongoro lakini pia ni vyanzo vya maji kwa ajili ya hifadhi hii?
Swali la pili, wakati Ngorongoro inaanzishwa mwaka 1959 ilikuwa na wakazi 8,000 lakini kwa takwimu za mwaka 2013 hifadhi hii ina wakazi elfu 87.7 kwa hivyo leo tunavyozungumza ni zaidi ya laki moja. Lakini kuongezeka kwa watu maana yake ni kuongezeka kwa mifugo lakini pia kuongezeka kwa mahitaji na huduma mbalimbali.
Naomba Serikali iliambie Bunge, wakati Hifadhi
inaanzishwa, master plan ya Ngorongoro Crater inasemaje juu ya uwepo wa idadi gani ya watu ambao wanaweza kuhudumiwa kikamilifu wakapata huduma zote, lakini pia hadhi ya hifadhi ikaendelea kubaki kama ambavyo tunategemea? Ahsante sana.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Magdalena Sakaya kwa kuwa kwanza yeye ni Mhifadhi kitaaluma lakini pia amekuwa miongoni mwa Wajumbe wa
Kamati ya Maliasili na Utalii ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kuishauri Serikali kuhusiana na masuala ya maliasili na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza ni kweli ukienda Ngorongoro leo utakuta kuna hoteli zimejengwa kandokando ya crater kwenye eneo linaloitwa rim ya crater. Lakini uwepo wa hoteli hizi ni ambao umetokana na mabadiliko mbalimbali tangu sheria ilipokuwa imeandikwa kwa mara ya kwanza mwaka 1952.
Sheria hii ilifanyiwa marekebisho ya kwanza mwaka 1963 lakini baadae sheria hiyo ilifanyiwa marejeo mwaka 2002. Katika vipindi hivyo mabadiliko mbalimbali yametokea, sasa tangu
amri ilivyotolewa kutokana na sheria kwamba sasa hakuna kuanzisha hoteli kandokando ya crater na hasa kwenye eneo la rim hakuna hoteli nyingine yoyote imeanzishwa katika kipindi hicho. Nyingi zilizopo ni zile ambazo zilianzishwa katika
kipindi cha nyuma.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili ni kweli kwamba mwaka 1959 wakati sheria hii inapitishwa kulikuwa na takribani watu 8,000 katika eneo la hifadhi na kwamba ni ukweli ulio wazi takwimu zinaonesha mwaka 2013 tayari idadi ya watu ilifikia 87,851. Ukifanya hesabu ni kama vile ongezeko la wakaazi 1500 takriban kwa kila mwaka. Hili ni ongezeko linaloashiria kwamba leo tukifanya takwimu kweli tunaweza kupata wakaazi wanaokaribia laki moja, hii ni idadi kubwa sana na ni tishio kwa shughuli za hifadhi katika eneo hili la Hifadhi la Ngorongoro.
Mheshimiwa Spika, hatua ambazo Serikali inafanya kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni uwepo wa sheria peke yake utakaoweza kutoa mwongozo na mwelekeo namna gani tunaweza kukabiliana na changamoto za hifadhi katika eneo la Ngorongoro. Sasa sheria iliyopo ina mapungufu ni kweli na ndiyo maana nimesema katika jibu la msingi kwamba katika kipindi cha muda mfupi ujao mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria ili iendane na matakwa ya sasa ya uhifadhi katika eneo linalohusika utaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, mara Serikali itakapoleta sheria hii mbele ya Bunge hili baada ya kukamilisha michakato ya awali, wote tuwe na spirit ya kutaka uhifadhi uimarishwe katika eneo la
Ngorongoro ili tuweze kupata faida zote za urithi na kiuchumi na faida nyingine zote zinazotokana na uhifadhi kupitia utalii.

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA Aliuliza:- Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ni hifadhi ya kipekee hapa nchini, Afrika na dunia kwa ujumla; hifadhi hii ina vivutio vya kipekee pamoja na kuwa na matumizi mseto (multiple land use) ambapo wanyama na mifugo inachungwa pamoja; kutokana na upekee huo hifadhi hii imetambuliwa na kuwekwa kwenye maajabu saba ya dunia chini ya Shirika la Uhifadhi Dunia (UNESCO). Je, Serikali ina mpango gani endelevu wa kuhakikisha hadhi ya hifadhi hii inabaki kwenye ubora wake kwa ajili ya vizazi vya leo na vijavyo na pia kwa uchumi wa Taifa letu?

Supplementary Question 2

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika,
ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hadhi ya Hifadhi ya
Ngorongoro inafanana kabisa na hadhi ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, mlima ambao ni mrefu sana, mlima ambao unaingiza kipato kikubwa kwenye utalii, mlima ambao ni wa pekee wenye theluji katika nchi za tropic.
Je, Serikali sasa ina mpango gani kuhakikisha
kwamba wanaozunguka mlima ule wanaweza kuwekwa katika hali ambayo wataendelea kuutunza ili ile theluji isije ikayeyuka yote na ule mlima ukabakia katika ubora wake?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kwa maana ya sifa za uhifadhi, lakini pia faida za kiuchumi zile za Ngorongoro zinafanana kwa karibu sana na za hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Sasa kuhusu swali lake nini Serikali itafanya ili kuweza kuboresha zaidi shughuli za uhifadhi kwa faida za kiuchumi Kitaifa lakini pia kwa faida ya jamii inayoishi kwenye maeneo haya ya Hifadhi ya Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba kwanza Serikali inatambua umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi na kwa kweli tunatoa wito kwa wananchi wanaoishi katika eneo hili la Mlima Kilimanjaro waweze kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba uhifadhi unaimarishwa katika eneo la Kilimanjaro. Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali ni kuendelea kusimamia sheria iliyopo lakini pia tunakaribisha maoni kutoka kwa wananchi wanaoishi kwenye eneo hilo hata wengine waweze kutusaidia ili kuweza kupata maoni ya
wananchi yatakayotuwezesha kuboresha zaidi shughuli za uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA Aliuliza:- Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ni hifadhi ya kipekee hapa nchini, Afrika na dunia kwa ujumla; hifadhi hii ina vivutio vya kipekee pamoja na kuwa na matumizi mseto (multiple land use) ambapo wanyama na mifugo inachungwa pamoja; kutokana na upekee huo hifadhi hii imetambuliwa na kuwekwa kwenye maajabu saba ya dunia chini ya Shirika la Uhifadhi Dunia (UNESCO). Je, Serikali ina mpango gani endelevu wa kuhakikisha hadhi ya hifadhi hii inabaki kwenye ubora wake kwa ajili ya vizazi vya leo na vijavyo na pia kwa uchumi wa Taifa letu?

Supplementary Question 3

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika,
ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa gharama kubwa ambazo Hifadhi ya Ngorongoro inatumia ni pamoja na kumtunza faru Fausta ambaye chakula chake kwa mwezi ni shilingi milioni zaidi ya 64. Naomba kufahamu, Serikali ina mpango gani juu ya faru huyu Fausta ambaye analigharimu Taifa au hifadhi ile kwa fedha nyingi sana kwa mwezi na
hata kwa mwaka?

Name

Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli yuko faru Fausta pale
Ngorongoro na amewekwa kwenye cage kwa sababu amekuwa mzee sana na amekuwa ananyemelewa na magonjwa aina mbalimbali na lengo ni kuhakikisha kwamba maisha yake yanaendelea utafiti na takwimu ambazo zinakusanywa kwa ajili ya faru huyu zinaendelea, kwa sababu wanyama hawa ni wachache sana nchini hivi sasa na kila takwimu ambayo tunakusanya na kuilinganisha na maisha halisi ya wale ambao wako kwenye pori ni muhimu kwa
maisha ya wale wengine ambao wanaishi humo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kufanya kazi hii kuna gharama, lakini hizi ndiyo gharama halisi za uhifadhi. Namuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kutuamini kwamba tunafanya jambo hili kwa nia njema na kwamba takwimu zinazopatikana zinathamani halisi kwa ajili ya
uhifadhi wa wanyama hawa.