Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA Aliuliza:- Je, ni lini Mfumo wa Taarifa za Watumishi LAWSON utaboreshwa na kuondoa dosari zilizopo sasa hivi kama vile watumishi wa Umma kuondolewa kwenye makato ya mikopo wakati hawajakamilisha malipo?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri
ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Ni wazi kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mfumo huu una upungufu na una changamoto nyingi ambazo nimeelezea mojawapo. Sasa nataka commitment ya Serikali kwamba hiyo Version 11 itaanza kutumika lini? Swali langu la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; changamoto nyingine ya mfumo huu ni kwamba, unasimama peke yake (stand
alone system) na wakati ukiangalia kwenye taasisi zetu, kwa mfano Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kuna mifumo mingi, tulitegemea kwamba mifumo hii ingekuwa inaongea; kuna EPICA, kuna LGMD, sasa je, Mheshimiwa Waziri atanihakikishia kwamba mfumo huu mpya Lawson Version 11 utakuwa unaongea na mifumo mingine?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nimpongeze sana kwa namna ambavyo amekuwa akisimamia suala zima la management ya rasilimali watu katika utumishi wa umma na yeye mwenyewe pia alikuwa katika utumishi wa umma na tunafahamu mchango wake na tunauthamini.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza, kwamba sasa Toleo hili la 11 ( Lawson Version 11) litaanza lini; nimhakikishie tu kwamba, katika Mwaka huu wa Fedha tumeshatenga Shilingi milioni 486 katika Idara yetu ya
Usimamizi wa Rasilimali Watu pamoja na Idara yetu ya TEHAMA na nimhakikishie tu kwamba katika Mwaka huu wa Fedha suala hili litakamilika. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, tumewakabidhi suala hili Wakala wa Serikali Mtandao ili waweze kusanifu na kusimamia usimikaji wake.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, kwamba ni lini sasa mfumo huu wa usimamizi wa rasilimali watu au
taarifa za kiutumishi na mishahara utaweza kuzungumza na mifumo mingine kama mifumo ya kifedha kama EPICA na mingine; nimwambie tu kwamba tunaiona hoja yake na hata e-government wamekuwa wakifuatilia suala hili kwa makini sana, si tu katika suala zima la kuongea, hata katika kuhakikisha pia gharama za mifumo yenyewe na udurufu wa kuwa na mifumo mingi wakati kunaweza kukawa na mifumo michache ambayo inaweza ikazungumza.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu kwamba pamoja na faida nyingine tutakazozipata tutakapoingia katika
Lawson Version 11 ni pamoja na kuunganisha mifumo mingine kama EPICA lakini pia kuhakikisha Mifumo kama ya NECTA, NIDA, RITA pamoja na mingine nayo pia ni lazima izungumze na Mfumo wetu wa Lawson.