Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Primary Question

MHE. SALEH ALLY SALEH (K.n.y. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) Aliuliza:- Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na matendo ya dhahiri yanayoonesha kuvunjwa kwa haki za binadamu hapa nchini bila ya Serikali kuchukua hatua yoyote. Je, Serikali haioni kwamba wananchi watakosa imani na Serikali yao?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ahsante kwa mwalimu wangu. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mwalimu wangu utakuwa unajua kwamba katika siku za karibuni kumekuwa na vitendo vingi vya utesaji na vimekuwa vikitajwa hadharani, lakini Mahakama zitapewa nguvu zaidi kama Tanzania itaridhia mikataba ya Kimataifa. Kuna mkataba mmoja muhimu wa Convention Against Torture mpaka leo Serikali inasuasua kujiunga.
Je, ni lini Serikali itaridhia mkataba huo muhimu ili Mahakama zipate nguvu zaidi kushughulikia masuala haya? Pamoja na kwamba suala hilo limetajwa katika Katiba, lakini mkataba huo ni muhimu.
Swali la pili, hadi sasa mfumo uliopo hauruhusu Ripoti ya Haki za Binadamu kujadiliwa katika Bunge, inawasilishwa lakini haijadiliwi na kwa maana hiyo, Waheshimiwa Wabunge hawana uelewa wa pamoja au uelewa mkubwa wa kujua kiasi gani madhara ya haki za binadamu na namna zinavyokiukwa kwa kulinganisha hata ripoti ya karibuni ya Amnesty International inayoonesha kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu Tanzania ni mkubwa sana.
Je, kwa weledi wako, ushawishi wako, karama ulizopewa na Mwenyezi Mungu, ni vipi utaweza kuishawishi Serikali ili ripoti hiyo iweze kujadiliwa ili Waheshimiwa Wabunge wajue yapi yanatokezea katika nchi yao?

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kama alivyoeleza, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenyewe inakataza vitendo vyovyote vya kumtesa, kumtweza na kumdhalilisha mtu. Tafsiri ya Ibara hiyo ya Katiba imewekwa wazi na Mahakama na Rufaa katika kesi ya Mbushuu Mnyaroje dhidi ya Serikali ambapo Mahakama ya Rufaa ilieleza wazi kabisa kwamba vitendo vyovyote vinavyomtesa mtu, kumtweza na kumdhalilisha, havikubaliki na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Rufaa ilikwenda mbele zaidi, ilitumia mikataba ya Kimataifa ile ambayo Tanzania imeridhia na ile ambayo haikuridhia kama msaada kwao wa kutafsiri maana ya neno au maneno utesaji, udhalilishaji na utwezaji. Kwa hali hiyo basi, maoni hayo kwamba mkataba huu dhidi ya utesaji ambao tayari misingi yake imo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambayo tayari Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo Mahakama ya mwisho ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeyakubali, yatafikiriwa ili kwa wakati muafaka jambo hilo lifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ripoti ya CHRAGG kuletwa Bungeni, maoni hayo nimeyapokea na labda kwa upya wangu nitauliza ni jinsi gani yanafikishwa, maana hata kikao kimoja cha Baraza la Mawaziri sijakaa ili nijue utaratibu wa kuyafikisha, kujadiliwa ili nikiongozwa njia ya kuku mgeni kamba kuwa imefunguka, basi nitajua jinsi ya kwenda nalo.

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SALEH ALLY SALEH (K.n.y. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) Aliuliza:- Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na matendo ya dhahiri yanayoonesha kuvunjwa kwa haki za binadamu hapa nchini bila ya Serikali kuchukua hatua yoyote. Je, Serikali haioni kwamba wananchi watakosa imani na Serikali yao?

Supplementary Question 2

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba nimwulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa kuna wananchi ambao wanakamatwa kwa uhalifu mbalimbali, aidha wa kubandikiziwa kesi na kupata kipigo kikali sana na kufanyiwa majeraha kwenye miili yao na kufikishwa kwenye vyombo vya mahabusu bila kupatiwa huduma za afya, hamuoni kama mnakiuka haki za binadamu?

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kama jambo hilo limetokea Zanzibar, pia kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, vitendo hivyo ni vitendo vya kukiuka Katiba kama vimetokea. Kwa yule viliyemtokea kama vimemtokea; moja, anayo nafasi ya kuiambia Mahakama ameteswa au amefanywa hivyo na hatua kuchukuliwa. Pia kuchukua hatua hizo kuziarifu mamlaka nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ushahidi upo kama ilivyovyoelezwa, Serikali na vyombo vyake inao utaratibu wa kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo ambavyo Katiba yenyewe imevizuia, sheria imevizuia, lakini hiyo haina maana hakuna binadamu wanaofanya hayo. Tumepewa amri kumi na Mwenyezi Mungu, mara nyingi tunazihalifu, lakini haina maana kwamba hazipo. Kwa hiyo, yakitokea hayo, tuarifiwe.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. SALEH ALLY SALEH (K.n.y. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) Aliuliza:- Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na matendo ya dhahiri yanayoonesha kuvunjwa kwa haki za binadamu hapa nchini bila ya Serikali kuchukua hatua yoyote. Je, Serikali haioni kwamba wananchi watakosa imani na Serikali yao?

Supplementary Question 3

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa katika swali hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa kwamba baadhi ya askari polisi wetu wanashindwa kutumia sheria ambayo inawaelekeza namna ya kukamata watuhumiwa na mara nyingi sana polisi wamekuwa wakiwahukumu watuhumiwa kwa kipigo kikali sana kabla hawajawafikisha Mahakamani na wakiwafikisha Mahakamani, Mahakama zinawaona watuhumiwa kwamba hawana hatia. Kama Mahakama ilivyoamua hivi majuzi kwenye kesi ya Bwana Mdude, Nyangari na wenzake huko Mbozi.
Je, Serikali iko tayari kwa Wizara hizi mbili; ya Sheria pamoja na Mambo ya Ndani kupiga marufuku na kuchukua hatua dhahiri na za wazi kwa polisi ambao wanaidhalilisha Serikali kwa kuwaumiza raia kwa kipigo?

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Selasini, naye ana heshima ya kuwa mdogo wangu kwa sababu Lamwai ni kaka yetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu wa Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara na Mambo ya Ndani kukaa chini na kuyapitia mambo hayo. Moja ya msisitizo ambao umekuwepo katika Wizara hizi mbili ni kuendelea kuwapa polisi mafunzo ya juu ya haki za binadamu, lakini pia jinsi ya kutumia mamlaka waliyonayo ya kukamata watu na kuzuia uhalifu kwa namna ambayo inaheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaheshimu Sheria ya Kuanzisha Jeshi la Polisi na inaheshimu sheria zilizowekwa. Kwa hiyo, tutakaa na kulijadili.