Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Philipo Augustino Mulugo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songwe
Primary Question
MHE. PHILLIPO A. MULUGO Aliuliza:- Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya sheria zetu hapa nchini kutoendana na mabadiliko na kasi ya maendeleo ya Taifa na kuonekana kuwa zimepitwa na wakati. Je, ni lini Serikali italeta hoja ya kufanya marekebisho ya kuboresha baadhi ya sheria zilzopitwa na wakati?
Supplementary Question 1
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ambayo kidogo hayajatosheleza, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hamu na haja ya Waheshimiwa Wabunge wengi, toka nimeingia Bungeni hapa mwaka 2010, Wabunge wengi wanahitaji sana mabadiliko ya sheria ndogo ndogo ili mambo yaweze kuendana na wakati. Iko Sheria ya Ndoa ambayo inasema lazima mtoto awe na miaka 14 kuweza kuolewa; lakini mimi nimekuwa mwalimu muda mrefu, najua miaka 14 kwa sheria ya leo ilivyo ya elimu msingi, anakuwa bado ni mtoto yupo form two na tunasema elimu msingi mtoto atoke chekechea mpaka form four na ni elimu ya lazima. Kwa hiyo, unakuta ile sheria imepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi nilisema hapa kuhusu Sheria ya TMAA ya Madini kwamba Halmashauri kule zinapata ile ruzuku (service levy) ambayo unakuta hawajui source yake imetoka wapi kwa sababu hawashiriki katika kuangalia pato lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ipo Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 1978, imepitwa na wakati. Sasa yote hayo nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mwaka 1980 Serikali iliunda Tume kwa ajili ya kuangalia Sheria Mbalimbali na mabadiliko ili iweze kuletwa Bungeni, mpaka leo Tume hiyo ni kama vile imeshindwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Bunge liwe na Tume yake, Serikali iwe na Tume yake ili na sisi tuonekane kweli tunatunga sheria. Maana toka nimekuja mwaka 2010 hapa sijawahi kuona Mbunge kaleta hoja binafsi hapa na ikapita. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wana hoja binafsi nyingi, lakini wakileta hapa hakuna kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iruhusu Bunge liwe na Tume ili sisi wenyewe tuanze kutunga sheria na Serikali iwe na Tume, tuzilete pamoja tuweze kujadili ili tuweze kufanya marekebisho ya sheria kadri mambo yanavyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali italeta hoja ya kuruhusu Bunge iwe na Tume yake binafsi?
Name
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la nyongeza la Sheria kuliruhusu Bunge kuwa na Tume yake, liko nje ya mamlaka na uwezo wangu, kwa sababu ni suala la Bunge lenyewe, lakini nitalitolea indhari, haitakuwa muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kazi za Tume hii, Tume hii imefanya kazi nyingi na baadhi yake zimezaa matunda. Kwa mfano, sheria ambazo zimetokana na utafiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria ya Tanzania ni pamoja na Sheria ya Upimaji wa Vinasaba wa Binadamu (The Human DNA Regulation Act No. 8 of 2009); Sheria ya Mtoto (The Law of the Child Act No. 21 of 2009); Sheria ya Makazi na Mahusiano Kazini (The Employment and Labour Relations Act No. 6 of 2004); Sheria ya Watu Wenye Ulemavu (The Disability Act No. 9 of 2010); hizi ni baadhi ya sheria tu ambazo zimetungwa kutokana na kazi ya Tume ya Kurekebisha Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa iko Sheria ya Ndoa ambayo mchakato wake unaendelea kuhusu moja, umri wa mtoto kuoa na kuolewa. Niseme leo, kuna jambo ambalo haliko sahihi; ukiangalia kuhusu umri wa miaka 14, naomba mwende muisome ile sheria, inaruhusu mtoto wa kike kuolewa na miaka 14 na mtoto wa kiume kuoa na miaka 14.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu kile mwaka 1971 kiliwekwa ili kukidhi mahitaji ya jamii mbili, Wamasai na Mabohora. Sasa ikifika wakati hali imebadilika, umuhimu huo haupo, tutalijadili. Kwa hiyo, umri wa miaka 14, someni sheria, siyo kwa msichana tu, ni kwa hata mtoto wa kiume kuruhusiwa kuoa chini ya miaka 14 kama Mahakama imeruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakubali, mtoto wa kiume kuoa miaka 14 hajafikia umri wa kuoa; na mtoto wa kike kuolewa miaka 14 hajafikia umri wa kuolewa, lakini jambo hili linataka mwafaka wa kijamii kama ambavyo mwaka 1970 ilikuwa ni muhimu kuwaangalia Wamasai na Mabohora ambao ni sehemu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maadam mchakato unaendelea, tunaendelea kuzungumza Inshallah siku itafika, jambo hilo litapita.
Name
Susan Anselm Jerome Lyimo
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PHILLIPO A. MULUGO Aliuliza:- Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya sheria zetu hapa nchini kutoendana na mabadiliko na kasi ya maendeleo ya Taifa na kuonekana kuwa zimepitwa na wakati. Je, ni lini Serikali italeta hoja ya kufanya marekebisho ya kuboresha baadhi ya sheria zilzopitwa na wakati?
Supplementary Question 2
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Naomba nirudie hapo hapo aliposema Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Waziri, tarehe 08/07/2016 Majaji wawili; Jaji Lila na Jaji Munisi walitoa hukumu in favour ya Rebecca Gyumi kuhusiana na suala la vifungu vya 13 na 17 kwenye suala la Sheria ya Ndoa. Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza agizo la Mahakama Kuu ili kufuta vifungu vya 13 na 17?
Name
George Mcheche Masaju
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Answer
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maamuzi yale Serikali imekata rufaa. Kwa mujibu wa sheria ya Basic Rights and Duties Enforcement Act, kama ni kesi ya kikatiba, unapowasilisha notice ya kukata rufaa inasimamisha utekelezaji moja kwa moja wa maamuzi ya Mahakama. Kesi ile haikuwa na mambo haya ya ndoa tu, kuna mambo mengi yalijitokeza na hayo yote lazima tupate mwongozo wa Mahakama ya Rufaa. Kwa hiyo, naomba kuwasihi Waheshimiwa Wabunge wawe na subira hadi hapo Mahakama itakapotoa maamuzi.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. PHILLIPO A. MULUGO Aliuliza:- Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya sheria zetu hapa nchini kutoendana na mabadiliko na kasi ya maendeleo ya Taifa na kuonekana kuwa zimepitwa na wakati. Je, ni lini Serikali italeta hoja ya kufanya marekebisho ya kuboresha baadhi ya sheria zilzopitwa na wakati?
Supplementary Question 3
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ambaye ni mwalimu wangu nampongeza sana kwa majibu mazuri. Kama hawatamharibu, ataenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba yeye mwenyewe kama mzazi na kama mwalimu umri wa mtoto wa kiume kuoa miaka 14 hakubaliani nao na umri wa mtoto wa kike kuolewa hakubaliani nao. Sasa Serikali kwa mujibu wa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maana yake anataka kuniambia Serikali inataka watoto wadogo waendelee kuolewa. Kwa hiyo, watoto wa kike wasipate haki yao ya kucheza na kupata elimu na kuwa viongozi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hukumu ilikuwa ni miezi sita na imeshapita na rufaa haijakatwa. Sasa naomba niulize swali, kwa nini Mheshimiwa Waziri sasa asilete Muswada Bungeni ili amri hiyo ya Mahakama ya Rufaa itekelezwe ili kuwapa haki watoto wadogo wa kike na kiume wapate haki ya kusoma na kuwa viongozi wa Taifa hili?
Name
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wote ambao wamesoma Legal Anthropology wataelewa kwamba mambo ya mila, desturi, imani ya dini na itikadi hayataki haraka, yanataka muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yoyote na bahati mbaya, aah, kwenye Kiswahili hakuna bahati mbaya. Kuna umuhimu sasa wa vyuo vyetu kufundisha Legal Anthropology. Huwezi kubadili mila, desturi, imani ya dini na itikadi kwa kutumia sheria peke yake tu, utakuwa unajidanganya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka katika utamaduni ambao umekuwa na mila siyo nzuri ya ukeketaji. Sheria ipo, imezuia, lakini kwa sababu bado ni suala la imani na itikadi kwa watu, leo wamelihamishia kwa watoto wachanga. Sasa nazungumza kama Profesa wa Sheria, ni hatari. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Waitara Chacha, rafiki yangu mkubwa, anajua kabisa kuna mila na desturi za anakotoka leo, mimi siafikiani nazo, lakini zinahitaji elimu, zinahitaji uelewa. Ni vigumu sana mtu anayetoka nje ya eneo hilo kuelewa kwamba mapenzi ni pamoja na kipigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namsihi Mheshimiwa Waitara, tukae nje, tukutane. Namsihi na nimesema hivi kwa masihara haya kwa sababu ni mtu tumeshibana, hawezi kunichukulia tofauti. Tutalijadili, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutalijadili, ahsante