Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Primary Question

MHE.OSCAR R. MUKASA aliuliza:- Ibara ya 57(b) ya Ilani ya CCM inaahidi kuweka mfumo wa kuvitambua, kuvisajili na kuviwezesha vikundi vyote vyenye mwelekeo wa ushirika na ujasiriamali nchini. Kwa kuwa kundi la waendeshaji wa vyombo vya usafiri wa abiria maarufu kama bodaboda ni kundi la kijasiriamali, na inawezekana ndilo kundi lenye mwelekeo na fursa za kiushirika ambalo ni kubwa zaidi Wilayani Biharamulo na nchini kote kwa sasa. Je, Serikali ina mpango gani mahususi juu ya kundi hili?

Supplementary Question 1

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa mujibu wa takwimu tulizopewa kwenye majibu na Mheshimiwa Waziri, asilimia 80 ya waendesha bodaboda hawana leseni, jambo ambalo linawafanya waishi kwenye mzunguko wa kukimbizana na polisi badala ya kuzalisha mali kwa ajili kujenga uchumi wao na uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, Serikali iko tayari kuwasaidia kwa kuwawekea ruzuku ya kupunguza walau kwa mara moja kodi ya kulipia leseni angalau kwa nusu ili waweze kupata leseni kama hatua ya kwanza ya kuwasaidia ili tuweze kushirikiana nao kuongelea habari ya kuwahamisha kuwapeleka kwenye ushirika wa SACCOS na mambo mengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi twende Biharamulo kuziona fursa nyingine zaidi ya kuwaomba tu wajiunge kwenye SACCOS ambazo Serikali Kuu ikishirikiana na sisi tunaweza kuzitumia kuwatoa kwenye yale waliyonayo ili Biharamulo iwe mfano wa kusambaza hatua kama hiyo maeneo mengine ili kundi kubwa la bodaboda nchini tulisaidie liwe la ujasiriamali kweli kweli? Ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZAA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Mbunge kama ikiwezekana Serikali ifanye uwezeshaji, naomba nikiri wazi kwamba hatuwezi kusema kama Serikali tufanye uwezeshaji kwa watu wote, lakini tunakuwa na mikakati mbalimbali ya kufanya uwezeshaji. Mimi niwapongeze Wabunge wengi humu ndani ambao wamefanya initiatives katika Majimbo yao kuhakikisha vikundi mbalimbali vinahamasishwa na wao wanasaidia ku-chip in humo kwa ajili ya kuwasaidia vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mimi ninajua wazi kwamba kuna baadhi ya Halmashauri nyingine zina mipango mbalimbali yenye lengo la kuwasidia hawa vijana ili hatimaye, kama ulivyofanya Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lako ambapo na sisi tume-recognise shughuli na juhudi kubwa unazofanya katika Jimbo lako, nadhani tukifanya uhamasishaji sisi wengine tutafanya kwa kuangalia fursa zilizopo katika maeneo yetu na hivyo tutaweza kuwasaidia hao vijana kwasababu lengo letu ni kwamba vijana waweze kukomboka katika jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kikubwa zaidi kama hatufahamu; bahati nzuri Ofisi ya Mama Jenista Mhagama katika Baraza la Taifa la Uwezeshaji, hata jana nadhani walikuwa wanafunga mafunzo yao, wameona kwamba jinsi vijana wengi wanavyokosa fursa hizi kwa kutokuwa na ufahamu wa kutosha na ndiyo maana wamesema sasa hivi wanataka kuzifanya programu zao kupitia maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sehemu ya pili naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi nipo radhi, nilifika Biharamulo mara ya kwanza, lakini kama kuna jambo lingine mahususi tutakwenda tena ili kuwasaidia vijana wetu waweze kufika mbele katika suala zima la maendeleo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Jafo kwa majibu yake mazuri kwenye swali hili la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaka kuiuliza Serikali ni kwa kiasi gani inaweza ikajipanga kupeleka juhudi za ziada ili kuhakikisha kwamba vijana wa Tanzania, hasa vijana wa kule Biharamulo wanaweza kufaidika na mikopo mbalimbali na kuweza kuwaboreshea shughuli za ujasiriamali wakiwemo vijana wa bodaboda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie kwamba, Mheshimiwa Mbunge ni kati ya Wabunge ambao walihudhuria maonyesho ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, na tumeshakubaliana na Mheshimia Mbunge kwamba baada ya shughuli hizi za Bunge kukamilika, Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na timu ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na yeye Mheshimiwa Mbunge watakuwa na ziara maalum kule Biharamulo ili kuangalia Serikali inaweza ikafanya nini kwa ajili ya maendeleo ya vijana na sekta nyingine.
Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, tumefunga maonesho ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, tunaomba sana tuendelee kuwasiliana ili fursa zilizopo ndani ya Serikali ziweze kuwafikia Watanzania wengi hasa wakipato cha chini na kipato cha kati wakiwemo vijana na kuweza kuwainua kiuchumi. Nakushukuru