Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mendard Lutengano Kigola
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Primary Question
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:- Serikali iliahidi kupeleka gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Mgololo lakini hadi sasa gari hilo halijapelekwa:- Je, ni lini gari hilo litapelekwa ili liweze kusaidia Vijiji vya Idete, Itika, Holo, Isaula, Rugema, Makungu, Rugolofu na Kitasengwa?
Supplementary Question 1
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini pamoja na majibu yake Naibu Waziri kwamba hili gari kwenye bajeti ya mwaka 2013/2014 na swali la msingi niliuliza mwezi wa Tisa na kwenye bajeti walisema kwamba wametenga milioni 150 kwa ajili ya ununuzi wa hili gari la wagonjwa wa kule Mgololo, mpaka leo hili gari halijapelekwa. Niliwahi kumuuliza Waziri wa Afya akaniambia kwamba kuna magari matano yamenunuliwa mojawapo litapelekwa kule, lakini mpaka leo halijakwenda. Je, bajeti ya mwaka uliopita ambayo ilitengwa kwa ajili ya hilo gari, hiyo fedha ya shilingi milioni 150 ilikwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hii gari ni ya msingi sana, kwa sababu itahudumia Kata tatu, kuna ya Kiyowela, Kata ya Idete na Kata ya Makungu. Kule kuna watu wanakaribia karibu 120,000 hivi, akinamama wanapata taabu sana kuna milima, jiografia ya kule ni ngumu sana. Sasa naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anithibitishie kwa sababu hii pesa ya Halmashauri haina uhakika, ni lini hii gari hili la wagonjwa litapelekwa Mufindi?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri wazi kwamba nilifika Mufindi katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge mpaka Mgogolo. Hili ni miongoni mwa Jimbo ambalo lina changamoto kubwa kutokana na jiografia yake ilivyo. Hata hivyo, nipende kumshukuru pia kwa juhudi kubwa anayofanya katika kuhakikisha mambo yanakwenda katika Jimbo lake kwa sababu katika miaka mitano iliyopita alikuwa akipigania mambo mbalimbali katika maeneo yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la msingi la kwanza aliposema bajeti ya mwaka ilitengwa lakini haikupatikana ni kweli, na nyinyi mnafahamu sio bajeti ya ambulance peke yake, isipokuwa miradi mingi sana ya maendeleo katika kipindi kilichopita, imekumbwa na changamoto kubwa sana hasa ya upelekaji wa fedha. Maombi haya yalikuwa ni katika maombi maalum, hivyo ni imani yangu kwamba katika bajeti ya mwaka huu sasa kwa vile jiografia yake inajulikana, Ofisi ya Rais - TAMISEMI tutaweka kipaumbele kuhakikisha gari hilo linapatikana. Kikubwa zaidi katika hayo yote maana yake maombi maalum wakati mwingine yana changamoto kubwa sana na sana sana zinalenga katika collection ya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote tushikamane kwa pamoja kuisaidia nchi yetu ili tupate mapato ya kutosha, yale maombi maalum yote tuliyoyapeleka, Serikali iweze kuona ni jinsi gani yatayafanyiwa kazi.
Sehemu ya pili, ni kwamba ni lini gari litapatikana, nimesema kwamba, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sababu tunaguswa na hili, katika uongozi wetu wa sasa tutapambana kwa kadri iwezekanavyo. Ndugu yangu wa Mufindi tujitahidi kwa pamoja Mungu akijalia tutapata gari, naomba amini Ofisi yako.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved