Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Jimbo la Tabora Mjini hususan katika Kata za Mpera, Malolo, Mbugani na Ng’ambo (Kidongo Chekundu) kuna migogoro ya muda mrefu ya ardhi na bomoa bomoa ya nyumba za wananchi. Je, Serikali inafanya juhudi gani kuhakikisha inamaliza migogoro hiyo ya ardhi ambayo ni kero ya muda mrefu kwa wananchi?
Supplementary Question 1
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongezana ninaomba kuiuliza Serikali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba hii migogoro kweli ipo na ni ya muda mrefu, Jimbo la Tabora Mjini linazungukwa na kambi nyingi za Jeshi ambazo migogoro mingi inapelekea kuhatarisha amani miongoni mwa wanajeshi pamoja na raia. Ni lini sasa Serikali au Serikali ina mpango gani wa kuwakutanisha wanajeshi wahusika ili waweze kukaa na wananchi kuweza kutatua migogoro hiyo ya ardhi iliypo Tabora Mjini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali inafanya uhakiki mbalimbali kuanzia watumishi wa Serikali na mpaka leo tumeona wale wa vyeti, lakini ni lini Serikali itafanya uhakiki wa hawa Maafisa wa Ardhi ambao wanaingiza migogoro kwa makusudi kati ya wananchi pamoja na Serikali kwa kufanya mpango wa kugawa viwanja; kwa mfano kiwanja kimoja kutolewa zaidi ya mtu mmoja (double allocation). Maafisa hao wapo na hawajafanyiwa uhakiki ili wachukuliwe hatua. Ni lini Serikali itafanya uhakiki wa hawa maafisa wanaoleta migogoro ili na wao wachukuliwe hatua?
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA, MAENDELEO NA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu ni kweli alichokisema kwamba maeneo mengi ambayo yamezungukwa na Majeshi na wala si majeshi tu hata watu wengine wa kawaida, kumekuwa na migogoro baina ya wananchi na pande ya pili inayomiliki wakiwemo Jeshi. Kuhusu zoezi alilouliza, mimi nimwambie tu kwamba naomba wananchi wa Tabora wawe na subira kwa sababu tayari zoezi la kuhakiki maeneo ambayo yana migogoro na yale ambayo yanamilikiwa na Jeshi limeshaanza. Upande wa wenzetu Wizara ya Ulinzi wameshaunda kamati ambayo imeanza kupitia katika maeneo na mimi nikiri tu wazi na ni-declare interest kwamba hata kwenye Wilaya yangu pia kulikuwa na tatizo hilo lakini tayari Kamati ile imeanza kupita na wanafanya uhakiki wa mipaka.
Mheshimiwa Spika, na wanapofika katika maeneo
yale wanahusisha uongozi wa eneo husika. Kwa hiyo, wakifika pale lazima uongozi wa Wilaya na uongozi wa Mitaa au Vijiji vinavyohusika watahusishwa ili kuweza kubaini ile mipaka iliyokuwepo toka mwanzo. Wenzetu Jeshi wameenda mbali zaidi, kwa yale maeneo ambayo watakuwa hawayahitaji baadae watasema nini cha kufanya katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuyarejesha pia kwa wananchi; lakini ni baada ya uhakiki kwasababu mengine yako strategically huwezi kuyaondoa leo na kuwapa wananchi. Kwa hiyo, uhakiki huo Mheshimiwa nikuhakikishie umeshaanza, unafanyika na Tabora watafika na tatizo litakuwa solved.
Mheshimiwa Spika, swali la pili amezungumzia suala la uhakiki wa maafisa ambao wanaingiza mgogoro kati ya Serikali na wananchi. Mimi niseme tu kwamba katika ziara ambazo tunafanya mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri kila tunapopita tukikuta kuna tatizo hatua zinachukuliwa palepale. Ni juzi tu hapa alikuwa Lindi ambako tumekuta kuna mtu kamilikishwa eneo kubwa la wananchi zaidi ya ekari 4,000 lakini Mheshimiwa Waziri ame-declare pale pale kwamba ardhi ile irudi kwa wananchi na yule mtumishi amesimamishwa. Hata hivyo mimi pia nilipopita katika maeneo yale kuna wafanyakazi idara hiyo tumewatoa katika eneo lile na kuweza kutafuta wale wengine wanaohusika.
Mheshimiwa Spika, niseme kwa upande wa Maafisa Ardhi wale ambao ni wateule ni jukumu la Halmashauri, tukiona kwamba huyu mtu hafanyi kazi yake vizuri ni lazima tumuondoe na tunaleta jina lingine kwa maana ya ku-propose ateuliwe kuwa Afisa Ardhi Mteule; kwa sababu wale nao wasipofanya kazi yao vizuri hawa wadogo wa chini wanaharibu kazi zaidi. Kwa hiyo, ni jukumu letu sote katika maeneo yetu kuona wasiofanya kazi vizuri wachukuliwe hatua kwa sababu mamlaka ya ajira yako pale pale katika maeneo yao, kwa maana ya Mkurugenzi. (Makofi)
Name
Joseph Roman Selasini
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Jimbo la Tabora Mjini hususan katika Kata za Mpera, Malolo, Mbugani na Ng’ambo (Kidongo Chekundu) kuna migogoro ya muda mrefu ya ardhi na bomoa bomoa ya nyumba za wananchi. Je, Serikali inafanya juhudi gani kuhakikisha inamaliza migogoro hiyo ya ardhi ambayo ni kero ya muda mrefu kwa wananchi?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, kuna zoezi linaendelea katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Kata za Kitendeni, Tarakea, Reha na Nanjara katika Jimbo la Rombo. Nyumba za wananchi zinawekwa ‘X’ na wameamriwa kuzivunja. Sababu wanayopewa ni kwamba wanataka kuhakiki mpaka wa Kenya na Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nyumba hizi na wananchi hawa wameishi katika maeneo hayo kabla hata ya uhuru. Sasa naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, uko tayari kusimamisha zoezi hili ili wananchi wale wa Kikerelwa, Nayeme na maeneo mengine wapewe maelezo ya kutosha kuhusu zoezi hilo na labda pengine uko tayari tuongozane wewe na mimi kwa ajili ya kwenda kuwapa hawa wananchi maelezo ya kuridhisha? (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunilinda.(Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ni kweli zoezi la uhakiki katika mipaka yetu linaendelea, lakini naomba tukumbuke kwamba usalama wa nchi yetu hii tusipouangalia sisi wenyewe tunaweza tukajikuta tunaiingiza nchi katika matatizo. Kwa sababu wananchi wanapokuwa wanaingiliana katika yale maeneo ndipo hapo hapo uharifu unakuwa ni mkubwa zaidi, huwezi kujua ni nani amefanya zoezi hili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kuhakiki mpaka tunakwenda sambamba na ile eneo ambalo ni no man’s land lazima libaki wazi, lakini pia ile buffer zone inayotakiwa kuwepo pale lazima hatua zinazotakiwa zionekane kubaki. Kwa hiyo, lazima tu katika lile eneo pawe wazi ili kuweza kutambua na kuainisha mipaka ilivyo na ile no man’s land imekaa namna gani. Na hili tatizo pia lipo hata upande wa Tunduma, Uganda na Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niwaombe tu kamba tunapofanya zoezi hili kama kuna mtu ambaye amevunjiwa tofauti na utaratibu pengine hakustahili kuvunjiwa hilo ndilo tunaloweza tukalisikiliza. Kwa wale waliojenga kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kujengwa yanatakiwa yabaki wazi zoezi litaendelea kwa sababu ya kuangalia usalama wa nchi yetu ili tuweze kuudhibiti uingiaji holela katika maeneo. (Makofi)