Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mariamu Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Kumekuwa na ujenzi wa nyumba za ghorofa kando kando ya barabara kuu na Serikali ndiyo inatoa vibali vya ujenzi huu ambapo baada ya muda maghorofa hayo yanaweza kubomolewa na mwenye jengo kulipwa fidia. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuainisha maeneo yenye mipango ya maendeleo ili kuepuka gharama kubwa ya kulipa fidia?
Supplementary Question 1
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, kwanza, kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna ujenzi mkubwa unaoendelea katika barabara za Morogoro, Kilwa, Bagamoyo na Pungu, lakini Serikali inatoa hati pamoja na vibali vya ujenzi kwa wananchi hawa wanaojenga pembezoni mwa barabara. Inapotokea wakati wa upanuzi wa barabara wananchi hawa wanaambiwa kwamba wamefuata barabara na hawastahili kulipwa fidia.
Je, kwa nini sasa Serikali wanatoa vibali kwa wananchi wanajenga mpaka wanamaliza nyumba hasa nyumba ya ghorofa mpaka inaisha pasipo kutoa ushauri wa kitaalam kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wananchi wanapenda maendeleo, wanajenga majumba makubwa ya ghorofa na nyumba za kawaida pembezoni mwa barabara lakini wanakosa kuelewa matumizi sahihi ya ardhi iliyopo. Je, Serikali wako tayari kutoa elimu kwenye kata, vijiji na mitaa ili kuwaeleza wananchi wetu waelewe matumizi bora ya ardhi kuingana na mipango ya maendeleo iliyopangwa na Serikali? (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, la kwanza ameuliza juu ya utolewaji wa vibali katika maeneo ambayo pengine hayakustahili kupewa vibali hivyo na baadaye yanabomolewa. Naomba kupitia Bunge lako hili Tukufu nitoe wito kwa halmashauri zote; kwa sababu tuna imani kila halmashauri inazo ramani za mipango miji katika maeneo yao; na ujenzi wowote unaoendelea unaangalia ile Mipango miji yao au Master Plan ambazo zinakuwepo zinasema nini katika maeneo hayo. Hili limekuwa likifanyika maeneo mengi na Mwanza ikiwemo.
Mheshimiwa Spika, sasa niseme kwamba, katika hili na ambalo tumekuwa tukilitolea maelekezo mara kwa mara. Pale ambapo uongozi wa Halmashauri husika utatoa kibali tofauti na matumizi ya eneo ambalo limetajwa au ambapo mtu kapewa kibali kwenda kujenga, halmashauri hiyo ijue itakuwa tayari kulipa fidia hasa kwa wale ambao waliohusika katika kupeleka vibali ambavyo vinakwenda kinyume na utaratibu kwa sababu tunazo ramani na master plan zetu. Kwa hiyo, niseme hili ni jukumu la kila Halmashauri kujiridhisha kwanza kabla ya kutoa vibali vya ujenzi kwenye maeneo. Tusingependa wananchi wapate hasara kwa kujenga halafu baadaye anabomolewa.
Mheshimiwa Spika, swali la pili amezungumzia kuhusu kutoa elimu sahihi kwa wananchi ili watambue. Niseme tu kwamba, sasa hivi tuna miji zaidi ya 13 ambayo inaandaa mipango miji yake, I mean kwa maana ya kuwa na master plan. Kabla ya master plan ile kutekelezwa lazima kunakuwa na ushirikishwaji wa jamii, ukiangalia sasa hivi katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na maeneo mengine ambayo master plan zinaendelea ikiwemo na Musoma lazima kunakuwa na ushirikishwaji wa wananchi. Unapowashirikisha pale ndipo wanatakiwa na wao pia watoe mawazo yao ili kuweza kuona na watambue master plan ile inakwenda kujengeka namna gani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niseme elimu itaendelea kutolewa. Wizara tunavyo vipindi maalum ambavyo mara kwa mara Maafisa wetu huwa wanakwenda wanatoa na hata tunapofanya ziara tunatoa, kwa hiyo hili litaendelea kufanyika. Vile vile tuziombe, halmashauri kwa sababu unapokwenda ku- implement master plan utekelezaji wake lazima jamii iliyopo pale itambue. Pale mtu anapojenga nyumba ya kawaida wakati kwenye master plan yako inaonesha ni ghorofa, gharama ile utaibeba wewe ambaye unatoa kibali kujenga eneo ambalo tayari una Master Plan na bado unakiuka taratibu.
Name
Salma Mohamed Mwassa
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Kumekuwa na ujenzi wa nyumba za ghorofa kando kando ya barabara kuu na Serikali ndiyo inatoa vibali vya ujenzi huu ambapo baada ya muda maghorofa hayo yanaweza kubomolewa na mwenye jengo kulipwa fidia. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuainisha maeneo yenye mipango ya maendeleo ili kuepuka gharama kubwa ya kulipa fidia?
Supplementary Question 2
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante
kwa kuniona. Sheria ya Fidia inasema kwamba watu walipwe ndani ya miezi sita, lakini katika Jiji la Dar es Salaam kwa sasa kuna uwekaji wa alama za X kwenye nyumba za wananchi usioeleweka na alama hizo zinawekwa hazina muda maalum hasa kwenye nyumba ambazo zipo pembezoni mwa barabara na maeneo mengine katika Jiji la Dar es Salaam. Unakuta alama ya X imewekwa miaka mitano, mitatu au sita; yule mwananchi haelewi hii alama ya X inakuwaje? Naomba niiulize Serikali, ni kwa nini alama ya X inapowekwa yule mtu asilipwe fidia ndani ya miezi sita awe ameshalipwa na kuondoka katika eneo lile? (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni wazi Sheria ya Ardhi kifungu namba 13(2) na (3) kinaelezea mtu unapotaka kuchukua eneo fidia ilipwe ndani ya miezi sita na kama hukulipwa ndani ya miezi sita basi kuna hali halisi ya kuweza tena kuchaji gharama hiyo kulingana na rate iliyopo katika financial institution kwa kipindi hicho. Hata hivyo, hii imekuwa haifanyiki kutokana pengine na wachukua ardhi wenyewe kutokuwa tayari kufanya ile kazi kwa wakati. Hii tumeisemea na tumeipigia kelele na ndiyo maana kukaja na ile Sheria ya Uthamini ambayo tumeifanya hapa; ambayo inazungumzia suala la baada ya miaka miwili kama mtu hajaweza kulipa fidia ule uthamini uliofanyika mwanzoni wote unakuwa umefutika. Hii ilikuwa imefanyika hivyo mwanzoni kwa sababu ile sheria ilikuwa inaachia mtu anaweza akaenda miaka 10 mpaka 20 hajalipa.
Mheshimiwa Spika, sasa tunasema baada ya kupitisha ile sheria hivi sasa ndani ya kipindi kilichotajwa lazima fidia ile ilipwe na hakuna kuchukua ardhi ya mtu kama hujalipa fidia, hili kila siku tunalirudia. Tunasema kuanzia sasa, kwa sababu wananchi wengi wameteseka katika masuala ya ulipaji fidia. Hakuna kuchukua ardhi ya mtu kama mwekezaji au yeyote anayechukua ardhi ile hajaweza kulipa fidia kwa gharama iliyopo katika soko baada ya kuwa imefanyiwa uthamini kwa kipindi hicho. Vinginevyo wananchi tunasema wasitoe maeneo yao kama hawajathibitishiwa katika kutoa eneo lile.
Mheshimiwa Spika, suala lingine katika hilo hilo, kuna shughuli zingine ambazo zinafanyika za kiserikali ambazo ukiing’ang’ania ile ardhi unakuwa umekwamisha mambo mengine. Sisi ndani ya Serikali tunajipanga vizuri kuona kwamba yale maeneo ambayo yanatumika kwa ajili ya manufaa ya umma tutayafanyia utaratibu wa haraka na mapema ili wananchi wale wasiweze kulalamika.