Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Elias John Kwandikwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Primary Question
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:- Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mauaji ya wazee na walemavu wa ngozi kutokana na sababu mbalimbali. (a) Je, ni idadi ya watu wangapi waliopoteza maisha katika Jimbo la Ushetu kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015? (b) Je, mauaji ya makundi haya yanapungua au yanaongezeka katika Jimbo la Ushetu? (c) Je, Serikali imeshirikisha vipi jamii kupiga vita mauaji haya, vikiwemo vikundi vya dini, walinzi wa jadi (sungusungu) na uongozi wa kimila Jimboni Ushetu?
Supplementary Question 1
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali.
Kwa kuwa tuna kituo cha polisi chenye hadhi ya Wilaya, hiki ni kituo kipya na bado kina changamoto, tunao askari wachache 38 tu, lakini askari hawa wanafanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wananchi, Madiwani na Halmashauri.
Pia kwa kuwa hakuna vifaa/vitendea kazi yakiwemo magari, kwa sasa Halmashauri ya Ushetu tumewapa Polisi jengo pamoja na gari. Tunahitaji kuwa na vituo vidogo kandokando kwa sababu Jimbo la Ushetu ni kubwa, linapakana na majimbo nane na tumedhamiria kutokomeza kabisa mauaji ya wazee na walemavu.
Je, ni lini Serikali itatupatia vifaa ikiwemo magari pamoja na askari ili angalau tufikishe askari 100. Hii itasaidia sana pia kupunguza makosa katika majimbo nane ambayo napakana nayo. Ni lini sasa Serikali itatusaidia?
Swali la pili, kwa kuwa tunazo jitihada za kujenga vituo vidogo kando kando katika maeneo ya Kata ya Chambo, Kata ya Ulowa, Kata ya Ubagwe na kata Idahina na kwa kuanzia katika Kata ya Idahina tuna jengo ambalo tumetumia nguvu za wananchi, Mbunge pamoja na wachimbaji wadogo, na litaweza kuwa accommodate ofisi pamoja na askari wapatao watano.
Je, Serikali iko tayari sasa kutusaidia kukamilisha jengo hili ili tuweze kupata askari tuweze kuimarisha masuala ya usalama katika eneo hili ambalo linakuwa kwa kasi?Ahsante. (Makofi)
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake kubwa alizonazo za kuhakikisha kwamba hali ya usalama katika Jimbo lake inaimarika, amekuwa akifuatilia kwa karibu sana maendeleo ya vyombo vyetu vya usalama katika Jimbo lake naomba nimpongeze sana kwa niaba ya wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kuongeza idadi ya askari na vitendea kazi vingine ikiwemo magari, naomba nilichukue hilo nikitambua kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tuna matarajio ya kuongeza na kuajiri vijana wapya japokuwa ni kweli tuna uchache wa askari siyo tu katika Jimbo lake, ni katika maeneo mengi nchi nzima. Kwa hiyo, tutazingatia kulingana na mahitaji ya nchi nzima ili tuone jinsi gani tunaweza kufanya kusaidia jitihada za askari wetu pale katika Jimbo lake pamoja na usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jengo lake ambalo amezungumzia vilevile kama nilivyokuwa nikijibu mara nyingi hapa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba majengo ya hivi vituo vyetu vya vyombo vya usalama vyote ni malengo ya Serikali kuhakikisha kwamba vinaimarika, tuna upungufu huo vilevile katika maeneo mengi nchini. Nichukue fursa hii kumhakikishia kwamba jitihada zinafanyika hata nje ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tumekuwa na utaratibu wa kutumia taasisi yetu ya Jeshi la Magereza kuweza kuanza ujenzi kwa kutumia rasilimali za maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge kulitumia Jeshi la Magereza katika eneo lake kwa ajili ya kuanza harakati za ujenzi wa kituo hicho na baadaye pale itakapofikia katika hatua nzuri tunaweza kulikamilisha kwani katika mwaka huu wa fedha tumetenga bajeti fedha za kutosha kuhakikisha kwamba tunamaliza maboma yote ambayo yamejengwea kwa nguvu za wananchi pamoja na nguvu na vyombo vyetu vya usalama kwa kutumia rasilimali za maeneo yale.(Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved