Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
John John Mnyika
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Kibamba
Primary Question
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:- Serikali inapaswa kuharakisha upimaji wa ardhi na utoaji wa hati za viwanja katika Jimbo la Kibamba ili kuepusha makazi holela. (a) Je, ni maeneo gani ambayo hayajapimwa na lini yatapimwa? (b) Je, kuna mpango gani wa kupunguza gharama na muda wa upimaji na utoaji wa hati ili kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma tajwa?
Supplementary Question 1
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, haijui mipaka ya Jimbo la Kibamba, kwa sababu kati ya kata alizozitaja kwamba ni za Jimbo Kibamba, kata zifuatazo ni za Jimbo la Ubungo. Kata ya Ubungo, kata ya Mburahati, kata ya Kimara na kata ya Makuburi. Kwa hiyo, maana yake Kata tano alizozitaja kwenye jibu siyo za Jimbo la Kibamba na siyo sehemu ya swali nililouliza. Ni aibu zaidi kwamba kasi ya upimaji ni viwanja 186 tu, kwa upande wa kata ya Kibamba. Sasa nina maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali la msingi halijajibiwa, je, Serikali iko tayari sasa kuainisha kata kwa kata, mtaa kwa mtaa, kwa upande wa Jimbo la Kibamba, ratiba ya kuharakisha upimaji ili kuepusha sehemu hii ambayo ni Jimbo jipya kabisa nalo kuwa na makazi holela na maeneo mengi yasiyopimwa? (Makofi)
Swali la pili, matatizo haya ya kuchelewa upimaji, na udhaifu katika upimaji yamekwisha leta madhara sasa hivi tunavyozungumza ambapo Serikali imetoa notice na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu kwa wananchi kutoka Stop Over mpaka maeneo ya Kiluvya mita 121 kutoka katikati ya barabara kwa maana ya mita 240 ukijumlisha pande zote mbili za barabara, wananchi wote hawa wanatakiwa kubomoa nyumba zao hivi sasa tunavyozungumza, lakini ninayo hukumu ya Mahakama ya mwaka 2013 yenye kuonesha kwamba wananchi hao walihalalishwa na hati za vijiji kwenye Kijiji cha Kimara, kijiji cha Mbezi na Kijiji cha Kibamba.
Je, Serikali iko tayari maana hili jambo tumeishauriana muda mrefu, kwa sababu sasa hivi ni dharura hili jambo, kutoa kauli ya kusitisha notice hii ya TANROADS kwanza ili majadiliano yafanyike kuhusu utata huu wa upana wa barabara, maana maeneo mengine yote ni mita 60 lakini hapa peke yake ni mita 121.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu ya Serikali. (Makofi)
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mnyika, siyo aibu kwa sababu tunajua nini tunachokifanya. Hapa tulikuwa tunazungumzia matatizo ya Watanzania kama Ofisi ya Rais – TAMISEMI na unafahamu Jimbo lako limegawanywa juzi tu.
Mheshimiwa Mnyika, ukisema aibu na wakati wewe ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani na taarifa tunazipata mwaka mzima toka Baraza halijaanza, ndiyo maana mambo mengine ya msingi unashindwa kuyasimamia kwa wananchi wako, hilo ndio jambo la msingi lazima tukubaliane nalo.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndiyo hoja ya msingi kwanza, mipango ya Serikali tumesema nimezungumza maeneo mbalimbali na jinsi Serikali inavyochukua hatua mbalimbali na ndiyo nimekuambia Mheshimiwa Mnyika hii ni politics, haya ni mambo rahisi hata hayataki nguvu haya. Kikubwa zaidi naomba niwasihi Waheshimiwa Wabunge, katika mipango hii ya upimaji katika maeneo yetu tunapaswa wenyewe tuwe karibu jinsi gani tutafanya ili maeneo yetu yapimwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema katika jibu letu la msingi, leo hii ukiaangalia maeneo mengine wamefanya vizuri kwa kutumia wataalam wao mipango shirikishi zaidi na kutumia makampuni mbalimbali, kufanya mipango shirikishi ambayo mwisho wa siku inaweza kujibu jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba Serikali imesikia kilio chako Mheshimiwa Mbunge, wala usiwe na hofu, itajitahidi kufanya kila liwezekanalo eneo la Jimbo la Kibamba kama nilivyosema, nashukuru sana, kwa sababu timu sasa iko site na Wizara ya Ardhi siku moja ilikuwa inajibu kijumla yake swali la ardhi katika Wilaya ya Ubungo kwa ujumla wake. Naomba nikutoe hofu kwamba, Serikali itashirikiana vema na Baraza la Madiwani kwa kuangalia jinsi tutakavyofanya ili tuweze kupima, ambayo itakuwa ni manufaa makubwa kwa wananchi wako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la upana wa barabara. Upana wa barabara upo kwa mujibu wa sheria, bahati nzuri wenzetu wa Wizara ya Ujenzi hapa ndiyo wanajua sheria ukianzia ile sanamu pale Posta mpaka unafika Ubungo kuna upana maalum ambao umezungumzwa kisheria, na ukitoka pale mpaka ukija pale Kimara Temboni kuna sheria inaelekeza. Ukitoka pale mpaka unafika maeneo ya karibu na Mto Ruvu sheria inazungumza hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile kuna notice nadhani wenzetu wa Wizara ya Ujenzi wanajua nini wanachokifanya katika eneo lao hilo watatoa maelekezo kwa kadri wanavyoona kwamba inafaa, kutokana na notice iliyotolewa na utaratibu wa kisheria jinsi ulivyo katika eneo lao la kazi. (Makofi)
Name
Saed Ahmed Kubenea
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Ubungo
Primary Question
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:- Serikali inapaswa kuharakisha upimaji wa ardhi na utoaji wa hati za viwanja katika Jimbo la Kibamba ili kuepusha makazi holela. (a) Je, ni maeneo gani ambayo hayajapimwa na lini yatapimwa? (b) Je, kuna mpango gani wa kupunguza gharama na muda wa upimaji na utoaji wa hati ili kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma tajwa?
Supplementary Question 2
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, majibu ya Serikali yameonesha kwamba eneo pekee lililopimwa katika Jimbo la Ubungo ni eneo la Kimara ambalo kumepimwa viwanja 3,196 au nyumba 3,196; je, Serikali inasemaje katika maeneo yaliyobaki ya Makuburi, Manzese, Ubungo na maeneo mengine ya Jimbo la Ubungo?
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri amejibu vizuri. Maswali haya yanapaswa kuwa ndani ya mipango ya Halmashauri husika, kama tunavyopanga mipango juu ya shughuli nyingine za maendeleo ndani ya Wilaya basi tujipangie mipango ya namna ya kupima na kupanga miji yetu ndani ya Wilaya zetu, haiwezi kuanzia hapa. Nataka niwaambie wote wawili hata huo mnaosema Mheshimiwa yangu Kubenea tulikuwa wote hapa Kimara, hatupimi pale tunarasimisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam ni moja ya miji ambayo imejengwa siku nyingi, imejengwa vibaya ni makazi holela. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa ni kurasimisha angalau wananchi waweze kupata barabara za kupitisha huduma zao, waweze kupata hati kidogo ili angalau nyumba zao thamani zile zisipotee, angalau thamani ya mali waliyowekeza pale na zile hati ziwasaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imekuja na mpango mbadala wa kuwawezesha hawa maskini kurasimisha mali zao ili angalau ziwasaidie katika kujitegemea. Kwa hiyo, tunafanya zoezi la urasimishaji, hapa unaposema ndugu yangu Kubenea tulienda wote Kimara tunafanya zoezi la urasimishaji na haya anayosema ndugu yangu tunafanya zoezi la urasimishaji, upimaji mpya utafanywa Dar es Salaam baada ya kumaliza master plan, tuliyonayo ni ya mwaka 1979, sasa hivi tunaandaa master plan tume-engage wataalam, tukishamaliza master plan ambayo itashirikisha viongozi wote wa Dar es Salaam na wananchi wa Dar es Salaam, Dar es Salaam itapangwa upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ni zoezi la urasimishaji kuwawezesha wananchi kutoka kwenye hadhi ile ya makazi holela angalau waitwe nao wanaishi kwenye makazi rasmi. Hilo ni zoezi ambalo linaendelea sasa na zoezi hili ni shirikishi, wananchi kwenye mitaa wanashiriki wenyewe, wanachangia gharama wenyewe, kupanga maeneo yao katika mitaa yao. Kwa hiyo naomba zoezi hili tushirikiane na ninyi tuanzie kwenye mitaa kujadili halafu Wizara hizi mbili tushirikiane na mipango yenu. (Makofi)