Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Primary Question

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:- Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani, Wabunge na Rais huchaguliwa na watu wanaoishi katika eneo la mipaka yake na wote hawa wanafanya kazi ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao. Je, Serikali imeridhika na malipo wanayopata Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani?

Supplementary Question 1

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Serikali kwa maana ya TAMISEMI wametoa muongozo katika makusanyo yale ya Halmashauri kwa maana ya kwamba asilimia 60 zinapaswa kwenda kwenye maendeleo, asilimia 20 zinapaswa kwenda kwenye kata, asilimia 10 zinapaswa kwenda kwa vijana na wakina mama, kwa hiyo Halmashauri inabakia na asilimia 10 peke yake ambayo ndiyo sasa ilipe mishahara na kuendesha Halmashauri. Je, kutokana na hali hiyo ni kwanini sasa hawa Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wasilipwe moja kwa moja kutoka Serikali Kuu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ukiwaangalia
hao Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanayo majukumu mengi na makubwa kwa hiyo hata wakati mwingine wanashindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na tabu walizonazo hasa hasa za usafiri. Je, Serikali sasa imejiandaaje kuhakikisha kwamba nao inawawezesha kupata usafiri ili waweze kutekeleza majuku yao ya kila siku?(Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ni kwamba kwanini sasa hawa Wenyeviti wasilipwe moja kwa moja kutoka Serikali Kuu na msingi umesema kwamba kwa sababu kulikuwa na suala zima la mgawanyo wa zile fedha kwamba asilimia 60 ziende katika maendeleo;
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipowasilisha bajeti yetu mwaka Mheshimiwa Waziri alitoa ufafanuzi hapa kwa kina kwamba hili limeonekana kwa sababu lilikuwa hoja ya msingi ya Waheshimiwa Wabunge, ndiyo maana tumetoa maelekezo. Mheshimiwa Waziri alizungumza wazi hapa kwamba fedha hizi sasa zitagawanyika tofauti, kwamba kwa baadhi ya Halmashauri hasa zile ambazo uwezo wake ni mdogo, sasa asilimia 60 zitakwenda katika matumizi haya mengine na asilimia 40 itakwenda katika maendeleo, huu ndio ufafanuzi kulingana na bajeti ya mwaka huu tuliyoipitisha hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo, lengo letu kubwa katika dhana ya ugatuaji wa madaraka ni kutafuta jinsi ya kufanya katika kuongeza nguvu za Halmashauri za kuweza kukusanya mapato. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mathayo tutaendelea kulisimamia hilo, lakini kubwa na la msingi ni jinsi ya kufanya katika kukusanya vizuri mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ya pili, kuhusu vyombo vya usafiri; ni kweli, tukiangalia viongozi wetu wana changamoto kubwa ya usafiri, kwa sababu kama Madiwani wanafanya kazi kubwa, lakini hili naomba tulichukue sisi Serikali kwa sababu ni jambo ambalo naona ni la msingi hapo baadaye kwa kupitia Halmashauri zetu ni kwa jinsi gani tutafanya kupitia mifuko mbalimbali ili aangalau kuwezesha Waheshimiwa Madiwani waweze kupata vyombo vya usafiri. Hata hivyo jambo hili tutashirikishana vizuri kupitia katika Serikali zetu za Mitaa.

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:- Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani, Wabunge na Rais huchaguliwa na watu wanaoishi katika eneo la mipaka yake na wote hawa wanafanya kazi ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao. Je, Serikali imeridhika na malipo wanayopata Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani?

Supplementary Question 2

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kama ilivyoulizwa katika swali la msingi, baadhi ya Madiwani wanaruhusiwa kuingia katika vikao vya Halmashauri husika lakini baadhi ya Wakurugenzi imekuwa vigumu kwao kuwaruhusu, na mfano mzuri ni Mheshimiwa Stella Allex Ikupa ambaye anapaswa kuingia katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Ilala, lakini mpaka leo hii imekuwa vigumu kuhudhuria vikao hivyo.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri unatoa kauli gani ili aweze kuingia katika Baraza hilo na kuwatendea haki watu wenye ulemavu katika kuhakikisha kwamba masuala yao yanaingizwa katika bajeti husika?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii nadhani kwamba imeshakwisha, kwa hiyo kama kuna ukakasi wa aina yoyote ofisi yetu italifanyia kazi; lengo kubwa ni kwamba mtu aliyepewa dhamana katika eneo hilo aweze kushiriki vizuri hasa lile kundi analoliwakilisha, kundi la walemavu.

Name

Joshua Samwel Nassari

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Mashariki

Primary Question

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:- Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani, Wabunge na Rais huchaguliwa na watu wanaoishi katika eneo la mipaka yake na wote hawa wanafanya kazi ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao. Je, Serikali imeridhika na malipo wanayopata Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani?

Supplementary Question 3

MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna watu ambao wanasaidia kazi za uongozi kwenye nchi hii nafikiri hata kuliko sisi Waheshimiwa Wabunge na wamekuwa msaada mkubwa sana kwetu kwenye kutekeleza majukumu yetu kwenye majimbo na kwenye Halmashauri zetu ni viongozi wa Serikali za Mitaa kwa maana ya Wenyeviti wa Vijiji, lakini ambao wanafanya kazi kubwa zaidi ni Madiwani kwenye Halmashauri zetu. Hata hivyo ukweli ni kwamba unapoangalia maslahi ambayo hawa watu wamekuwa wakiyapata ni madogo sana na mara nyingine Serikali inaamua ku-temper nayo kwa makusudi kabisa hata kuingilia ule utendaji wa ndani wa Halmashauri wa moja kwa moja inapokuja suala la matumizi ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila wakati tumekuwa tukihoji kwenye Bunge hili kwamba ni lini Serikali inakwenda kuboresha maslahi ya Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Madiwani ili nao waweze kuishi kama viongozi na waonekane kwamba kweli kazi wanayoifanya inathaminika kwenye Taifa? Kila siku Serikali inasema…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, Serikali naomba iji-commit kabisa kwamba ni lini watakwenda kuboresha kabisa haya maslahi ya wenyeviti wa vijiji pamoja na Madiwani na waache kusema tutaliangalia, tutaliangalia………..

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali tunatambua viongozi hawa wa ngazi za chini, Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Madiwani wanafanya kazi kubwa sana katika nchi hii, maendeleo yote yanasimamiwa na wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni kweli pia kwamba maslahi ya watumishi mbalimbali wa umma pia watumishi wa kisiasa kila mmoja anasema hayatoshi, tuongeze. Hata Wabunge wanasema hivyo, walimu wanasema hivyo na wote wanasema tuongeze. Hili litawezekana endapo uchumi wa nchi utatengemaa. Katika mazingira ya sasa, kinachowezekana na ambacho sisi tunaona kinapaswa kufanywa na Serikali kwa ngazi hizi za chini ni ile asilimia 20 tunayoipeleka kwa ajili ya kuendesha ofisi, lakini pia huwa kuna posho ambayo inapatikana. Asilimia 20 ya kiasi cha shilingi bilioni moja au Halmashauri zingine zinakusanya makusanyo ya ndani mpaka shilingi bilioni 50 si hela kidogo zikigawanywa vizuri Kwa hiyo mimi niseme tu kwamba tunatambua mchango wa viongozi hawa wakati ambapo uchumi utatengemaa tunaweza tukaongeza lakini kwa sasa utaratibu ndiyo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgawanyo wake kama tulivyosema, 40% zitakwenda kwenye miradi wa maendeleo kwenye fedha ile ya own source, lakini 10% kwa mikopo kwa ajili ya wanawake na vijana na 20% itakwenda kwa ngazi za chini na hiyo 30% itatumika katika kuendesha Halmashauri. Hii ndiyo hesabu mpya ambayo tumeiweka baada ya bajeti yetu tuliyoisoma hivi karibuni.