Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Immaculate Sware Semesi
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. MARY D. MURO) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Mbuga ya Saadani iliyoko Mkoa wa Pwani ili kuongeza pato kwa wananchi walio kando ya mbuga hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ahsante kwa majibu Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza, napenda kujua Serikali imefikia hatua gani kwenye kulipa fidia au kuboresha mazingira ya wanakijiji wa Uvinje vis-a-vis TANAPA?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali imejipangaje kwa vijiji vile vinavyozunguka au vilivyo ndani ya Saadani kuona vinashirikishwaje katika shughuli za kitalii ili kudumisha au kuboresha uchumi wao? (Makofi)
Name
Prof. Jumanne Abdallah Maghembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Answer
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu fidia kwenye vijiji alivyovitaja. Kwa kuwa hadi nasimama hapa bado nilikuwa sijapata taarifa zilizokamilika kuhusiana na madai hayo, nimuahidi nikitoka hapa anipe kwa ufafanuzi vijiji hivyo ni vipi na kwa nini vinastahili fidia ili niweze kuangalia tumefikia katika hatua gani pale Wizarani kuweza kukamilisha utaratibu huo wa kuwalipa fidia ikiwa watakuwa wanastahili kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la namna gani Wizara au Serikali inashirikisha vijiji vinavyozunguka maeneo ya Hifadhi ya Saadani katika masuala ya kuendeleza vivutio, utaratibu wetu kwa kawaida ni kwamba kila wakati tunapofikiria kuanzisha mradi, wadau wa kwanza kabisa na hii nimeisema hata katika swali la msingi, kwamba uendelezaji wa vivutio katika hifadhi zote unashirikisha jamii zinazozunguka katika maeneo ya hifadhi na Serikali pamoja na mashirika binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata kwa upande wa vijiji alivyovitaja katika Hifadhi hii ya Saadani tumeweza kuwashirikisha kwa mujibu wa taratibu tulizonazo lakini kama ana mawazo ya kuweza kuipatia Serikali ili tuweze kuboresha zaidi namna ya kuweza kushirikisha wananchi hawa au wadau hawa wanaoishi kwenye maeneo ambayo ni jirani na hifadhi basi tupo tayari kupokea ushauri huo tuweze kuboresha zaidi taratibu zinazotumika katika kuboresha vivutio kwenye maeneo ya hifadhi.
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Primary Question
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. MARY D. MURO) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Mbuga ya Saadani iliyoko Mkoa wa Pwani ili kuongeza pato kwa wananchi walio kando ya mbuga hiyo?
Supplementary Question 2
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Ili kuboresha sekta hii ya utalii ni pamoja na kuboresha miundombinu yake. Ukiangalia hii mbuga ya Saadani barabara ambayo inaifikia mbuga ile ni mbovu na haipitiki kwa muda wote. Je, Wizara hii haioni haja sasa ya kukaa na Wizara ya Miundombinu ili kuhakikisha kwamba inaijenga barabara hii ya Tanga - Pangani - Saadani ili watalii waweze kufika kwa urahisi?Ahsante sana.
Name
Prof. Jumanne Abdallah Maghembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Answer
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli ili utalii uweze kwenda sawasawa, ili tuweze kupata idadi kubwa ya watalii, ili watalii wakija waweze kufurahia kuwepo kwenye hifadhi zetu na kwenye maeneo yetu ya vivutio, wakae muda mrefu zaidi ili waweze kutumia fedha zaidi na kuweza kuboresha pato zaidi ni lazima mazingira hapo ambapo tumeweka vivutio yawe bora zaidi ikiwa ni pamoja na miundombinu ya usafiri lakini pia hata malazi. Upande wa malazi kwa kiwango kikubwa hili ni eneo ambalo linafanywa au linatekelezwa na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miundombinu kama barabara ukweli ni kwamba eneo hili linatekelezwa na Serikali, lakini pia hata ndani ya Serikali, barabara zile ambazo zinaelekea kwenye hifadhi kutoka kwenye maeneo mengine ya miji jirani, hizi ni barabara ambazo zinatekelezwa kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kwa upande wa barabara ambazo ziko ndani ya hifadhi, kwa mfano barabara zilizoko ndani ya Hifadhi ya Saadani, hili ni jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara pamoja na matengenezo yake ya kuweza kuzifanya zipitike hili ni jukumu ambalo linafanyika na Wizara kwa kupitia Shirika la TANAPA ambalo ni Shirika la Hifadhi za Taifa. Katika bajeti ya mwaka huu TANAPA wametenga fedha kama ambavyo tunatenga kila mwaka kazi yake ni kuboresha miundombinu kwa maana ya kuboresha iweze kupitika mwaka mzima hata msimu wa mvua, lakini pale ambapo inawezekana kupasua barabara mpya kutegemeana na bajeti na uwezo wa kifedha, basi utekelezaji wa mradi huo utaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara aliyoitaja ya Tanga – Pangani – Saadani, hii ni barabara ambayo tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Miundombinu ili kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea na hasa pale ambapo bajeti itakuwa imeweza kuruhusu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved