Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Suala la madai ya walimu nchini limekuwa ni tatizo sugu hususan kwa walimu wa shule za msingi na sekondari. Je, Serikali imechukua hatua gani ili kumaliza tatizo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, lakini ni aibu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Majibu hayo ni ya Arumeru na siyo ya Mkoa wa Rukwa. Halafu mnajiita Serikali ya kazi tu, hapa! Swali hili sijaleta jana, lakini kwa sababu madai ya walimu yako nchi nzima, nitauliza maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa madeni kwa wakati walimu ambao wamekuwa wakilia kila siku na ni malalamiko ya kila siku!
Swali la pili, mpaka sasa walimu wanadai fedha walizosahihisha mitihani ya mwaka 2015 ya kidato cha nne, ni lini Serikali itawalipa walimu hawa na kuwatendea haki kama wafanyakazi wengine wa nchi hii?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niweke wazi, katika mchakato wa madeni ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI pale ina maswali zaidi ya takriban 15 ambayo yote moja kwa moja yanalenga katika suala zima la madai ya walimu na yote yanafanana fanana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo, kwa concern ya Mheshimiwa Mbunge siyo kwamba Serikali haiko makini, isipokuwa jambo hili limekuwa ni kilio karibuni kwa Wabunge wote. Kwa hiyo, suala la msingi ni jinsi gani tutafanya kutatua tatizo hili tuweze kulimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati uliopo, nilisema Serikali kwa awamu ya kwanza ilishalipa haya madeni, lakini naomba niwambie, katika madeni haya katika sehemu nyingine ni fake. Tunafahamu sasa hivi hata katika suala zima la mishahara hewa, mmeona jinsi ambavyo kuna matatizo makubwa, wengine wanaingiza ilimradi waweze kupata pesa. Kwa hiyo, Serikali imejipanga na ndiyo maana uhakiki umefanyika. Katika jibu langu la msingi nimesema kwamba kuna madeni yameshaanza kulipwa na ndiyo maana tulichokifanya ni kuelekeza Halmashauri zote zifanye uhakiki kwa haraka ilimradi walimu waweze kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tukiri kwamba madeni haya hata tukilipa lazima yataendelea kwasababu kila siku walimu wanahama na kila siku walimu wanaenda likizo. Jambo la msingi ni kwamba madeni yanapojitokeza, inapaswa sasa watu waweze kulipwa haki zao wanazostahili.

Name

Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Suala la madai ya walimu nchini limekuwa ni tatizo sugu hususan kwa walimu wa shule za msingi na sekondari. Je, Serikali imechukua hatua gani ili kumaliza tatizo hilo?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, tunatambua kwamba Serikali ina mzigo mkubwa sana kuhusiana na masuala ya madai ya walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza kwamba kuna zaidi ya 3,000 ambao wamestaafu mwaka 2014 na mwaka 2015, mpaka sasa hivi hawajalipwa mafao yao. Je, ni lini Serikali angalau mafao ya watu ambao wameshastaafu tayari wanahitaji walipwe warudi majumbani kwao watalipwa pesa hizi?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna Walimu wamestaafu, nami naomba nikiri kwamba hata katika Ofisi yangu kuna baadhi ya walimu walifika pale moja kwa moja kuleta madai yao. Kwa mfano, kuna mwalimu mmoja alikuwa akifundisha pale Bahi. Walimu wengi waliokuwa na changamoto, walikuwa katika Mfuko wa PSPF.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imetoa maelekezo katika Mfuko wa PSPF kwamba haraka iwezekanavyo walimu wote waliokuwa wanadai, wahakikishe stahili zao zimelipwa, kwa sababu Serikali imefanya mchakato mkubwa sana kuiwezesha PSPF katika madeni iliyokuwa inadai kwamba iweze kupata mafungu ya kutosha ilimradi PSPF iendelee kulipa madeni na Serikali imetimiza hilo.
Sasa naomba nitoe agizo kwamba Mamlaka zinazohusika katika hii mifuko zihakikishe kwamba Walimu wote ambao waliokuwa wanadai waweze kupata stahili yao. Siyo jambo jema kutokuwalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, mwalimu mmoja kutoka pale Morogoro alizimia kabisa kwa kudondoka kwasababu hakupata mafao yake. Ndiyo maana tumetoa maelekezo mazito na ni imani yangu kwamba Mfuko wa PSPF kwa sababu umeshaanza kupata mafungu yale yaliyokuwa yanadai Serikalini, iwalipe walimu wetu ilimradi waendelee kuishi maisha mazuri.