Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. JAMES F. MBATIA) aliuliza:- LEKIDIA imeweza kushirikiana na wananchi wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki na kufanikiwa kukarabati barabara za kata hiyo zenye urefu wa kilometa 17 kwa gharama ya shilingi milioni nane, lengo kuu ni ujenzi wa barabara inayoanzia Uchira hadi Kolaria yenye urefu wa takribani kilometa 12 kwa kiwango cha lami; na LEKIDIA wamefanikiwa kufanya harambee na kupata shilingi milioni 130 ambapo shilingi milioni 60 zimetumika kununua mapipa 300 ya lami na kubakiwa na shilingi milioni 70. Je, Serikali itashirikianaje na LEKIDIA kutekeleza mradi huo kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, LEKIDIA imekuwa ikishirikiana na wananchi katika kuibua vipaumbele vya maendeleo katika Kata ya Kirua Vunjo Mashariki kwa muda mrefu na kipaumbele cha sasa ni hii barabara ya Uchira - Kisomachi - Kolaria ambao wamejitahidi kuchanga fedha na sasa wana lami pipa 300. Kipaumbele chao ni kwamba hii barabara ijengwe kwa kiwango cha lami.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kusaidia ili lami hii isije ikaharibika kujenga walau hatua kwa hatua kilometa tano na baadaye kilometa nyingine tano ili hatimaye hii barabara iweze kukamilika kwa kiwango lami badala ya kutumia fedha nyingi kwa ukarabati mara kwa mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wamekuwa wakishiriki sana katika kuchangia maendeleo, wamekuwa wakichangia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, shule na kadhalika. Katika Jimbo langu la Rombo karibu kila kijiji kuna miradi ya maendeleo inayoendelea kwa michango ya wananchi lakini kwa upande wa Serikali fedha zimekuwa haziendi kwa wakati jambo ambalo sasa linawavunja moyo wananchi.
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu upelekaji wa fedha za maendeleo jinsi ambavyo zimekubaliwa kwenye bajeti ili kuwatia moyo wananchi hao waendelee kuchangia shughuli za maendeleo ambazo tayari zimeshaanza?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli LEKIDIA wamechanga wamenunua mapipa takribani 340 kwa rekodi niliyokuwa nayo. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema kwa sababu sasa hivi tumeunda Wakala mpya wa TARURA na bahati nzuri tumepata Meneja maalum wa mradi katika Halmashauri ya Rombo na katika Halmashauri zote Tanzania. Meneja hawa jukumu lao sasa ni kufanya needs assessment katika kila Halmashauri. Tuagize Meneja wetu apitie barabara hiyo then ataleta tathmini halafu tutajua nini cha kufanya katika barabara hiyo. Kwa hiyo, ni jukumu kubwa la Serikali kuhakikisha barabara hizi zote zinafanyiwa matengenezo. Kwa hiyo ni commitment yetu Serikali kwa Tanzania nzima, hili jambo tutaenda kulifanya nikitambua juhudi kubwa ya wananchi wanayoendelea kuifanya, lazima tuwaunge mkono. Kwa hiyo, kazi itafanyika baada ya tathmini ya Mameneja wetu walioko site kuangalia kipi kilichopo na kipi kifanyike katika utaratibu gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala zima la upelekaji wa fedha, nimesema hapa kwa mfano fedha za barabara tumetenga karibuni shilingi bilioni 263 lakini hizi kuna fedha za barabara zenye vikwazo lakini zingine za road fund na maeneo mbalimbali. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha tunapata fedha hizi na bahati nzuri jana tulikuwa na Waziri wa Fedha katika kikao chetu cha mambo ya lishe amesema commitment ya Serikali katika mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha fedha zote za maendeleo zinafika katika maeneo husika. Kwa hiyo, ondoa hofu, jukumu letu sasa hivi naomba tuungane mkono wote kwa pamoja tukusanye mapato, tulipe kodi na mwisho wa siku kwamba fedha hizo zitapelekwa katika vijiji vyetu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma nzuri katika maeneo mbalimbali.