Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAY aliuliza:- Katika mwaka wa fedha 2013/2014, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilipeleka maombi maalum ya fedha za ujenzi wa daraja la Gunyoda na wakati huo kutokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Mbulu kupata Wilaya mbili, daraja la Gunyoda limebaki kuwa kiungo muhimu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mbulu vijijini. Serikali Kuu ilitoa kiasi cha Sh.100,000,000/= ambazo Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Mbulu kwa maagizo ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne fedha hizo zilielekezwa kwenye ujenzi wa maabara za sayansi katika Halmashauri zote nchini na kuacha daraja hilo bila kujengwa kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu haina uwezo wa kulijenga kwa fedha za ndani: (i) Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi wa daraja hilo ambalo ni kikwazo kikubwa kwa huduma za kijamii katika Halmashauri zote mbili? (ii) Kwa kuwa mabadiliko ya Tabianchi yamesababisha uwepo wa makorongo makubwa ambayo yako katika Kata za Gonyoda, Silaloda, Gedamara, Bargish, Dandi, Marangw’ na Ayamaami jambo linalosababisha jamii kukosa huduma za jamii, afya na utawala. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta fedha za dharura ili kusaidia janga hilo katika Halmashauri mbalimbali ikiwemo Mbulu Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wetu, hali hii ya makorongo na jiografia inayobadilika kutokana na tabianchi imesababisha jamii yetu hasa akinamama kukosa huduma za afya, watoto na wanafunzi kukosa masomo na kwa kuwa ni tatizo la nchi nzima, je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuona ni namna gani hata madaraja ya dharura kama yale ya chuma kuwekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, sasa hivi tunabadilika kutoka Watendaji wa Halmashauri na barabara zote zinazohudumiwa na Halmashauri zinapelekwa kwa Wakala wa Barabara za Vijijini. Je, ni kwa namna gani Serikali itatazama suala hili kutokana na kwamba fedha zinazotengwa ni kidogo sana kulingana na fedha za Mfuko wa Barabara kwa zile barabara zilizokuwa zinahudumiwa na halmashauri za wilaya katika maeneo ya vijijini ili fedha zitakazotengwa kwa dharura ziweze kusaidia tatizo hili na jamii ipate huduma stahiki na kwa wakati kuliko sasa ambavyo inapoteza maisha katika hali ya dharura na mvua nyakati za masika? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika nchi yetu kuna maeneo mbalimbali yanaathirika sana, na hasa katika Mkoa ule wa Manyara. Nikiri wazi kwamba eneo lile lina changamoto kubwa sana na wakati mwingine mvua ikinyesha utakuta sehemu nyingine mpaka mito inahama. Hali hiyo inajitokeza hata katika Mkoa huu wetu wa Dodoma na Mkoa wa Morogoro maeneo ya Gairo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa suala la upatikanaji wa madaraja ya chuma naomba tu niseme kwamba jambo hilo tumelipokea, japokuwa siwezi kusema kwamba hilo daraja litapatikana lini; lakini kwa haja ya kusaidia wananchi nadhani ngoja tuliweke hilo katika vipaumbele vyetu. Katika maeneo ambayo mwanzo yalikuwepo madaraja hayo, lakini leo hii yametengenezwa madaraja mengine, yale madaraja ambayo ni ya chuma yaliyohamishwa kule, tutaangalia jinsi ya kufanya, kwa kushirikiana na wenzetu wa TANROADS katika maeneo mbalimbali ili kuisaidia jamii yetu hasa kule Mbulu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la TARURA na bajeti; ni kweli katika fedha zinazokwenda za Mfuko wa Barabara; kwa sababu kuna ule mgawanyo wa sheria ambapo sheria ya TANROADS ni tofauti na sheria za halmashauri; lakini tumeunda Wakala mpya ambao una mikakati vile vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine linalofanyika ni suala zima la resource mobilization, kutafuta fedha, kwa hiyo naamini; katika kipindi hiki ambacho TARURA inaanza sasa naomba Waheshimiwa Wabunge muwe na imani, kwamba kazi nzuri itafanyika na mtakuja kuona kwamba kuna faida kubwa sana kwa kuanzisha Wakala huu; ambapo iliainishwa wazi katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwamba lazima katika kipindi hiki Wakala uanzishwe. Sisi jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tutasimamia Wakala huu ili uweze kufanya kazi vizuri ili wananchi waweze kupata huduma vizuri