Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

RITTA E. KABATI aliuliza:- Mwaka 2000 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini:- Je, hali ya utekelezaji wa mpango huo wa TASAF ikoje?

Supplementary Question 1

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukurru sana. Naomba tu nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze na kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuhakikisha kwamba kaya maskini angalau zinaweza kunufaika na huu mpango wa TASAF na kwa kweli katika mkoa wetu kaya nyingi zimeweza kunufaika na mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Manispaa yetu ya Iringa ambayo ipo Jimbo la Iringa Mjini tuna mitaa 192 na mitaa 98 tu ndiyo ambayo imeweza kunufaika na mpango huu na kuna mitaa 84 ambayo bado haijaweza kufikiwa kabisa na mpango huu wa TASAF; kwa mfano kwenye Kata ya Nduli kuna mitaa ya Kisoeyo, Mikoba, Kilimahewa, Mgongo na Njiapanda na kwenye Kata ya Kituli kuna mtaa wa Hoho; Kata ya Mkwawa kuna mtaa wa Mosi. Je, ni lini Serikali sasa itazifikia kaya hizi maana hali ya kaya katika mitaa hii ni mbaya kuliko hata zile ambazo zimeweza kufikiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nina swali lingine la pili. Kwa kuwa zipo kaya ambazo ni maskini na pia zina watoto wenye ulemavu. Kwa mfano katika Mkoa wetu wa Iringa kwenye Jimbo la Kilolo, Kijiji cha Lulanzi, kuna kaya ambayo ina watoto wanne, wote wana ulemavu na baba yao amepooza, mama yao sasa hivi amevunjika mguu. Je, katika mpango huu Serikali inawasaidiaje watu ambao tayari ni maskini na hawawezi kufanya kitu chochote katika kuwasaidia ili waweze kupata miradi? Kwa mfano labda kujengewa/kuwekewa mradi wa kisima ambao wanaweza wakauza maji wakiwa pale pale au wakapewa bajaji ili kuweza kunusuru kaya ambazo ni walemavu halafu ni maskini?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa niseme Serikali inakubali kwamba ni kweli si vijiji vyote, mitaa, kata na shehia nchini mwetu zimeweza kufikiwa na mpango huu wa TASAF. Ni takriban asilimia 70 tu kama nilivyoeleza ya vijiji, kata, shehia 9,989 ndiyo imefikiwa.
Napenda tu kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi sasa tumeanza taratibu, tunasubiri tu fedha zitakapotoka tuweze kuendelea na zoezi la kuwatambua na kuwaandikisha walengwa liweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sasa hivi tuko katika mpango tuliokuwa tunamalizia kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAf ambayo itamalizika mwaka 2018 kuelekea 2019; na sasa hivi tumeanza kusanifu awamu nyingine na tunaamini pia katika zoezi hilo nalo pia tutaendelea kufanya utambuzi na kujua program itakuwaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi tu fedha zitakapopatikana tutaweza kuendelea na zoezi la utambuzi wa walengwa na kuweza kuwaandikisha. Vile vile tutakapoendelea katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF tunaamini walengwa wataweza kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili amezungumzia kaya za watu ambao ni maskini ambao unakuta ni watu wenye ulemavu. Nipende tu kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati program hii ya TASAF awamu ya tatu inasanifiwa, suala zima la ulemavu halikuwa kigezo, kigezo kilikuwa ni umaskini lakini pia walikuwa wanaangalia umaskini wa kaya nzima kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika aina za ruzuku ambazo zinatolewa, ruzuku ya kwanza kabisa ambayo inatolewa bila hata masharti ya kuangalia kama familia ina watoto ilikuwa inatolewa kwa kaya nzima. Hata hivyo, nipende kusema, endapo kaya hiyo ina watu wenye ulemavu ambao wako chini ya miaka minane walikuwa wanakuwa treated au wanahesabiwa kama watoto wengine katika familia hiyo kwa mujibu wa ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa familia ambazo tumezikuta zina ulemavu wamekuwa wakishirikishwa katika miradi mbalimbali ya ajira ya muda. Hata hivyo, bado kama alivyoeleza yeye tulipata changamoto, ziko familia ambazo unakuta zina watu ambao wamezidi miaka 18, hata wakipewa ajira ya muda wengine ni mpaka wabebwe na hawawezi kufikia katika hiyo miradi mbalimbali. Niseme tu, tumelipokea na sasa hivi tunaposanifu awamu ya tatu ya mradi huu tutaendelea kuliangalia; kwamba katika awamu nyingine ni nini kifanyike kwa ajili ya watu wenye ulemavu lakini pia kwa sasa tunaangalia tunaweza tukawasaidiaje. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru (Makofi)

Name

Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

RITTA E. KABATI aliuliza:- Mwaka 2000 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini:- Je, hali ya utekelezaji wa mpango huo wa TASAF ikoje?

Supplementary Question 2

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. TASAF awamu ya pili ilianzisha mradi wa barabara ya Bungurwa-Msunga; leo ni zaidi ya miaka 10 na yapo makalvati yapo tayari zaidi ya 50. Je, ni lini sasa mradi huo au ujenzi wa barabara hiyo utatekelezwa?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kama nitakuwa nimemsikia vizuri; ni kwamba kuna mradi wa makalvati ambao ulikuwa haujamalizika na anataka kufahamu ni lini labda utatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kusema kwamba, tulipotekeleza TASAF awamu ya kwanza na awamu ya pili ni kweli iko miradi ambayo haikuweza kukamilika. Hata hivyo kwa maelekezo ambayo Serikali iliyatoa; tulitoa maelekezo kwa halmashauri zetu kuhakikisha kwamba wanaorodhesha miradi yote ambayo walikuwa hawajatekeleza au imeanza kutekelezwa lakini haijakamilika waweze kutengea fedha katika bajeti ili iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge tutafuatilia mradi huo wa kalvati katika Kata ya Misungwi ili tuone ni hatua gani imefikiwa ili mradi huo uweze kukamilika mapema.

Name

Nuru Awadh Bafadhili

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

RITTA E. KABATI aliuliza:- Mwaka 2000 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini:- Je, hali ya utekelezaji wa mpango huo wa TASAF ikoje?

Supplementary Question 3

MHE. NURU AWADH BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna baadhi ya kaya ambazo ni maskini sana lakini hazikuorodheshwa katika zoezi hili la kuwezeshwa katika mradi huu wa TASAF na kuna wengine wana uwezo lakini vile vile wanapokea pesa hizi za TASAF; je, Serikali inatuambia nini kuhusu hili?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA
BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nipende kusema kwamba ni kweli ziko kaya ambazo zilikuwa ni kaya maskini sana lakini unakuta haijaorodheshwa katika mpango na kinyume chake kaya ambazo si maskini au angalau zina ahueni ziliorodheshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika mchakato huu mzima wa uandikishwaji wa walengwa, ni mikutano yetu mikuu katika kata, kijiji na shehia ambayo inashirikishwa. Kwa kiasi kikubwa baadhi yao katika mikutano mingine mikuu unakuta itikadi za kisiasa zimetumika lakini pia unakuta kuna wengine wameorodheshwa wanaogopa kusema kuwabaini kwamba huyu ameingizwa lakini hastahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kutoa rai kwa wananchi wetu pamoja na mikutano mikuu, watakapoona kuna kaya zimeorodheshwa hazistahili basi waweze kutoa ushirikiano na waweze kuziondoa na tunaamini wataweza kufanya hivyo kwa sababu mpaka sasa tumeshaondoa zaidi ya kaya 73,851 na tutaendelea kufanya hivyo. Tunaomba wananchi waweze kutoa ushirikiano ili wawe ni wale tu ambao kweli wanazo sifa ndio waweze kunufaika na mpango huu. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.