Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yussuf Salim Hussein
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Chambani
Primary Question
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED) aliuliza:- Tanzania ni nchi yenye amani kubwa katika nchi za Maziwa Makuu. • Je, Serikali imejipanga vipi kuimarisha amani katika nchi yetu? • Je, mipaka yetu na nchi zenye mizozo na wakimbizi imeimarishwa kiasi gani kiulinzi?
Supplementary Question 1
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, sina wasiwasi na uimara, uwezo na weledi wa Jeshi letu katika kusimamia majukumu yake na ndiyo maana nje ya mipaka yetu sasa hivi tuko salama lakini ndani ya nchi yetu hali siyo salama na mifano miwili ya juzi ya Mbunge na Meja Jenerali inadhihirisha kwamba ndani ya nchi yetu tuna matatizo.
Je, ni kwa nini sasa Jeshi la Wananchi lisishiriki kikamilifu kukomesha matumizi ya silaha na mauaji ya raia wasio na hatia ndani ya nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, navyoamini mimi au navyoelewa, silaha za kivita zinamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na matumizi ya silaha ndani ya nchi yetu ni matumizi ya silaha za kijeshi ambazo zinatakiwa zimilikiwe na chombo hiki.
Je, kwa nini sasa Jeshi letu halioni ni wakati muafaka kutumia IO’s wake kuhakikisha kwamba inazikamata silaha zote za kivita ambazo zinatumika kwa matumizi mabaya ya kuua raia katika nchi yetu?
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kazi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni ulinzi wa mipaka lakini pale ambapo linahitajika au linaombwa kusaidia mamlaka nyingine iwe za kiraia au iwe Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama basi wanakuwa tayari kufanya hivyo. Tunavyozungumza ni kwamba mamlaka hizo ambazo ni Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vikihitaji msaada wa Jeshi, mara zote Jeshi linakuwa tayari kutoa msaada huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa itaundwa task force itakayojumuisha Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama ili kuweza kulifanyia kazi tatizo hili la uvunjifu wa amani ndani ya nchi. Sina shaka kwamba kazi hiyo imeanza na nataka niwahakikishie wananchi wa Tanzania kwamba jukumu hili litafanywa vyema ili hali ya usalama ipatikane ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la matumizi ya silaha za kivita; ni kweli kwamba silaha za kivita zinadhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kwamba ifanyike kazi maalum ya kuhakikisha kwamba silaha hizo zinapatikana, hiyo kazi inafanyika mara zote.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema bila shaka kwa kutumia task force hizi zilizoundwa kazi ya kuhakikisha kwamba raia au watu wengine wote ambao wanamiliki silaha za kijeshi au za kivita ambazo kikawaida au kitaratibu/ kisheria hawapaswi kuwa nazo zinapatikana na kurudishwa katika mamlaka zinazohusika. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved