Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Primary Question

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:- Mgodi wa GGM - Geita umekuwa ukitumia milipuko mikubwa wakati wa kulipua miamba ya dhahabu na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi jirani na maeneo hayo, kama wale wa eneo la Katoma. • Je, Serikali inafahamu kwamba nyumba za wananchi zinapasuka na baadhi ya watu huzimia kutokana na mshtuko? • Je, Serikali inalitatua vipi tatizo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nilitaka kumtaarifu kwamba hiyo Blast Monitoring Committee ilivunjwa na haipo tena, na ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, mgodi huu unaendelea na mfumo huu wa ku-blast ambapo kutokana na blasting hii watu wameendelea kupata madhara na tarehe 30 Machi watu nane walizimia, mama mmoja ambaye alikuwa ni mama lishe alizimia karibu siku tatu na kulazwa hospitali, lakini juhudi za Mkuu wa Wilaya za kuwataka watu wa mgodi kwanza walipie matibabu, lakini walipe gharama za mama lishe huyu ziligonga mwama baada ya watu wa mgodi kukataa.
Je, ni utaratibu gani utumike ili wanaoathirika kiafya waweze kulipwa fidia?
Swali la pili, kupitia Bunge na kupitia mikutano kadhaa Mheshimiwa Naibu Waziri na Nishati, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Waziri wa Nishati aliyeondoka walitoa maagizo mengi ya kuhakikisha kwamba waathirika, wa milipuko hii wanalipwa fidia katika eneo la Katoma, lakini mpaka sasa tunapozungumza ni mwaka mmoja umepita. Je, ni lini ahadi hii ya Serikali itatekelezwa?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Constantine anavyohangaika na matatizo ya wananchi hasa wa Katoma na Nyamalembo Compound na ninaamini wananchi wanaona juhudi zako Mheshimiwa Constantine.
Mgodi wa GGM kweli umekuwa ukifanya shughuli za ulipuaji na tarehe 30 mwezi Machi mwaka huu, ulifanya ulipuaji na kama alivyosema Mheshimiwa Constantine kuna mtu mmoja ambaye alipata madhara, kampuni tumeendelea kujadiliana nao na wanaangalia namna ya kufanya fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Constantine huyo mwananchi pamoja na wananchi wengine watafidiwa fidia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini, tuliunda timu kama ambavyo nimeeleza na kwa kweli tumetuma timu zaidi ya mara mbili na sasa hivi timu itakayokwenda sasa kutathmini yale wananchi wenye nyumba 890 ambao nyumba zao zimeathirika, tarehe 05 Juni watakwenda sasa kujadiliana pamoja na wenye nyumba zilizoathirika ili hatima yao ya kulipwa fidia iweze kufanyika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Constantine wewe pamoja na uongozi wa Halmashauri pamoja na mgodi na timu itakayoundwa mtashirikishwa ili wananchi hao sasa waanze kulipwa fidia zao.