Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:- Je, ni lini miradi ya umeme yenye zabuni Na. PA/001/2015/DZN/W/12 maeneo ya Chamazi Dovya, Kwa Mzala 1 – 3, Mbande kwa Masista na Chamazi Vigoa itakamilika ili wananchi wa maeneo hayo wapate umeme?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza nionyeshe masikitiko yangu makubwa kwa majibu ya Serikali, lakini natambua ugeni wa Mheshimiwa Naibu Waziri na nimhakikishie kwamba hayo majibu ambayo umeandaliwa yana mapungufu makubwa.
Je, utakuwa tayari kwenda field kutembelea ukajionee hali halisi iliyopo katika mradi huu kwa sababu sio kweli kwamba umekamilika?
Mheshimiwa Spika, la pili, kumekuwa na matatizo makubwa ya kukatikakatika kwa umeme na hasa kunapokuwa na dalili za mvua au mvua inaponyesha. Je, tatizo hili la kukatikakatika kwa umeme litakwisha lini katika Halmashauri ya Temeke?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi mwenyewe binafsi Jumapili nilifanya ziara ya kutembelea miradi hii na nilipita pamoja na TANESCO. Tulikuwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme (TANESCO) na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke tuliitembelea. Katika majibu yangu ya msingi nimeainisha miradi ambayo haijakamilika na mradi ambao haujakamilika ulikuwa Masista Magogo Na. 2 na Na. 3 ambao utakamilika Disemba 2017.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba miradi hiyo kwa kweli nimeiona lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwamba wakati miradi inakuwa designed scope yake na tunatambua maeneo ya Mbagala na Wilaya ya Temeke na Kigamboni ujenzi wa makazi unaongezeka kwa kasi, kuna maeneo yameongezeka wananchi wengi wamejenga. Kwa hiyo, scope ile imewaacha nje kwa hiyo unaona kwamba mahitaji yameongezeka kuliko ambavyo scope ilizingatiwa. Kwa hiyo, nimthibitishie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza tatizo la kukatikakatika kwa umeme kwa Wilaya ya Temeke litaisha lini. Ni kweli kuna tatizo la kukatikakatika kwa umeme maeneo ya Temeke, Mbagala, Yombo Dovya, Buza na Kigamboni. Serikali kupitia TANESCO imekuwaikitekeleza miradi mbalimbali, hata mwaka huu wa fedha imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.2.
Mheshimiwa Spika, sambaba na hilo kuna ujenzi wa miradi inayoendelea chini ya Mradi wa TEDAP (Tanzania Energy Development and Access Expansion Project). Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa msongo wa KVA 232 unaotoka Gongolamboto mpaka Mbagala na ujenzi wa kituo kikubwa cha kupoozea umeme chenye MVA 50.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia kuna ujenzi wa msongo wa umeme wa kilovoti 132 ambao unatoka Mbagala unaelekea Kigamboni, ujenzi wa msongo wa umeme unaotoka Kurasini kuelekea Kigamboni. Kwa hiyo, jitihada zote hizo na tatizo linasababishwa na kuongezeka kwa mahitaji ya umeme Mbagala na ndio maana unakatikakatika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kutokana na kazi zitakamilika Desemba 2017 na kuanzia Disemba, 2017 nakuthibitishia kwamba tatizo la kukatikakatika kwa umeme kwa Wilaya ya Temeke litakuwa limepungua na litaisha kabisa. Ahsante sana. (Makofi)