Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Primary Question

MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza:- Uandaaji wa Mashindano ya Kimataifa ya Mpira wa Miguu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) unataka Miji miwili iteuliwe kuendesha mashindano hayo:- Je, Serikali imeteua mji upi wa pili mbali na Dar es Salaam kuendeshea Mashindano ya AFCON ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya mwaka 2019 yatakayofanyika Tanzania?

Supplementary Question 1

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nina nyongeza ndogo. Kwanza kabisa kwa kifupi sana na mimi nimpongeze sana dada yangu Juliana na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona vijana wanaweza kumsaidia. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa je, Serikali ipo tayari kuweza kuitumia Miji aidha Mji wa Dodoma au Singida kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, inajulikana kabisa kwamba Singida sasa hivi tayari tuna kiwanja cha kisasa kabisa cha Namfua ambacho kimeshafanyiwa miundombinu ya kisasa na Singida tunaendelea tuna hoteli za kisasa ambazo zimejengwa na wazalendo.
Mheshimiwa Spika, Dodoma pia tunaona Serikali yetu imehamia hapa na Mheshimiwa Rais anakuja hapa, Waziri Mkuu tayari tunae hapa na Makamu wa Rais anakuja. Sasa kwa nini Serikali isiamue tu kwa makusudi kuchagua mikoa hii miwili kati ya Singida au Dodoma kufanyika mashindano ya AFCON 2019? (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuweza kuwapongeza Wabunge wote wa Mkoa wa Singida kwa jitihada zao nzuri ambazo wamezifanya katika kurekebisha Uwanja wa Namfua. Nichukue nafasi hii kuomba Wabunge wote lakini vilevile mikoa yote ya Tanzania kuweza kuiga mfano huu mzuri ambao umeoneshwa na Wabunge wa Singida lakini vilevile wananchi wa Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikienda sasa kwenye swali lake la msingi ambapo amependekeza kwamba nini Uwanja wa Namfua, Singida usitumike katika mashindano haya. Niseme kwamba moja ya vigezo ambavyo huwa vinazingatiwa katika kuchagua haya maeneo. Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba huo mji ambao unapendekezwa uweze kuwa na viwanja ambavyo vinakidhi ubora wa Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kigezo cha pili ni lazima kwamba mji huo uweze kuwa na hoteli ambazo zitaweza ku- accommodate wageni wote ambao watakuja katika mashindano hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, Mheshimiwa Kingu kwamba sasa hivi kuna Kamati ambayo imeundwa na Mwenyekiti wa hiyo Kamati ni Waziri wangu Dkt. Mwakyembe.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba nimtoe hofu mimi kama Naibu Waziri nitamshauri Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe sasa aangalie namna gani kwamba ile Kamati ambayo imeundwa ifike Singida ili kuweza kukagua ile miundombinu ya michezo ambayo ipo katika Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ametaka kujua kwamba kwa nini Dodoma isitumike katika mashindano haya. Kwanza napenda nichukue nafasi hii kuweza kumpongeza sana kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa sababu kwa jitihada zake yeye binafsi sasa hivi Dodoma tunajengewa uwanja mkubwa kabisa wa Kimataifa wa michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba hii inaonesha kabisa kwamba Rais wetu ni Rais ambaye ana ushawishi mkubwa sana kwa Mataifa ya nje lakini inadhihirisha kwamba Rais wetu ni mwanadiplomasia na ni Rais ambaye anapenda michezo ndio maana ameweza kumshawishi Mfalme wa Morocco kuja kutujengea kiwanja hapa katika Mkoa wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba wazo lake ni zuri na niseme sisi kama Wizara tunachukua hilo wazo lakini kama ambavyo nimesema awali, kwamba uwanja huo unajengwa kwa msaada wa Mfalme wa Morroco. Kwa hiyo, sisi kama nchi hatuwezi kumpa deadline kwamba uwanja huo ukamilike ndani ya muda gani.
Mheshimiwa Spika, tunachokifanya na nimwombe kabisa Mheshimiwa Kingu kwamba endapo uwanja huo utakamilika kabla ya hayo mashindano kufanyika mwaka 2019, basi tutaangalia ni namna gani ambavyo uwanja huo unaweza kutumika katika mashindano hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)