Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Primary Question
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa katika Halmashauri ya Momba?
Supplementary Question 1
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya kuridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza, miradi ya umeme ya REA III imezinduliwa karibu nchi nzima katika kila Mkoa, lakini utekelezaji wake mpaka sasa hivi haupo, isipokuwa ipo katika mipango kama hivi ambavyo inaonesha. Nini ambacho kinasababisha au kimesababisha kucheleweshwa kwa miradi ya REA III kuanza kukamilika tofauti na iliyopo katika maandishi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba pamoja na majibu yake, Miradi ya REA tuliiwekea zuwio la fedha, yaani tuli-ring fence fedha zake ambazo zilitakiwa zisiguswe, lakini mpaka sasa hivi miradi hii haitekelezeki kwa sababu hizi fedha hazieleweki mahali ziliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu nataka niulize je, hizi fedha ambazo tumezi-ring fence kwa ajili ya utekelezaji wa hii miradi, kwa nini hazitumiki kutekeleza mradi ikizingatiwa kuna fedha ambazo tunakata katika mafuta shilingi 50 kwenye kila lita ya mafuta? Kwa nini zinashindwa kutumika kwa ajili ya kumalizia hii miradi? Ahsante. (Makofi)
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi hii ya umeme vijijini ilizinduliwa mwezi wa Sita mwaka 2017. Naomba nimhabarishe Mheshimiwa Mbunge kwamba wakandarasi wote ambao waliteuliwa takribani 27 tulikutana nao tarehe 13 Januari, 2018 hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa miradi una kazi mbalimbali. Kwanza, walikuwa wana-survey na mnakumbuka Waheshimiwa Wabunge wengi mlileta mapendekezo, maombi ya vijiji mbalimbali, kwa hiyo, lazima survey ifanyike.
Pili, baada ya survey lazima kuwe na michoro, lakini nimthibitishie kwa Mkoa wake wa Songwe na Wilaya yake ya Momba, mkandarasi wake ameshaagiza vifaa na kesho tarehe 31 Januari na tarehe 01 TANESCO wanaenda Mkoa wa Arusha kuangalia zile transfoma. Kwa hiyo, ni wazi kwamba miradi hii inatekelezeka, lakini zipo hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee kwa kusema pia, vipo vijiji ambavyo vimeshawashwa umeme REA hii ya III. Kwa hiyo, inategemea Mkandarasi na huo muda. Kwa mfano, Geita kuna vijiji vimewaka; Mwanza Halmashauri ya Bumbuli pia umeme umewaka REA hii ya III. Kwa hiyo, miradi inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili alikuwa anasema kwamba, vipi kuhusu pesa zake za miradi hii ya umeme vijijini? Ni kweli nalishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Bunge hili iliwekwa tozo maalum kwenye mafuta na mfuko huo kweli umelindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niishukuru Wizara ya Fedha kwamba pesa zimekusanywa, zimewasilishwa na mpaka sasa tumeshapata shilingi bilioni 170.
Kwa hiyo, pesa kwenye miradi hii siyo tatizo. Tatizo ambalo lipo, changamoto tuliyokuwa tunaiona ni hawa wakandarasi kujipanga kwa mujibu wa wakati na ratiba wanavyozipanga. Ndiyo maana baada ya kuona hilo tatizo, tumekutana nao hapa Dodoma na tumewapa maelekezo kwamba mwisho tarehe 28 Februari, wakandarasi wote waanze kazi. Siyo kazi ya survey, kazi ya kuweka nguzo na miundombinu mingine ili miradi itekelezeke.
Mheshimiwa naibu Spika, nilithibitishie Bunge lako, miradi hii muda wake, hii awamu ya kwanza hii ni kipindi hiki mpaka Aprili, 2019.
Kwa hiyo, niwatoe hofu. Kwa kuwa pia tumeweka usimamizi mzuri, kila mkoa tumemtaka engineer mmoja asimamie, kila Wilaya kuwe na engineer mmoja kwa ajili ya miradi ya REA tu. Kwa hiyo, ninaamini, hata kasoro ambazo zilijitokeza kwa miradi ya REA awamu nyingine, kwa Awamu hii ya III itaenda vizuri na itakamilika kwa wakati. (Makofi)
Name
Joram Ismael Hongoli
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Primary Question
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa katika Halmashauri ya Momba?
Supplementary Question 2
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina vijiji 12 tu ambavyo vimepata umeme wa REA, lakini vijiji 22 bado havijaingizwa kwenye mpango huu wa REA III. Naomba kujua ni lini sasa Serikali itaingiza hivi vijiji 22 vyote ili waweze kupata umeme wa REA? Ahsante sana.
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Hongoli kwamba vijiji vyake 22 vilivyosalia vyote vitaingizwa kwa Awamu ya Tatu round ya pili ambavyo vinahusika vijiji 4,314. Kama ambavyo nimejielekeza tangu mwanzo, lengo la Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha vijiji vilivyosalia 7,873 vyote vinafikiwa na miundombinu ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu hii tumeanza na vijiji 3,559 vinasalia vijiji 4.314. Kwa hiyo, ndani yake kuna vijiji 22,000 vya Jimbo lake la Njombe. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania wote, Serikali ya Awamu ya Tano inaenda kufanya mapinduzi ya nishati vijiji vyote. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved