Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. JOSHUA S. NASSARI) aliuliza:- Shamba Na.112 (Ex-Arusha Coffee Estate) lililopo Nduruma Wilaya ya Meru lililokuwa likimilikiwa na Tanzania Flowers Ltd. lenye ukubwa wa ekari 721 lilishawahi kufutwa mwaka 2000 na hati ya utwaaji ardhi (Deed of Acquisition) ikasajiliwa 12/6/2001 na aliyekuwa Waziri wa Ardhi wa wakati huo, Mheshimiwa Gideon Cheyo lakini hadi leo wawekezaji hao bado wanazidi kuiuza ardhi hiyo ambayo ilifutwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi wenye shida ya ardhi:- Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya jambo hilo hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ilishawahi kuwaambia wananchi wa maeneo hayo kuwa shamba hilo halimilikiwi na wawekezaji tena?

Supplementary Question 1

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa Wilaya ya Arumeru Mashariki kwa kiasi kikubwa ardhi yake inamilikiwa na wawekezaji na ni ukweli mara nyingi kumetokea migogoro kutokana na wananchi kuwa na mahitaji makubwa ya ardhi, na kwa kuwa mpaka sasa mnasema ni ekari 80 tu imerudi katika Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru, je, Serikali haioni sasa uko umuhimu wa kupitia mashamba hayo na kufanya tathmini upya ili wananchi hawa ambao wanahitaji ardhi waweze kupata ardhi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa mzima wa Arusha maeneo mengi pia ardhi yao imemilikiwa na wawekezaji ikiwemo Wilaya ya Karatu ninayotoka na kumekuwa na mgogoro mkubwa sana wa wananchi kuhitaji ardhi kwa sababu ardhi nyingi imemilikiwa na wawekezaji mfano Shamba la Tembo Tembo liloko Karatu. Je, Serikali sasa iko tayari kufika Wilaya ya Karatu na kufanya tathmini ya kuwatambua wawekezaji ili wananchi waweze kupata ardhi yao?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ametaka kujua Serikali ina mpango gani katika kuyatambua mashamba yote haya na kufanya tathmini ili yaweze kugawiwa kwa wananchi. Naomba niseme kwamba mpaka sasa Waziri alishapeleka barua katika Mikoa yote ikiwataka kwanza wao wayatambue kwa sababu wanayafahamu, lakini mpaka sasa Wizara yangu imeshabaini mashamba 22 katika Mkoa wa Arusha ambayo tayari yameshabatilishwa kwa minajili ya kuja kuwagawia wananchi wenye shida ya maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anazungumzia habari ya mgogoro na uhitaji wa ardhi katika eneo la Karatu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi mwenyewe nilifika Karatu na migogoro hiyo niliambiwa na wakati huo nilikuwa nashughulikia masuala ya Mabaraza ya Ardhi. Hata hivyo, kwa sababu Wizara imeweka mpango mzuri kwa ajili ya kuweza kuyafikia maeneo yote kwa wakati, tunajaribu kukusanya migogoro yote na ndiyo maana tuliomba tuweze kuipata na tuko tayari kurudi tena Karatu kwa ajili ya kutatua mgogoro huo ambao anauzungumzia. Kabla ya Bajeti ya Wizara kuisha, Wabunge wote watakuwa wamegawiwa vitabu na wataweza kubaini migogoro ambayo tumeiainisha ambayo tunatarajia kuanza kuitembelea baada ya Bunge hili kumalizika. Kwa sababu migogoro ya ardhi ni suala mtambuka na Wizara zingine zitahusika. Kwa hiyo, kila Mbunge ataona katika Mkoa au Wilaya yake ni migogoro ipi ambayo Wizara imeiainisha kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi.