Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka mradi wa TASAF awamu ya III katika vijiji ambavyo havijapata mradi katika Jimbo la Kaliua?

Supplementary Question 1

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kumuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza Halmashauri ya Kaliua hatujafikiwa kuwa asilimia 70 tumefikiwa kwa asilimia 50 tu; kati ya vijiji 102 ni vijiji 54 tu. Katika vijiji ambavyo vilipata miradi kuna baadhi ya makosa ambayo yalifanyika katika kuanisha wale ambao walikuwa ni walengwa na baada ya kulalamika wakaambiwa waandike rufaa kwa sababu kuna wazee ambao wanastahili kupata mradi hawakupewa mradi wakaenda kupewa watu ambao wana uwezo. Leo ni mwaka wa pili waliambiwa waandike rufaa na mpaka leo rufaa haijarudi wala majina yao hayajaingizwa kwenye mradi, jambo ambalo limeleta manunguniko makubwa na masikitiko kwa sababu wanashindwa kuishi lakini wenzao ambao wana hali nzuri wanaendela kupata mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba zile rufaa ambazo ziliandikwa na walengwa zinarudi ili waingizwe kwenye mradi waendelee kunufaika na mradi huu wa kunusuru kaya maskini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili mradi huu umeanza mwaka 2013, lakini kwa baadhi ya wilaya ikiwemo Kaliua tumeanza mwaka 2015, Januari. Naomba kuuliza Serikali kwa zile wilaya ambazo zilichelewa kupata mradi kwa miaka miwili, je, wataendeleza mradi kwa miaka 10 kama ilivyo kawaida au wataenda kufanya evaluation kama wanavyokwenda nchi nzima na kusahau kwamba sasa hivi mradi ni mwaka wa tatu wakati wengine ni mwaka wa tano? (Makofi)

Name

Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Sakaya kwa jinsi anavyofuatilia kunusuru kaya maskini katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza kwamba kwake tumefikia asilimia 50 sio 70 kama katika maeneo mengine mimi kama Waziri ninayesimamia masuala ya TASAF nitafuatilia nione nini kimesababisha wao wawe chini kulingana na wilaya nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, anasema makosa yalifanyika katika kuwabaini walengwa na naomba nichukue nafasi kulieleza Bunge lako Tukufu, Watendaji wa TASAF hawana kauli juu ya nani asaidiwe. Wenye kauli juu ya nani asaidiwe ni watu katika mtaa, shehia, wao ndio wanaokaa wanasema hapa kijijini fulani bin fulani hali yake si nzuri. Kwa hiyo kwa yale maeneo ambayo makosa haya yamefanyika ni makosa ya wanavijiji na hasa viongozi wa vijiji kule Kaliua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo mmetuletea watu ambao hawakuhusika wamelipishwa fedha. Juzi nilikuwa Singida vijijini, watu walilipishwa milioni tatu laki tisa ambao hawahusiki, wamesharudisha milioni tatu bado laki tisa; na kila mahali wanarudisha. Katika maeneo mengine tumewawajibisha watendaji wa TASAF ambao walishiriki katika udanganyifu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zile wilaya ambazo zilichelewa nalo siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja hapa, nitalifanyia utafiti nijue walichelewa kwa sababu gani na nitachukua hatua stahiki.

Name

Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka mradi wa TASAF awamu ya III katika vijiji ambavyo havijapata mradi katika Jimbo la Kaliua?

Supplementary Question 2

MHE. ZITO Z. KABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mchakato wa bajeti mpya ya Serikali ya Mwaka 2018/2019 unaendelea, kumekuwa na taarifa kwamba Serikali sasa inajiondoa katika mfumo wa conditional cash transfer, yaani kwenda kuwapa fedha wananchi na inaanzisha mfumo tofauti. Baadhi ya mikataba ambayo Wizara ya Fedha ilikuwa iingie na baadhi ya nchi wafadhili ikiwemo Benki ya Dunia, Wizara ya Fedha imesitisha kusaini kwa sababu Serikali haitaki tena kuendelea kutoa hizi conditional cash transfer. Tunaomba taarifa rasmi ya Serikali ndani ya Bunge kuhusiana na jambo hili.

Name

CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Waziri mwenye dhamana ya TASAF sina taarifa ya Serikali sasa hivi kujiondoa katika kuwapelekea hizi fedha. Taarifa nilizonazo ni kwamba sasa hivi tunafanya utafiti wa hizi fedha. Badala ya watu kwenda kupanga foleni pale wilayani kila siku tunaangalia uwezekano wa kupekea fedha zao kwa njia ya simu ili kuwaondolea usumbufu wa kwenda wilayani. Hilo ambalo anasema Mheshimiwa Zitto Kabwe kama analisema liko njiani, lakini halijafika mezani kwa Waziri mwenye dhamana ya TASAF. (Makofi)

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka mradi wa TASAF awamu ya III katika vijiji ambavyo havijapata mradi katika Jimbo la Kaliua?

Supplementary Question 3

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuandaa mpango huu wa kunusuru kaya maskini. Katika jimbo langu Mheshimiwa Waziri alishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri, kwa sababu anajua Bonde la Yaeda Chini kwa Hadzabe kule wana tatizo hili la umaskini. Je, ataweza kutuongezea angalau Vijiji vile Mungwamono, Eshkeshi na Endagechani tukapata zaidi msaada huu wa TASAF?

Name

Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nakubali kwamba nilikuwa DC wa Mbulu 1983 mpaka 1988 na maeneo anayoyataja ya Yaeda Chini nimefika, wanakaa Wahadzabe, wanaishi kwa kuwinda tu badala ya kulima. Nataka nimwahidi kwamba kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge, wanachotakiwa wao ni kuzitambua zile kaya maskini, wakituletea sisi tutachukua hatua. Nilipita siku nyingi kule Yaeda Chini, Mheshimiwa Mbunge akinialika kwenda kuwahamasisha, nitashirikiana naye.