Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Primary Question

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Mkoa wa Katavi?

Supplementary Question 1

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa kazi nzuri na juhudi zinazoendelea kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunashukuru kweli tunajengewa Mahakama ya Mkoa pamoja na Wilaya katika jengo moja. Lile jengo limejengwa vyumba vinne tu na Mahakimu wa Mkoa wanahitajika wawili na Mahakimu wa Wilaya wanahitajika wawili. Jaji akija hana ofisi ya kukaa na hakuna sehemu nyingine ya huduma mbalimbali za kiofisi.
Je, Serikali haioni kwamba hilo jengo ni la muda tu siyo la muda mrefu? Serikali haioni kama itapata hasara kujenga sasa hivi na wakati mwingine wajenge tena. Lini sasa Serikali itaongeza lilelile jengo liwe kubwa na la kutosheleza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi Mahakimu ni wachache sana, je, Serikali itaongeza lini Mahakimu ndani ya Mkoa wetu wa Katavi?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anazungumza kuhusu jengo hili kuwa na vyumba ambavyo havitoshi na kama Serikali itaingia hasara kwa sababu baadae tena itahitajika kujenga jengo lingine. Nianze kwa kusema jengo hili la Mahakama ya Mkoa linajengwa katika eneo moja ambalo linaitwa Ilembo, Manispaa ya Mpanda. Tumempeleka mkandarasi ambaye anaitwa Moladi Tanzania yuko pale anafanya kazi hiyo, kilichojitokeza ni kwamba baada ya mvua kubwa kunyesha na udongo wa pale Ilembo ni mfinyanzi mkandarasi na consultant wameshauriana tumebadilisha michoro tena ambayo inachorwa upya na lengo hapa ni kuhakikisha tunajenga jengo lenye ubora wa juu ili shughuli za Mahakama ziendelee katika eneo hilo la Ilembo katika Manispaa ya Mpanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hatua ya kwanza ambayo Serikali imefanya. Mheshimiwa Mbunge naomba ukubaliane kwamba ni hatua kubwa sana ya ujenzi wa vyumba hivyo ambavyo vitawaweka Mahakimu wa Mkoa pamoja na Mahakimu wa Wilaya. Yako bado maeneo mengi nchi nzima ambayo yana mahitaji ya Mahakama. Kwa hiyo, kwa kuanza pale Ilembo ni fursa ya kipekee kwa Mkoa na tushukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo msemo mmoja wanasema ndege mmoja wa mkononi ana thamani kuliko wawili wa shambani. Sasa tayari pale Mpanda wameshapata majengo haya, waishukuru Serikali ikitotokea bajeti nyingine tutaona namna ya kufanya lakini mahitaji ni makubwa sana kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, amezungumza kuhusu Mahakimu wachache, hii ni changamoto si tu katika Mkoa wa Katavi lakini katika Mikoa mingi sana ndani ya nchi yetu. Pindi pale bajeti itakaporuhusu ya kuwaajiri watumishi wengine, Mkoa wa Katavi pia na wenyewe tutauangalia ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa Mahakimu.