Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Julius Kalanga Laizer
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Primary Question
MHE. JULIUS K. LAZIER aliuliza:- Hivi karibuni Serikali ilitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa kusimamia urejeshwaji wa mashamba makubwa ambao hayakuendelea yakiwemo ya Wilaya ya Monduli. Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kufuta mashamba 25 katika Wilaya ya Monduli ambayo mchakato wake kwa ngazi ya Halmashauri umekamilika?
Supplementary Question 1
MHE. JULIUS K. LAZIER: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza swali la nyongeza naomba nikiri kwamba kwa kweli naipongeza Wizara hii kwa jitihada kubwa ambazo imefanya katika kusaidia wananchi wa Wilaya ya Monduli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla pia sijauliza swali la nyongeza, naomba nimwambie tu Waziri kwamba waliokuandalia majibu wamekudanganya. Kwanza kwa mujibu wa taarifa tu ekari zilizofutwa Monduli ni ekari 13,000 na si 131,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, mashamba tunayoyazungumzia ni mashamba ambayo Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alivyokuja katika Jimbo la Monduli mwaka 2016 mwezi Machi, alizuiliwa na wananchi njiani na akatoa maelekezo kwamba Halmashauri ifanye mchakato wa mashamba yale ambayo yalikuwa na mashamba pori na wananchi wale walikuwa wanasumbuliwa na wale ambao waliyatelekeza mashamba na kuchukua mikopo kwa hati ya mashamba yale. Waziri akatoa maelekezo ambayo ndiyo ambayo mchakato wake ukafanyika na tarehe 09 Januari, 2018 tuka-submit taarifa ya Wilaya kwa kamishina wa ardhi wa kanda ambae taarifa yake haionekani hapa, kwa hiyo mchakato wa Halmashauri tulishamaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri, nataka nijue tu kwamba, kwa kuwa jambo hili Waziri wa Ardhi alishatoa maelekezo na kwa kuwa Halmashauri ilishafanya mchakato wa kuyafuta mashamba haya 25, je, ni lini Serikali itamalizia huu mchakato wa ufutaji wa mashamba hayo 25 ambayo tumeanza mchakato upya kama ulivyoeleza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Waziri alitoa pia maelekezo kwamba mapendekezo ya matumizi ya mashamba yale 13 yaletwe na kwa kuwa Halmashauri na wananchi tumeshamaliza mchakato wa kutenga maeneo kwa ajili yauwekezaji, maeneo ya akiba ya ardhi na maeneo mengine ya wananchi na kwa kuwa huu ni msimu wa kilimo na mchakato huo bado haujakamilika japo Halmashauri imeshakamilisha na taarifa yote iko Kanda; ni lini Serikali itaagiza Mkoa na Kanda walete mapendekezo ya wananchi ya matumizi ya mashamba hayo 13? Nakushukuru.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua ni lini mchakato utakamilika. Mchakato wa kukamilika unategemea na wao wenyewe kwa sababu si kazi ya Wizara kufuatilia na kuweza kujua ni jinsi gani mchakato unakwenda mbele; kwa hiyo wao wameshaona hawajaendelezwa na sheria zipo. Ibara ya 45 mpaka ya 47 kuna maonyo ambayo yanaweza kutolewa kwa muhusika kama hajaendeleza; na Ibara ya 48 unabatilisha kwa maana ya kumpelekea ilani kwa ajili ya ubatilisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wao wenyewe ndiyo wanatakiwa wakamilishe na wakileta kwa Waziri haina tatizo. Kwa hiyo si jukumu la Wizara kuona ni lini itakamilishwa ni mchakato ambao unatakiwa umalizwe na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anauliza kwamba ni lini Wizara itaagiza Mkoa ili waweze kutimiza. Kila Mkoa unataratibu zake katika mipango yake, kwa hiyo kama mlileta maombi mahitaji ambayo mnataka kutumia yale maeneo ni jukumu lenu pia kuona kwamba maeneo hayo yanatakiwa yafanyiwe kazi ile iliyokusudiwa. Kwa sababu unapoleta kubatilisha tayari umeshaona kuna hitaji na tayari una mpango.
Mhe shimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimesema kwamba hawajaleta mpango wowote kwa hiyo sisi hatuwezi kuwasukuma mfanye nini pengine hamjahitaji kwa maana hiyo. Kwa hiyo, ni jukumu la Mkoa kuhakikisha taratibu zote zinakamilika na Wizara inaweza ukafanya pale ambapo itakuwa imeletewa ofisini.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mweyekiti, nampongeza sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anasema kazi zote ziko kwenye kanda na watumishi wa kanda ni wa Wizara sisi tutafuatilia kule kwenye kanda tuone yale yaliyokwama yaje haraka Wizarani ili niweze kuyaona. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved