Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Omary Tebweta Mgumba
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini Mashariki
Primary Question
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:- Kata sita za Tegetelo, Kibuko, Tomondo, Tununguo, Seregete, Matuli na Mkulazi katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hazijafikiwa na miundombinu ya umeme mpaka sasa. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata hizo?
Supplementary Question 1
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tulipata vijiji 17 kati ya vijiji 64 katika miradi ya umeme ya REA Awamu ya Kwanza na REA Awamu ya Pili, na kwa kuwa katika awamu zote hizo utekelezaji wake wa miradi hiyo kuna taasisi za umma kama vile shule, zahanati, vituo vya afya na nyumba za ibada na vijiji na vitongoji vingi kwa mfano, Kijiji cha Tomondwe, Mfumbwe, vitongoji vya Misala vilirukwa.
Je, Serikali huu mradi wa densification utafika lini Morogoro hususan katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ili vijiji na vitongoji hivi vilivyorukwa vipatiwe umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na majibu hayo nataka niweke kumbukumbu sawa. Swali kama hili niliuliza katika Bunge lililopita katika swali la nyongeza na swali la msingi Bunge lingine lililopita. Serikali ilinipa majibu katika jimbo langu wamenipa vijiji 20 na si 14; mpaka sasa hivi huyo mkandarasi ameshafika na amefanya survey ya vijiji vyote 20. Hata hivyo kwa kuwa amefanya vijiji saba amepata mkataba wa kufanya survey pamoja na kujenga miundombinu ya umeme. Lakini vijiji 13 ameambiwa tu afanye survey ukizingatia ndani ya vijiji hivyo ndiko kunakojengwa kiwanda kikubwa cha sukari ambacho kitaanza ujenzi mwaka huu pamoja na Bwawa la Kidunda.
Je, Serikali imejipanga vipi ili kumalizia na ujenzi katika vijiji hivi 13 na vijiji vile vingine vya Tomondo na sehemu zingine? (Makofi)
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Mgumba amejielekeza kwenye utekelezaji wa miradi ya REA Awamu ya Kwanza na REA Awamu ya Pili ambako yako maeneo mbalimbali yalirukwa.
Napenda nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo ambayo yalirukwa katika awamu ya kwanza na ya pili Serikali yetu imekuja na mpango wa densification, kwa maana ya ujazilizi katika maeneo ambayo taasisi za umma, vijiji na kaya mbalimbali. Kwa kuwa densification imetekelezwa katika mikoa nane ya awali kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge lako Tukufu, awamu inayofuata sasa Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini imeajiri mshauri elekezi ambaye ni Multconsult ASA kutoka Norway pamoja na NORPLAN ya Tanzania kwa ajili ya kufanya verification ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia kupitia Wakala wa Umeme Vijijini imeomba ufadhili kutoka Norway, Sweden na Ufaransa kwa ajili ya densification ya awamu ya pili. Nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba maeneo mbalimbali na mikoa mbalimbali yataanza kufikiwa na densification ya awamu ya pili ikiwemo Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mheshimiwa Mgumba amejielekeza kwenye maeneo yale ambayo kama ambavyo amerejea jibu letu Bungeni la Mkutano wa Tisa kwamba katika vijiji vyake 20, vijiji saba vimefanyiwa survey na hivyo 13. Kama tunavyotambua jimbo hilo miradi mikubwa ya kimkakati inatekelezwa ikiwemo ujenzi wa Kiwanda cha Sukari pia na ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge nia yetu sisi kama Wizara ya Nishati ni kuwezesha sekta zingine. Kwa hiyo ni wazi kabisa kwamba vile vijiji 13 ambavyo vipo katika maeneo ambayo miradi mikubwa inapita tumemuelekeza mkandarasi ambaye ni State Grid maeneo yote ambayo amefanya upembuzi yakinifu amalizie kuendelea na ujenzi wa miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimtoe hofu Mheshimiwa Mgumba kwamba maeneo yote ambayo ameyataja, hivyo vijiji 20 lakini pia kwa kutambua umuhimu wa maeneo hayo pia tumemuongezea vijiji nane vikiwemo vijiji viwili katika Kata ya Mkulazi ambako mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unafanyika na Bwawa la Kidunda. Pamoja na kwamba maagizo ya Serikali pia yameelekeza kwamba maeneo ambayo kuna miundombinu mikubwa ya umeme iliyopita katika kata yake mojawapo ambayo ameitaja Tomondo pia tumempa vijiji vinne kwa sababu iko karibu na Kata ya Kiloka na Mikese ambako kuna miundombinu ya umeme. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara inafanya kazi pamoja naye. Ahsante sana.
Name
Justin Joseph Monko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Primary Question
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:- Kata sita za Tegetelo, Kibuko, Tomondo, Tununguo, Seregete, Matuli na Mkulazi katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hazijafikiwa na miundombinu ya umeme mpaka sasa. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata hizo?
Supplementary Question 2
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii, na niwashukuru sana wana-CCM na Chama changu cha Mapinduzi na hasa wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa kuniwezesha kuwa mwakilishi wao hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yaliyozungumwa katika Jimbo la Morogoro Kusini yanafanana sana na Jimbo la Singida Kaskazini. Jimbo la Singida Kaskazini wakati unaongelea usambazaji wa umeme REA Awamu ya Tatu tulipata Mradi wa REA Awamu ya Pili katika vijiji vya Mrama, Makhandi, Mitula, Merya, Mipilo, Magojoha, Msange, Madasenga, Njia Panda, Mohamo, Mwamba na Mgori. Hata hivyo, mwaka 2016 mwishoni mkandarasi huyo alifilisika wa SPENCON na kazi hiyo ilisimama tangu mwaka 2016 na hadi sasa mradi huo haujaendelea mpaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri atuambie Serikali inatueleza ni lini mkandarasi mwingine atapatikana kwa sababu mkandarasi huyu aliyekuwepo tunaambiwa hawezi kuomba tena kazi hiyo ya kuendeleza shughuli hiyo ya REA Awamu ya Pili, atapatikana mkandarasi mwingine na kumalizia shughuli hiyo ili wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini waendelee nao kunufaika na nishati ya umeme? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali hili la nyongeza la Mheshimiwa Monko. Na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Monko kwa kuaminiwa na wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge, na tumeweza kuwapa pole wananchi wa Mikoa ya Singida na Kilimanjaro baada ya kutokea matatizo ambayo hayakutarajiwa ya mkandarasi SPENCON ambaye kwa kweli alifanya kazi kama asilima 65 na akashindwa kumalizia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyopata kusema pia, Serikali kwa kuliona hilo ikachukua hatua stahiki kupitia Wakala wa Umeme Vijijini na kuanza harakati za kutafuta mkandarasi mpya kwa ajili ya kumalizia kazi zilizosalia katika Jimbo la Singida Kaskazini pamoja na majimbo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mchakato huu ambao umefanyika na Wakala wa Umeme Vijijini tumefanikiwa kumpata mkandarasi katika Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ameshaanza kazi na mimi nimejiridhisha, nilienda nikamuona, lakini katika Mkoa wa Singida mchakato unaendelea kwa sasa kwa wakandarasi wale watarajiwa kuwasilisha performance bond na baada ya hapo mkataba wa awali ambao wameuwasilisha kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mapitio na tunatarajia mwezi Machi mwaka huu kazi zianze.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, na baada ya kikao hiki cha Bunge lako tukufu naomba tuonane naye kwa ajili ya kumweleza kazi zitakazofanyika na vijiji ambavyo vitafikiwa ili aweze kuwaambia wananchi wake. Nakushukuru. (Makofi)