Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Raisa Abdalla Mussa
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA aliuliza:- Wapo wanawake ambao wamefungwa kwenye magerezani wakiwa na watoto wachanga/wadogo ambao bado wanahitaji uangalizi au huduma za mama zao. (a) Je, Serikali imejipanga vipi katika kuwanusuru watoto hao ambao hawana hatia? (b) Je, Serikali haioni kuwa inavunja haki za binadamu kwa kuwaweka gerezani watoto hao wasio na makosa? (c) Je, Serikali inaweza kulipa Bunge takwimu za wanawake waliokinzana na sheria na wamefungwa kwa miaka mitano iliyopita?
Supplementary Question 1
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida wafungwa wanawake au kisheria wanatakiwa walindwe au wasimamiwe na askari magereza wanawake na tunaamini kwamba magereza wale ambao wamefungwa kule wako katika mikono salama. Inakuwaje akina mama wale wanapata ujauzito wakiwa katika magereza? (Makofi)
Swali la pili ni kwamba, je, Waziri haoni kwamba iko haja ya akina mama hawa kupewa vifungo vya nje ili kutoa haki kwa watoto wale wasiwemo ndani ya magereza kama walivyo mama zao? Ahsante.
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mujibu wa utaratibu na ndivyo hali ilivyo kwamba wafungwa wanawake wanasimamiwa na askari magereza wa kike. Sasa hoja kwamba wafungwa wale wanapata mimba wakiwa gerezani hiyo inahitaji uthibitisho, kwa sababu katika hali ya kawaida huwezi kujua mimba ile ameipata vipi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kimsingi mazingira hayaruhusu hali hiyo kutokea katika Magereza. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba inawezekana pengine waliingia pale hali ya kuwa walikuwa na mimba changa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na vifungo vya nje kwa akina mama hawa. Tunao utaratibu ambao haubagui jinsia ya kuweza kuwapatia vifungo vya nje kwa mujibu wa taratibu. Tuna utaratibu wa huduma za jamii, tuna utaratibu vilevile wa msamaha na wanawake wanafaidika katika taratibu zote mbili. Kwa hiyo, utaratibu huo upo lakini inategemea na makosa. Kwa wanawake ambao makosa yao hayakidhi vigezo vya kuweza kupata fursa hiyo wataendelea kutumikia vifungo vyao kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Waheshimiwa Wabunge wamesimama wengi sana.
Waheshimiwa Wabunge, nimezunguka takriban Magereza ya Mikoa yote na katika zunguka ile hakuna eneo hata moja ambako nimefika nikaelezewa kwamba mama ama mwanamke aliyekuwa amefungwa kifungo cha muda mrefu amegundulika amepata mtoto akiwa katika kifungo cha muda mrefu. Ni kweli unaweza ukakuta wale waliokuwa wana vifungo vya muda mfupi wakajifungua wakiwa gerezani, lakini kujifungua wakiwa gerezani haina maana kwamba mimba kaipatia gerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge niwaambie tu vyombo vyetu hivi ni vyombo vinavyofanya kazi kwa sheria kali sana. Haingewezekana mwanamke apatie mimba ndani halafu ijifiche isijulikane kwamba kapatia mimba pale. Kwa hiyo, hatua zingeshachukuliwa na wale watu ni wachukuaji wa hatua kweli kweli. (Makofi)
Name
Anna Joram Gidarya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA aliuliza:- Wapo wanawake ambao wamefungwa kwenye magerezani wakiwa na watoto wachanga/wadogo ambao bado wanahitaji uangalizi au huduma za mama zao. (a) Je, Serikali imejipanga vipi katika kuwanusuru watoto hao ambao hawana hatia? (b) Je, Serikali haioni kuwa inavunja haki za binadamu kwa kuwaweka gerezani watoto hao wasio na makosa? (c) Je, Serikali inaweza kulipa Bunge takwimu za wanawake waliokinzana na sheria na wamefungwa kwa miaka mitano iliyopita?
Supplementary Question 2
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na majibu ya Waziri na swali la msingi kumekuwa na msongamano mkubwa katika magereza ya wanawake, pia inaonekana kuna matatizo makubwa sana ya kisaikolojia kwa wale watoto wanaokulia pale gerezani kwa sababu mazingira siyo rafiki. Je, ni lini sasa Serikali itatenga kituo maalum kwa ajili ya wale wanawake wanaofungwa wakiwa na mimba na wakiwa na watoto wachanga? (Makofi)
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mazingira ya magereza ya wanawake, Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya magereza yetu kila mwaka kadri hali ya uwezo wa bajeti inavyoruhusu ikiwemo maeneo ambayo magereza ya wanawake yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amezungumza, tumekuwa tuna utaratibu wa kufanya ziara kwenye magereza haya. Naomba nikiri hapa kama kuna maeneo ambayo yana mazingira mazuri ni magereza ya wanawake kuliko wanaume.
Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuwapongeza sana akina mama inaonekana siyo tu katika hali ya maisha ya kawaida lakini hata hali ya gerezani maeneo yao yanakuwa ni maeneo ambayo yanakuwa safi na mazuri zaidi kimazingira pia Serikali inafanya jitihada kwa kutoa kipaumbele maalum katika maeneo ambayo magereza ya akina mama wenye watoto yapo.
Name
Stella Ikupa Alex
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA aliuliza:- Wapo wanawake ambao wamefungwa kwenye magerezani wakiwa na watoto wachanga/wadogo ambao bado wanahitaji uangalizi au huduma za mama zao. (a) Je, Serikali imejipanga vipi katika kuwanusuru watoto hao ambao hawana hatia? (b) Je, Serikali haioni kuwa inavunja haki za binadamu kwa kuwaweka gerezani watoto hao wasio na makosa? (c) Je, Serikali inaweza kulipa Bunge takwimu za wanawake waliokinzana na sheria na wamefungwa kwa miaka mitano iliyopita?
Supplementary Question 3
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita Mkoani Dar es Salaam lilitokea tukio la kusikitisha dhidi ya watu wenye ulemavu ambao ni waendesha bajaji ambapo walifanyiwa vitendo vya udhalilishaji pamoja na vitendo vya kinyama, walipigwa sana na baadae kuburuzwa chini. Pamoja na makosa ambayo walidaiwa kuwa nayo lakini approach ambayo ilitumika na askari wetu haikuwa nzuri kabisa. Je, nini kauli ya Serikali kwa hili? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Ikupa kwa kuleta swali hilo na yeye ni Mbunge anayewakilisha kundi hilo, kwa sababu yupo ni-apologize kwa niaba yake awafikishie salamu hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba pamoja na utaratibu kuwepo ama ukiukwaji wa utaratibu, kwa kuzingatia hali yao ni nguvu kubwa imetumika. Serikali tumeshajadiliana na wenzetu wa TAMISEMI, watakutana na Wizara ya TAMISEMI pamoja na wenzao wa ngazi ya Mkoa ili kuweka utaratibu ambao utakuwa una taswira nzuri na kufanya jambo hilo ili lisiweze kujirudia kuweka utaratibu ulio wa kudumu ili liweze kufanya utaratibu huo wa kudumu. Kwa hiyo, tumepokea concern hiyo na linafanyiwa kazi ili jambo la aina hiyo lisijirudie. (Makofi)