Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Primary Question

MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:- Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?

Supplementary Question 1

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Niulize sasa maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa msimamizi wa mradi huu aliyejenga mradi wa maji wa Kijiji cha Ngomalusambo alijenga chini ya kiwango, ikiwa ni pamoja na kufunga pampu ya kusukuma maji ambayo haina uwezo na haikuwa stahili iliyokuwa imelengwa. Je, Serikali inachukua hatua gani kwa Mkandarasi na Msimamizi aliyejenga mradi huu chini ya kiwango na kuipotezea Serikali kiasi kikubwa cha fedha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miradi mingi ya maji imekuwa na tatizo ya usimamizi mbovu kiasi kwamba miradi inayoelekezwa haitengenezwi vizuri. Mfano pale Kijiji cha Majalila kulikuwa na mradi mkubwa wa maji ambao Serikali imetoa fedha nyingi lakini ilipangiwa kujengewa vituo vya maji 28 vikajengwa 12. Je, msimamizi wa mradi huu wanachukua hatua gani ili aweze kuwajibishwa.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi wa Ngomalusambo kwamba imefungwa mashine ambayo iko chini ya kiwango siwezi kulizungumza hapa sasa, lakini kwa taarifa nilizozipata ni kwamba ule mradi ulianza lakini charging capacity yake kile kisima imekuwa kidogo, kwamba pampu inafungwa lakini ikisukuma maji sasa hivi wanasukuma takribani masaa 18 wanavyotumia diesel maana yake gharama inakuwa kubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ni taarifa ambazo nilizipata kwa wataalam wangu. Hata hivyo, concern aliyozungumza Mheshimiwa Mbunge naomba tuifanyie kazi, kwenda kufanya uchunguzi je, ni kweli kisima kimepoteza uwezo au pampu iliyofungwa haina uwezo. Maana yake mpango uliopo sasa hivi katika Halmashauri ya Mpanda ni kwenda kuchimba kingine kuhamisha ile mitambo iendelee kufanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Mbunge anasema pampu iliyofungwa haina uwezo basi hili maana yake ni jambo kubwa sana lazima tukalifanyie kazi na ikiwezekana tuunde Tume maalum kwenda kuchunguza kwamba kipi kinachojili katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika katika mradi wa Majalila na Mbunge anakumbuka siku ile tulivyofika pale tulikuta ule mradi upo idle pale katika Wilaya Tanganyika haufanyi kazi. Nikatoa maelekezo na nimepata taarifa mradi ule umeshaanza kufanya kazi, lakini inaonekana kwamba kuna changa la macho, badala ya vituo vya maji 24 vimefungwa 12 maana yake hapo kuna tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa matatizo hayo yote, kama hali ipo hivyo, Ofisi ya TAMISEMI hatuwezi kuridhika na hali hiyo. Naomba nimhakikishie tutaunda Tume maalum kutoka ofisini kwangu kwenda kufanya uchunguzi wa miradi hiyo miwili, lakini siyo hiyo miradi miwili na ile miradi mingine minne inayoendelea, kuweza kubaini kwamba ni tatizo gani linaendelea lengo kubwa tuweze kulinda fedha za Serikali na kuhakikisha wananchi wanapata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilio cha Mheshimiwa Mbunge kimesikika, tunaenda kukifanyia kazi kama tulivyofanya kazi Mkoa wa Geita na maeneo mengine.

Name

Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:- Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?

Supplementary Question 2

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Miradi ya World Bank, miradi ya maji mikubwa ya World Bank Kijiji cha Rungu, Wilaya ya Mbozi lakini pia kuna mradi mwingine Kijiji cha Ihanda tangu imezinduliwa na Mwenge miradi hii haijawahi kutoa maji. Sasa naomba niulize kwa nini miradi inazinduliwa na mwenge lakini haitoi maji?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa hoja siyo miradi ya kuzinduliwa na Mwenge haitoi maji, nafikiri hoja ya msingi ni kwa nini mradi umezinduliwa lakini hautoi maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika,i naomba niwasihi Wabunge sisi ni Wajumbe wa Kamati za Fedha, Wajumbe wa Baraza la Madiwani. Tusikubali hata siku moja, mradi ambao tunasimamia katika Kamati ya Fedha watu wanakuja kufanya kanyaboya, mradi unazinduliwa hautoi maji na wewe Mbunge upo, niseme kwamba jambo hili ni la kwetu sote. Mheshimiwa Haonga naomba niseme kwamba hili la kwetu sote hatuwezi tukakubali katika jambo hili, kama mradi huo hautoi maji na kwa vile tumekubaliana kwamba baada ya Bunge hili tunakwenda kupiga kazi ngumu Mkoa wa Songwe, tupitie huo mradi twende tukabaini kitu gani kinachoendelea hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku tulinde fedha hizi ambazo wananchi wana shida kubwa ya maji hatuwezi kukubali, sio mbio za mwenge peke yake isipokuwa kiongozi yoyote au mradi wowote unaozinduliwa ni lazima ufanye kazi kama unavyokusudiwa. Kwa hiyo, naomba nimsihi nikifika pale, hata kama ratiba yangu haijawekwa huko naomba aniambie kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri ule mradi uko hapa, lazima tufike hapo site twende kuangalia nini kinaendelea.

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:- Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?

Supplementary Question 3

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Katika Wilaya ya Mpwapwa, Vijiji vya Bumila, Mima na Iyoma vilichimbwa visima vya maji na maji yalipatikana, sasa ni miezi nane hakuna cha bomba, hakuna cha pampu. Sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri vile visima vilichimbwa kwa ajili ya mapambo kuonyesha wananchi tu au ni lini wataweka pampu na mabomba wananchi wanapata tabu?

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulishazungumza naye na nimeshazungumza ndani ya Bunge lako hili Tukufu, ukishachimba kisima maji yakapatikana Mkurugenzi unatakiwa utengeneze quotation ya kununua pampu. Ukishatuletea quotation sisi hiyo tunaiweka kama ni certificate tunakupa hela ili uende ukanunue pampu na pampu hizi zifungwe wananchi wapate maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kama tulivyoongea nje kwamba amwambie Mkurugenzi wake wa Halmashauri atengeneze quotation na kama hana huo utaalam basi tuwasiliane ili Wizara ya Maji na Umwagiliaji, tutume mtaalam wetu akamsaidie Mkurugenzi wake wananchi wapate maji.

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:- Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?

Supplementary Question 4

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Ngomalusambo Wilayani Mpanda la mradi wa maji kukamilika lakini hautoi maji halina tofauti na mradi wa maji uliopo Wilayani Tunduru Kijiji cha Nandembo. Mradi ule ulitumia mamilioni mengi ya shilingi lakini mpaka hivi tunavyozungumza wananchi wale hawapati maji. Napenda kujua ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha sasa huduma hiyo inapatikana ipasavyo? Ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuna sababu inawezekana mradi mwingine kwa mfano juzi juzi nilikuwa na ndugu yangu Kibajaji hapa katika Kijiji chake cha Manzase mradi umekamilika lakini tatizo kubwa lilikuwa ni suala zima la power, kwamba nishati ya aina gani iweze kutumika, kwa hiyo case by case hii miradi haitoi maji kwa sababu maalum. Inawezekana sehemu nyingine pampu hazijakamilika, hazijanunuliwa au mradi haufanyi kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa case ya Mheshimiwa Mbunge, sifahamu mradi huo ukoje. Jambo ninalotaka kulifanya tukitoka hapa naomba anipe takwimu halisi ni kitu gani kinachoendelea pale tutoe maelekezo ya stahili nini kinachotakiwa kufanyika, kwa sababu najua miradi hii inakwama katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo Mheshimiwa Sikudhani naomba anijulishe baadaye kuna kitu gani pale kinachoendelea, tutoe maagizo mahsusi katika suala zima la mradi tuweze kuwasaidia wananchi wake waweze kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nilimwona Mheshimiwa Musukuma hapa akisimama kwa ajili ya mradi wake wa Changorongo, naamini alitaka kusimama kwa hoja hiyo. Mheshimiwa Msukuma kwa sababu tumekubaliana hapa miongoni mwa jambo tunalotaka kwenda kulifanya baada ya Bunge kutembelea ile shule ya msingi tutafika hapo kwa ajili ya kujibu lile swali kwa ajili ya wananchi wa Geita pale ambao muda mrefu tumewapigia kazi waweze kupata huduma inayostahili.

Name

Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Primary Question

MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:- Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?

Supplementary Question 5

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri sasa naomba niulize swali moja. Kwa kuwa, miradi ya maji imekuwa ikisumbua sehemu nyingi hata Wilaya ya Kilolo imekuwa haiishi vizuri na kwa kuwa kuna watu wanaitwa Wakandarasi Washauri wamekuwa wakilipwa pesa kwa ajiili ya kushauri miradi yetu ili iende vizuri pale inapokuwa imeharibika wanachukuliwa hatua gani hawa Wakandarasi Washauri?

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba huyu Mkandarasi Mshauri au Consultant kwenye usajili wake akipata kazi yoyote ya Serikali kuna kitu kinaitwa Design Liability Insurance. Insurance hiyo inalinda performance ya kazi yake na kama hakufanya vizuri kupitia kwenye ile insurance au kupitia kwenye ile bond basi anatakiwa arudishe hela kama mradi haukufanyika vizuri. Kwa hiyo, kama haujafanyika vizuri kwenye eneo lake naomba sana Mheshimiwa Mbunge awasiliane na TAMISEMI au na Wizara ya Maji ili tuweze kumwajibisha huyo Mhandisi Mshauri. (Makofi)

Name

Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:- Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:- Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?

Supplementary Question 6

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la maji la Mpanda Vijijini linalingana kabisa na tatizo la mradi wa maji wa World Bank katika kata ya Mkako, Wilayani Mbinga lakini pia katika Kata ya Litola, Wilayani Namtumbo na Kata ya Luwiko, Wilayani Songea Mjini, naomba kujua kwamba miradi hii imeonesha tayari imekamilika kwa mujibu wa taarifa, lakini haitoi maji hata kidogo, kiasi ambacho inaleta tafrani kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasanaomba nijue kwamba je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi katika Mkoa wangu wa Ruvuma kwenye maeneo haya niliyoyataja ili kuona hali halisi ya miradi hiyo na kuweza kuikamilisha ili wananchi, wanawake wote wa Mkoa wa Ruvuma kwenye maeneo hayo wapate maji?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kumjibu kwa haraka tu kwamba mimi nipo tayari. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba…

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Naomba nitoe maelekezo mahsusi kwamba karibu maeneo mengi miradi hii ina matatizo. Naomba niwaagize Wakurugenzi wote wa Halmashauri zote 185 by tarehe 20 mwezi Julai tupate takwimu za miradi yote iliyokamilika ipi inatoa maji na ipi haitoi maji tuje na suluhisho la kusaidia wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, endapo tutaona kwamba, tumepata takwimu hiyo, baadaye tunaona kwamba, Mbunge analalamikia mradi fulani, lakini katika orodha haupo, tutajua kwamba, mradi ule umehujumiwa makusudi na Halmashauri husika. Kwa hiyo, hatutosita kuchukua hatua stahiki kwa watu wote ambao kwa njia moja au nyingine wameshiriki kuhujumu hii miradi, mwisho wa siku wananchi wanashindwa kupata huduma hii ya maji. (Makofi)