Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Watumishi walio maeneo ya pembezoni mwa nchi ikiwemo Wilaya ya Ukerewe wanafanya kazi katika mazingira magumu, mfano walimu wa watumishi wa afya. Je, Serkali ina mpango gani wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa maeneo ya pembezoni?
Supplementary Question 1
MHE. MICHAEL J. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inakiri kwamba Ukerewe ni moja kati ya maeneo ambayo watumishi wake wanafanyakazi katika mazingira magumu na kwa kuwa huduma za elimu na afya visiwani Ukerewe hususan kwenye Visiwa vya Ilugwa, Ukara, Bwilo na kwingineko zinaadhirika sana na changamoto zinazowakabili watumishi kwenye maeneo haya.
Je, Serikali iko tayari kutoa fedha na kuwezesha sera hii ya malipo ya mishahara na motisha katika utumishi wa umma kuanza kutekelezwa ili kuokoa maisha na mazingira ya wakazi wa visiwa hivi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwanzoni mwa mwaka huu Serikali ilisambaza walimu kwenye Halmashauri zetu hasa walimu wa sayansi lakini kumekuwa na malalamiko mengi sana kutoka kwa walimu hawa kuishi katika mazingira magumu sana kwa sababu ya kutolipwa stahiki zao. Je, nini kauli ya Serikali juu ya tatizo hili? Nashukuru sana.
Name
Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NAUTWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli ukiangalia si tu kwamba wananchi wa Ukerewe wanaadhirika kutokana na ukosefu wa huduma za elimu na afya, lakini hata watumishi wenyewe walio katika mazingira magumu pia huduma ya elimu katika eneo lile na afya inapokuwa si nzuri inawafanya pia na wenyewe wasivutiwe kufanya kazi katika maeneo hayo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeiona changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kwa ujumla wake mwongozo huu haujaanza kutekelezwa lakini kupitia Bajeti ya Serikali na kupitia bajeti za Halmashauri ambazo zimepitishwa wameshaanza kutekeleza maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu pamoja na afya.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba tutaendelea kulifanyia kazi kama Serikali kutoa msisitizo ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yanayokabiliwa na changamoto hizi basi yanaweza kutengewa fedha za bajeti za kutosha ili kuweza kutekeleza sera hii.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusiana na walimu wa sayansi na hesabu walipangiwa vituo mwaka huu, kwamba hawajalipwa stahiki zao. Kwa kweli ni jambo ambalo limetusikitisha, na haswa ukizingatia katika Halmashauri moja unakuta mtu amepangiwa walimu 12 tu, inakuwaje Halmashauri inashindwa kuwahudumia kwa watumishi wake wapya waliopangiwa katika kituo kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, niseme kupitia hadhara hii natoa tamko au agizo kwa Halmashauri zote zilizopokea walimu wapya wa sayansi na hesabu lakini pia zilizopokea wataalam wa maabara za sayansi zihakikishe ndani ya siku saba zimewalipa watumishi hao stahiki zao zote. (Makofi)
Name
Martha Jachi Umbulla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Watumishi walio maeneo ya pembezoni mwa nchi ikiwemo Wilaya ya Ukerewe wanafanya kazi katika mazingira magumu, mfano walimu wa watumishi wa afya. Je, Serkali ina mpango gani wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa maeneo ya pembezoni?
Supplementary Question 2
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hamasa kubwa kwa vijana waajiriwa katika shule zetu hasa za maeneo ya pembezoni pamoja na vituo vya afya na zahanati, ni kule kuwepo kwa mitandao ya simu na umeme wa uhakika, kwa kuwa vijana wetu kwa kweli wanapenda kutumia simu za mikononi katika mitandao hiyo kwa uhakika; na kwa kuwa maeneo yetu ya vijijini hasa katika Mkoa wetu wa Manyara na kwingineko maeneo ya pembezoni, huduma hiyo ya umeme na mitandao ya simu haipo.
Je, Serikali hasa Wizara ya Utumishi ina mikakati gani mahususi ya kuwa na mawasiliano ya karibu kuhakikisha kwamba katika maeneo ya pembezoni katika shule hasa za sekondari na vituo vya afya kunakuwepo na umeme ili kutia hamasa ya waajiriwa waendelee kuishi maeneo hayo? (Makofi)
Name
Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba kwa utafiti uliofanywa na bodi yetu ya mishahara katika utumishi wa umma mwaka 2014/ 2015, moja ya changamoto ambazo zilibainika, kwanza katika mazingira haya magumu inategemeana na sekta kwa sekta maeneo mengine jiografia, hali ya miundombinu, huduma za kijamii zilizopo; lakini pia nafurahi kwamba ametaja suala zima la mitandao ya simu pamoja na umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kumuhakikishia tu kwamba kupitia ripoti ile ya utafiti tulitoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini pia tumewasilisha katika Wizara husika ikiwemo Wizara ya Nishati na nyinginezo kuhakikisha kwamba wanapopanga mipango yao ya maendeleo basi wanatoa vipaumbele katika maeneo haya yenye mazingira magumu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved