Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rose Kamili Sukum

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ROSE K. SUKUM aliuliza:- Serikali ina utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya shule za bweni nchini. Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 31/08/2013 hadi 10/02/2014 Halmashauri ya Hanang ilipokea kutoka Serikali Kuu kiasi cha shilingi 508,779,500 kwa ajili ya chakula cha shule za bweni. Taarifa zinaonesha kuwa fedha zilizotumika kununua chakula ni shilingi 225,585,000. Kwa takwimu hizo bakaa ni shilingi 283,194,500 na kwa mujibu wa mkaguzi, bakaa hiyo haionekani kwenye akaunti yoyote ya benki. (a) Je, fedha hizo zinarudishwa Hazina bila ya uwepo wa nyaraka zozote toka Halmashauri kuonesha muamala unavyofanya kazi? (b) Je, kama fedha hizo hazikurudishwa Hazina, nani anaweza kuidhinisha matumizi bila ya mpango wake kupitishwa na Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri? (c) Je, kama fedha zimetumika bila kupangiwa na Kamati halali, ni kwa nini wahusika bado wanaendelea kuwa ofisini bila ya kufunguliwa mashtaka ya wizi wa kuaminika?

Supplementary Question 1

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba unipe fursa niweze kumuelezea Mheshimiwa Waziri alivyodanganywa na waliomjibia maswali haya.
Mheshimiwa Spika, uchunguzi umeshafanyika Wilaya ya Hanang na uchunguzi huo umefanywa na timu ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa ajili kujua ubadhirifu wa fedha hizo, sio tu fedha za chakula bali ni fedha nyingine pia zipo za shilingi bilioni moja.
Mheshimiwa Spika, nasikitika Mheshimiwa Waziri, nimekuletea document hizi za uchunguzi uliofanyika ndani ya ofisi yenu, leo unakuja kujibu kirahisi kiasi hiki ina maana kwamba wewe umedanganywa, haya si majibu yaliyotakiwa. Fedha hizi zimetumika, shilingi milioni 100 unazozisema hizo zimetumika ni fedha za SEDEP ziko kwenye uchunguzi hii na nitakukabidhi sasa hivi. Hizi za SEDEP zimetumika kwenda kununua magodoro na kadhalika kwenye hayo mabweni. Kwa hiyo ni kosa moja wapo lilitumika la kutumia fedha ambazo hazistahili kutumika.
Mheshimiwa Spika, la pili taarifa ya Mkaguzi wa Ndani imeeleza Aprili 15 zikisema matumizi mabovu ya hizi fedha, fedha hizi hazikutumiwa na halmashauri zimetumiwa na mtu mmoja au watu wachache ndani ya Halmashauri. Sasa iweje Halmashauri irudishe hizi fedha ili kuweza kulipia deni la mtu ambaye amekula hizo hela? Pia kwa taarifa uliyosema majibu ya Mkurugenzi kwamba amesimamishwa, Mkurugenzi yuko kazini anafanya kazi yuko ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, na hawa watumishi wengine wako Wilaya ya Hanang wanafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, naomba unisaidie, ni kwa nini hawa watumishi hawakuchukuliwa hatua mpaka sasa hivi na taarifa hii iko ofisini kwako?
La pili, kama kweli inatakiwa ithibitike, utatumia hatua gani kuwezesha uchunguzi maalum ufanyike kwa ajili ya kujua ubadhilifu wa fedha za Wilaya ya Hanang? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza wizi ni wizi hakuna wizi mdogo hakuna wizi mkubwa; wizi ni wizi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sukum kwamba japokuwa hapa tulikuwa tunaeleza ule mchakato wa zile fedha maalum lakini kilichokuwepo kutokana na specific questions ambazo umeuliza ni kwamba inaonekana Halmashauri ya Hanang si hiyo, kuna lidudu likubwa liko katika Halmashauri ya Hanang. Ndiyo maana nimesema wizi ni wizi hauna mjadala.
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie, haya yote aliyosema Mheshimiwa Sukum kwamba tutafanyaje, nimesema hapa tumechukua hatua. Kama kuna ubabaishaji wa aina yoyote katika zile hatua tulizochukua naomba nikuhakikishie kwamba by this week ambapo leo Ijumaa, by next week ofisi yetu itatuma special investigation team. Lengo lake kubwa ni kwenda kujiridhisha ni kitu gani kimejificha ndani ya boksi; kwenda kutatuta tatizo la msingi la fedha ambazo inawezekana zimetumika kinyume cha taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na hili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sukum; katika jambo hili Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia uzembe wa mtu yoyote wa aina yoyote. Hili naomba niseme kwamba kwa concern aliyozungumza Mheshimiwa Rose Kamil Sukum, tunaiagiza timu yetu ya investigation and follow up kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, si kutoka ofisi ya Mkoa, kutoka katika ofisi yetu; iende ikafanye uchunguzi wa haraka, by next week tuweze kupata majibu halisia. Lengo kubwa tulinde fedha za walipa kodi wa Tanzania na hatimaye ziweze kusaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuyajibu maswali yake kwa pamoja kwa muktadha wa namna hiyo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri Jafo, lakini concern iliyooneshwa na Mheshimiwa Mbunge ni kubwa na kwa sababu hiyo basi kwa kuwa pia taarifa zetu zinakuwa tofauti na alizonazo, nimuombe baada ya kipindi cha maswali aje ofisini kwetu tuweze kupata taarifa zaidi, kwa sababu jambo hili ni la muda mrefu na bahati mbaya yule Mkurugenzi aliyekuwa pale sasa hayuko pale, lakini kesi ipo na inaendelea. Pengine kwa hatua hii sasa tunahitaji kwenda kwa haraka zaidi kulingana na concern aliyoonesha Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ni kweli kwamba kumekuwa na maamuzi mabaya kwenye Halmashauri yenye lengo la kutaka kuzitafuna fedha fulani kama zipo ambayo chanzo chake huwa ni kubadilisha matumizi. Waheshimiwa Wabunge mimi napenda niwasihi sana, mabadiliko ya matumizi ya fedha za miradi zinazoletwa kwenye Halmashauri yanafanywa na Waheshimiwa Madiwani na vikao vile vinaridhia. Kupitia mwanya huo basi yanayotokea ni mambo ya ajabu. Kuna watu wamebadilisha hela ya mradi ambayo fedha inatolewa na World Bank wamekwenda kufanya yao, wamegawana posho, wamelipana vitu vya ajabu na wamepeana safari.
Mheshimiwa Spika, sasa kuanzia sasa uamuzi tulioufanya sisi kama Wizara ni kwamba mabadiliko ya matumizi ya fedha yoyote itabidi na Katibu Mkuu - TAMISEMI aridhie. Kwa sababu yanayofanywa huko ni mambo ya ajabu sana, kuna watu wanabadili fedha lakini kubadili huko ni kwa lengo la kwenda kutaka kuzitafuna. Kwa hiyo, sisi Serikali ya Awamu ya Tano hatutakubali jambo hilo liendelee kutokea. Niwasihi Waheshimiwa Wabunge mtusaidie kwa sababu na ninyi mnakuwepo kwenye vikao hivyo. (Makofi)

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. ROSE K. SUKUM aliuliza:- Serikali ina utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya shule za bweni nchini. Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 31/08/2013 hadi 10/02/2014 Halmashauri ya Hanang ilipokea kutoka Serikali Kuu kiasi cha shilingi 508,779,500 kwa ajili ya chakula cha shule za bweni. Taarifa zinaonesha kuwa fedha zilizotumika kununua chakula ni shilingi 225,585,000. Kwa takwimu hizo bakaa ni shilingi 283,194,500 na kwa mujibu wa mkaguzi, bakaa hiyo haionekani kwenye akaunti yoyote ya benki. (a) Je, fedha hizo zinarudishwa Hazina bila ya uwepo wa nyaraka zozote toka Halmashauri kuonesha muamala unavyofanya kazi? (b) Je, kama fedha hizo hazikurudishwa Hazina, nani anaweza kuidhinisha matumizi bila ya mpango wake kupitishwa na Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri? (c) Je, kama fedha zimetumika bila kupangiwa na Kamati halali, ni kwa nini wahusika bado wanaendelea kuwa ofisini bila ya kufunguliwa mashtaka ya wizi wa kuaminika?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza nitashukuru sana kama TAMISEMI itakwenda kujua ukweli ni nini. Swali langu ni kwamba shule zile zilizotajwa za Katesh, Gendabi, Balangdalalu na Bassodesh sasa hivi kwa muda mrefu hazijapewa hela za chakula na ni shule za bweni. Taarifa hizo nimezifikisha kwa Mawaziri, nataka kujua, je, watoto waendelee kukaa bila chakula au kuna hatua ambazo zimechukuliwa? Ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli siku ya Mei Mosi tulikuwepo pale Katesh na Mama Mary Nagu na alilileta tena jambo. Hata hivyo alilifikisha ofisini kwetu na ofisi ya Naibu Katibu Mkuu Elimu ilikuwa inashughulikia jambo hili. Kwa hiyo Mama Mary Nagu naomba vuta subira, tunadhani jambo hili linafikishwa mahali pazuri. Nadhani tutahakikisha kwamba watoto wale wanaweza kupata huduma kama ulivyopeleka katika maombi yale. (Makofi)