Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Roman Selasini
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Primary Question
MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:- Wapo wananchi wengi waliotuhumiwa na kushtakiwa katika Mahakama tofauti na kutozwa faini na baada ya kulipa faini hizo wakakata rufaa Mahakama za juu kulalamikia hukumu hizo na Mahakama za juu zikawaona hawana hatia. (a) Je, Serikali inayo kumbukumbu ya taarifa za wananchi wa namna hiyo? (b) Na kama Serikali inazo taarifa hizo, je, ni lini wananchi hao watarejeshewa fedha zao?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri haya ya kaka yangu Profesa Kabudi, nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wengi sana wanakosa haki zao, kwanza kwa kutojua kwamba wanapaswa kudai fedha zao walizolipa kama faini baada ya kushinda kesi na pili kwa sababu nakala za hukumu custodian wake ni Mahakama yenyewe.
Je, Serikali haioni kwamba kwa kutotoa maelezo kwa hawa warufani wakati rufani zao zikiwa zinasomwa kwamba wanatakiwa wafuatilie zile faini walizolipa baada ya kushinda, Serikali haioni kwamba inawadhulumu na au inaendelea kuwaadhibu kutokana na kutowarejeshea fedha zao?
Swali la pili, kwa kuwa Mahakama huwa inatoa muda maalum wa kukata rufaa na mtuhumiwa yule anapokata rufaa Mahakama inakuwa inajua. Je, ni kwa nini Mahakama inapopokea fedha zile isiziingize kwenye akaunti ya akiba kwa ajili ya kusubiri rufani itakapoamuliwa na badala yake inaingiza kwenye akaunti ya mapato na hivyo kusababisha fedha zile zinatumika, zinapohitajika inakuwa shida kupatikana?(Makofi)
Name
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, moja ni kweli inawezekana wananchi wengi hawafahamu kwamba mara baada ya kuwa wameshinda rufaa zao wana haki ya kurejeshewa faini ambayo walikuwa wamelipa. Kwa hiyo, Wizara pamoja na Mahakama tutafanya jitihada kutoa elimu na maelezo kwa wananchi kwamba mara wanapokuwa wameshinda rufaa zao za mwisho basi waweze kufuatilia malipo ya rufaa zao kwa sababu ni haki yao. (Makofi)
Kuhusu swali la pili, kwa kuwa utaratibu wa Serikali ni kwamba, faini zinachukuliwa kama maduhuli na zinakatiwa risiti ya Hazina, basi jambo hilo tutakaa na Hazina ili tuweze kuona utaratibu unaoweza kutumika ili kuhakikisha kwamba malipo ya faini yanarejeshwa kwa haraka iwezekanavyo ili wananchi ambao wamelipa fedha hizo waweze kuzipata hela zao kwa wakati. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved