Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hassan Elias Masala
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Primary Question
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:- Je, ni nini kauli ya Serikali katika kushughulikia tatizo la migogoro ya mipaka katika Kambi za JKT Nachingwea na Kikosi Namba 41 Majimaji na vijiji vinavyozunguka Kambi hizo?
Supplementary Question 1
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na wananchi hao ambao Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba hawajalipwa fidia na anakiri kwamba wakati maeneo haya vikosi wanayatwaa hawajalipwa chochote bado vikosi vyetu vimeendelea kuwafukuza wananchi hawa wasifanye shughuli zozote ikiwemo kuokota korosho zao kwa wale ambao walishapanda mikorosho.
Naomba kupata kauli ya Serikali juu hatma ya watu hawa wakati wanaendelea kutengewa hii bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri ameisema ili waweze kuendelea kufanya shughuli zao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Waziri naomba kupata commitment ya Serikali kwa sababu tatizo ni la muda mrefu na Tume nyingi zimeshaundwa na tayari zilishaleta majibu ya kukiri kwamba kuna tatizo.
Ni lini Serikali sasa itaenda kufanya hili zoezi ili tatizo hili liondoke na wananchi wale waweze kujua hatma yao? (Makofi)
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, lazima tukiri kwamba tatizo kubwa limekuwa ni upungufu wa bajeti na kwa maana hiyo kupelekea wananchi wanaostahili kulipwa fidia kuchelewa. Hata hivyo, kulikuwa kuna maamuzi ya makusudi ya kuzuia wananchi kufanya shughuli za kibinadamu katika makambi haya. Sababu kubwa ya maamuzi hayo ni kwamba katika baadhi makambi haya kuna silaha na kuna milipuko ambayo inaweza kuleta athari kwa wananchi na ndiyo sababu wakakatazwa kufanya shughuli za kibinadamu.
Lakini ukiacha tatizo hilo, wapo wananchi ambao wakipewa ruhusa ya kufanya hivyo basi wanafanya maendelezo makubwa, wengine wanajenga hata nyumba ambayo inapelekea uthamini na fidia zao kuwa kubwa mno. Hizo ndiyo sababu zilizopelekea wakazuiwa kufanya shughuli zote za kibinadamu ili kwanza wasidhurike lakini pili wasiendeleze maeneo hayo kwa sababu yatapelekea fidia kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, kuhusu commitment ya Serikali kwamba ni lini zoezi hili litakamilika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumepokea fedha hizi kutoka kwenye bajeti yetu jukumu hili litafanyika mara moja ili tuondokane na tatizo hili la muda mrefu. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved