Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Willy Qulwi Qambalo
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Karatu
Primary Question
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:- Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa ardhi yote ya Tanzania inapangwa, inapimwa na kumilikishwa kisheria kama namna mojawapo ya kuondoa migogoro hususan ya wakulima na wafugaji nchini?
Supplementary Question 1
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Niulize maswali mawili madogo ya nyongeza; kama ambavyo Serikali imekiri katika majibu yake juu ya umuhimu wa zoezi hili la kupanga, kupima na hatimaye kumilikisha ardhi kisheria, lakini nakumbuka katika hotuba ya Waziri ya mwaka 2016/2017 aliliambia Bunge hili kwamba ni 15% tu ya ardhi ya nchi hii ndiyo imefanyiwa upangaji, upimaji na umilikishaji na nyingi ya hizo utazikuta ziko maeneo ya mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuliachia zoezi hili muhimu sana kama ambavyo Serikali imekiri kwa halmashauri zetu za wilaya na vijiji ni zoezi ambalo lina gharama kubwa na halmashauri nyingi hazitaweza kabisa. Je, kama Serikali inatambua umuhimu wa zoezi hili, kwa nini Serikali Kuu sasa isiingilie kati ikazisaidia mamlaka hizo za wilaya na vijiji kuhakikisha ardhi yote ya nchi hii inapimwa, inapangwa na pia kumilikishwa kisheria? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya Mwaka 1999 kifungu cha saba (7) kinamtaka Kamishna wa Ardhi kutoa cheti cha ardhi ya kijiji kwa vile vijiji ambavyo mipaka yake imetambulika na imekubalika lakini viko vijiji ambavyo vina sifa hiyo na havijapata hati hiyo. Nini kauli ya Serikali kwa Makamishna na Maafisa wa Ardhi wa Wilaya ili vijiji vipate hati hiyo muhimu sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu imekuwa inasaidia zoezi la upangaji, upimaji na hata kuandaa matumizi bora ya ardhi katika vijiji na master plan. Hata hivyo, kimsingi kwa mujibu wa sheria, zoezi hili lazima lisimamiwe na ni jukumu la halmashauri husika na vijiji. Ni kweli, kazi ya vijiji kupanga matumizi bora ya ardhi unaweza ukasema ni gharama, lakini viko vijiji ambavyo vimesimamia na vimepanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyao na maisha yanaendelea vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za upangaji wa matumizi bora katika kijiji kimoja haizidi shilingi milioni 22. Sasa kama wananchi wote wataona ni busara kutoa shilingi milioni 22 ili kila mmoja mwananchi wa kijiji kile awe na uhakika wa ardhi yake, wafanye hivyo, kwa sababu si gharama kwa sababu unapanga na kupima mara moja katika maisha yenu yote. Kwa hiyo, bado nahamasisha kwamba pamoja na Serikali Kuu kuendelea kusaidia, lakini jukumu hili lazima liwe ni jukumu la msingi, kwa mujibu wa sheria, la mamlaka za vijiji na wilaya husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, kama nilivyosema, Serikali inaandaa mpango wa jumla wa kupanga na kupima nchi nzima. Mpango huu tutaueleza vizuri kwenye budget speech nitakayosoma mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ni kweli kwamba ni jukumu la Kamishna kutoa cheti cha vijiji. Sasa kama ana taarifa juu ya vijiji ambavyo anahitaji na ambavyo havina vyeti vya vijiji, tuwasiliane ili tujue kwa nini imetokea hivyo tuweze kurekebisha tuwapatie hivyo vyeti.
Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea, Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima sasa aulize swali lake.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved