Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:- Jimbo la Segerea ni moja kati ya Majimbo ya Dar es Salaam ambalo wakazi wake ni wengi na wa kipato cha chini na sababu kubwa ikiwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara hasa madaraja na mitaro, hivyo kusababisha mafuriko ya mara kwa mara. Je, ni lini Serikali itajenga madaraja ya Tabata Kisiwani na Kisukuru sambamba na kujenga mitaro ili kupunguza adha ya mafuriko katika Kata za Jimbo hili?

Supplementary Question 1

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Majibu ya Naibu Waziri tumeyasikia wakati wote. Mradi wa mfereji anaousema wa DMDP ni mradi ambao tumeambiwa utatekelezwa tangu mwaka 2014 na wakazi wa kata zinazopitiwa na mradi huo waliambiwa wasiendeleze maeneo yao tangu 2014 wakiendelea kuhangaika na mafuriko kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna changamoto ya madaraja na barabara Kata ya Bonyokwa, Kata ya Kinyerezi, Kata ya Segerea, Kata ya Liwiti na kubwa kuliko ni Kata ya Tabata katika barabara ya kwenda Mwananchi, kalvati limebomoka na kwa sasa ninavyoongea…

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali; je, ni lini mradi huo mkubwa wa DMDP utajengwa na barabara au Daraja la Kisiwani? Swali la kwanza.
Swali la pili, uanzishwaji wa TARURA umeondoa uwajibikaji wa Halmashauri sambamba na Madiwani moja kwa moja katika ujenzi wa barabara za mitaa. Je, Wizara ina mkakati gani kuhuisha kazi za TARURA ili waweze kutoa report katika Baraza la Madiwani ambalo moja kwa moja ndiyo wanawajibika kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kujua kero zao za moja kwa moja za barabara? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Theonest amesema imekuwa ni muda mrefu hadithi imekuwa ikisemwa, lakini utakubaliana nami kwamba katika majibu yangu kwenye swali la msingi, nimemwambia kwamba kandarasi tunatarajia itatangazwa mwezi Mei na mwezi Mei siyo mbali sana, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumeahidi tutatekeleza katika hili ambalo nimelisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameongelea juu ya suala zima la uanzishwaji wa chombo hiki cha TARURA na anachoomba ni namna gani TARURA watahuisha ili wananchi waweze kupata ushiriki wao kwa kupitia Waheshimiwa Madiwani na Wabunge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA ina wajibu wa kuhakikisha kwamba taarifa zake zinapelekwa DCC na DCC Waheshimiwa Wabunge ni Wajumbe, lakini Mwenyekiti au Meya ni Wajumbe na Wakurugenzi ni Wajumbe. Kwa hiyo, taarifa itakuwa inatolewa hapo na tutapata fursa ya kuweza kuwahoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, pia kwenye chombo cha RCC ambapo sisi Waheshimiwa wote ni Wajumbe, naomba tushiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijaribu kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba kabla ya kuanzishwa kwa TARURA kila Mbunge na hasa kila Diwani alikuwa anaomba apate angalau hata kilomita moja ya kipande cha barabara au kalavati litengenezwe upande wake kiasi kwamba ule ufanisi (value for money) ilikuwa haionekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukienzi chombo hiki, bado ni mapema kabisa. Maeneo mengine ambayo TARURA imeanza kufanya kazi, wanapongeza. Naomba tukiunge mkono. (Makofi)