Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Serikali imeunda timu ya wataalam kutoka Wizara nne kupitia nchi nzima kuangalia hadhi za hifadhi zetu (Mapori ya Akiba na Hifadhi za Msitu) ili kuja na mpango utakaondoa kabisa migogoro ya ardhi inayotokea kati ya Hifadhi na Wafugaji, Wakulima na Hifadhi na watumiaji wengine. (i) Je, ni lini kazi hiyo itakamilika? (ii) Je, mpaka sasa Timu hiyo imetembelea maeneo mangapi na ni mikoa gani?

Supplementary Question 1

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kutokana na jibu la msingi tumeona namna gani ambavyo migogoro ni mingi hapa nchini. Migogoro hii inapoteza maisha ya Watanzania, migogoro hii inapoteza mali za Watanzania, watu wanafilisiwa mifugo yao, wanaharibiwa nyumba zao, wanachomewa vitu vyao, lakini pia migogoro hii inadumaza uchumi kwa kuwa watu wana - concentrate kwenye migogoro wanashindwa kufanya masuala ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nategemea Mheshimiwa Waziri baada ya kubaini matatizo haya aje na mpango mkakati, namna gani za haraka kutatua migogoro hii, tofauti anavyosema hapa wataendelea kushirikiana na wadau. Wakati timu zinaendelea kufanya kazi kubaini migogoro hii, bado Watanzania wameendelea kunyanyasika, wakati huu tunapoongea bado watu wanaendelea kunyanyaswa kwenye maeneo ya hifadhi, mipaka, mifugo yao inaendelea kupigwa mnada, vyanzo vinazidi kuharibiwa, nilitegemea wakati Serikali haijaja na mpango wa kutatua matatizo haya, wangesitisha kuendelea kunyanyasa watu ili wenyewe wafanye kazi yao, ndiyo waendelee kushughulikia watu ambao wako ndani ya hifadhi ambapo wamesajiliwa kisheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 2012/2013, Wizara ya Maliasili na Utalii ilinyang’anya vijiji 26 vyeti vya usajili kutoka Wilaya ya Kaliua kwa madai kwamba vimesajiliwa kinyume na utaratibu wakati walisajiliwa kisheria chini ya Wizara ya TAMISEMI, suala ambalo sasa hivi limeenda kuumiza uchumi wa wananchi wale kwa sababu makampuni ya tumbaku yamesema hayataingia mikataba ya biashara kununua tumbaku kwenye vijiji 26 kwa sababu havina vyeti vya usajili wa vijiji.
Mheshimiwa Spika, naomba Wizara ya Maliasili ituambie itarudisha lini vyeti vya usajili kwa vijiji 26 ambavyo leo wanaenda kuathirika kiuchumi kwa kuwa walisajiliwa kisheria, wanaishi kisheria, kama lilifanyika kosa ni suala la Serikali? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nitoe taarifa kwamba siyo lengo la watumishi wetu walioko kwenye hifadhi kuwanyanyasa wananchi, kwa mujibu wa kanuni na taratibu hawaruhusiwi kufanya hivyo, kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanalinda hifadhi na siyo kuwanyanyasa wananchi wanaozunguka katika maeneo hayo. Kwa hiyo kama kuna kesi kama hizo naomba tuwasiliane na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuwachukulia hatua stahiki hao ambao wanawanyanyasa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu mpango mkakati nimeeleza kwamba timu hiyo baada ya kukamilisha hilo zoezi Wizara zote zinazohusika zimepewa hii taarifa kwa ajili ya kuanza kuweka mkakati wa makusudi kabisa wa kutekeleza na kutatua migogoro ya namna hiyo. Hiyo kazi imeshaanza na kila Wizara ina mpango wake inatekeleza, sisi kama Maliasili na Utalii tumejipanga kwa ajili ya hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba, Mheshimiwa Waziri Mkuu alituagiza kuweka mipaka katika maeneo yote yenye migogoro, mipaka ile baada ya kuwekwa sasa Serikali inatathmini ni maeneo yapi yana migogoro, yapi yapo ndani ya hifadhi, yapi tunaweza kuyaachia, yapi lazima tuwape fidia wananchi na yapi tuwaondoe wananchi. Baada ya hiyo yote kukamilika, hatua stahiki zitafanyika na Mheshimiwa Mbunge atapata ule mpango wa Serikali kwa ujumla katika maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, kuhusu wananchi ambao Mheshimiwa Mbunge anasema walinyanga’anywa vyeti vyao wa usajili wa vijiji, hiyo taarifa naomba niseme bado sina lakini nitaifuatilia, nitashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba angalau tunapitia na tuone tunashirikiana pamoja na Wizara zingine ili katika hivi vijiji 366 ambavyo viko ndani ya hifadhi tuone kama na hivyo navyo vipo ili kusudi tuone hatua itakayochukuliwa na Serikali, basi itahusu maeneo yote hayo pamoja na vijiji alivyovisema. (Makofi)