Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Hospitali ya Amana imepelekwa Wizarani, hivyo Wilaya ya Ilala kwa sasa haina Hospitali ya Wilaya. Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia Hospitali ya Kivule itumike kama Hospitali ya Wilaya ya Ilala?
Supplementary Question 1
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, lakini naomba niwashukuru sana Serikali ya Korea, Serikali ya Tanzania na Manispaa ya Ilala ambayo inaongozwa na UKAWA na wananchi wa Kata ya Chanika kwa kutoa ushirikiano wa kupata hospitali kubwa ya mama na mtoto katika eneo hilo. Nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri anaonesha kwamba fedha kutoka Serikali Kuu ni shilingi bilioni moja, lakini kwenye bajeti ya TAMISEMI ambayo tumeshapitisha katika Bunge letu Tukufu ilionesha shilingi bilioni 1.5. Napenda nijue hii ni nyingine imeongezeka au ni ile ya shilingi bilioni 1.5 ambayo sasa imeshuka tena imekuwa one billion?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kuna changamoto kubwa katika eneo hili na Mheshimiwa Waziri anakubali kwamba kuna mpango wa kujenga hospitali hii; je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutembelea eneo hili aone kwanza eneo lipo vizuri, wananchi wametoa ushirikiano wa ekari 45 twende tufanye ziara ili waweke msukumo kwa kujengwa kwa haraka na kwa uhakika ili huduma ya afya iweze kupatikana katika eneo hili ambayo itahudumia Jimbo la Ukonga, Mkuranga na eneo la Kisarawe? Ahsante. (Makofi)
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waitara anauliza kwamba katika orodha ya Hospitali za Wilaya 67 ambazo zinajengwa, kwa hesabu yake anaona ilikuwa inaonesha kwamba Hospitali ya Kivule imetengewa shilingi bilioni 1.5, lakini taarifa nilizonazo ni kwamba imetengwa shilingi bilioni moja kutoka Serikali Kuu, lakini ukiunganisha na shilingi bilioni mbili ambayo ni mapato ya ndani ya Manispaa, maana yake wao wanakuwa na shilingi bilioni tatu. Kwa ramani ambazo zinatolewa kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya ni shilingi bilioni 1.5. Kwa hiyo, wao wako mara mbili yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba hospitali zinajengwa za kisasa, lakini kwa kutumia utaratibu wa Force Account.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kiasi hicho ni cha kutosha tukisimamia tukahakikisha kwamba kila shilingi ambayo inatoka inaenda kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili juu ya kwenda kutembelea maeneo hayo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nina mpango wa kwenda kutembelea eneo ambalo kinapanuliwa Kituo cha Afya cha Buguruni, Kinyerezi na maeneo mengine yote ili na mimi nijiridhishe tuwe katika page moja tunapoongea na Mheshimiwa Mbunge.
Name
Edward Franz Mwalongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Hospitali ya Amana imepelekwa Wizarani, hivyo Wilaya ya Ilala kwa sasa haina Hospitali ya Wilaya. Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia Hospitali ya Kivule itumike kama Hospitali ya Wilaya ya Ilala?
Supplementary Question 2
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe, Hospitali ya Kibena ndiyo hospitali inayotumika kama Hospitali ya Mkoa, lakini imechakaa sana na haina wodi ya wanaume wala x-ray.
Je, ni lini Serikali itatusaidia watu wa Njombe kupata wodi ya wanaume na x-ray?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala zima la kuchakaa Hospitali ya Wilaya ya Njombe ambayo kimsingi ilijengwa miaka ya zamani sana, tunakiri na tunatambua juu ya uchakavu huu. Kwa kadri bajeti itakavyoruhusu, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunazikarabati Hospitali za Wilaya ili zifanane na hadhi ya sasa hivi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika zile Hospitali ambazo zitakarabatiwa wakati bajeti ikiruhusu na Njombe nao hatutawasahau.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved