Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAINABU M. AMIRI aliuliza:- Je ni lini Serikali itapunguza bei ya gesi kwa matumizi ya majumbani ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kutumia gesi kwa matumizi yao ya nyumbani na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa?

Supplementary Question 1

MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na kugundulika kwa gesi nchini mwetu, je, ni lini Serikali itasitisha uingizaji wa gesi ili tuweze kutumia gesi yetu hapa nchini?
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pilot project iliyofanyika ni Mikocheni Dar es Salaam, je, ni vigezo gani vimezingatiwa katika project hiyo na isiwe kule ilikotoka gesi Mtwara? (Makofi)

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zainabu Mndolwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameuliza ni lini Serikali itasitisha uagizaji wa gesi kutoka nje ya nchi. Ni kweli ugunduzi wa gesi asilia iliyogunduliwa hapa nchini ni gesi zaidi ya mita za ujazo trilioni 55,000. Nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge matumizi ya gesi yapo mengi kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi ikiwemo kwenye uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwanda na matumizi ya majumbani.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna mipango mbalimbali ambayo inafanywa na Serikali ikiwemo pia ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi asilia Mkoani Lindi. Kwa hiyo, baada ya kiwanda hiki kukamilika na hizi fursa mbalimbali za usambazaji gesi na miundombinu mbalimbali ya kusambaza gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani itakapokamilika, Serikali itatafakari kwa kina namna ambavyo inaweza kusitisha uagizaji wa gesi hiyo nchini. Kwa sasa bado tuna mahitaji na kwa kuwa mipango inaendelea, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatafakari na kuchukua hatua pale ambapo tutakuwa tumejiridhisha na soko na uhitaji wa gesi asilia ndani ya nchi na kwa matumizi ya nchi. (Makofi)
Mheshimwia Spika, swali lake la pili alikuwa anauliza kuhusu vigezo vilivyotumika kwa maeneo ya kusambaza gesi kwa matumizi ya majumbani na ameuainisha Mkoa wa Mtwara. Nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuna miradi na tafiti zinazoendelea katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mwanza na Tanga chini ya Mradi wa JICA ili kuona mahitaji ya matumizi ya gesi ya kupikia ili kuanza mradi wa usambazaji wa gesi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, nimthibitishie katika Mkoa wa Mtwara kwa mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 140 zimetengwa kuendelea na study hiyo na kwamba mkoa huo utapatiwa usambazaji wa gesi kwa matumizi ya nyumbani. Nakushukuru.

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAINABU M. AMIRI aliuliza:- Je ni lini Serikali itapunguza bei ya gesi kwa matumizi ya majumbani ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kutumia gesi kwa matumizi yao ya nyumbani na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa?

Supplementary Question 2

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kufuatia ugunduzi wa gesi, Serikali ya CCM iliwahakikishia Watanzania na wananchi wa Mtwara kwamba maisha yetu kwa kiwango kikubwa yatabadilika. Ikumbukwe kwamba bomba la gesi lilijengwa kwa mkopo usiopungua shilingi trilioni 1.5 kwenda shilingi trilioni 2. Hivi tunavyozungumza na kwa taarifa za Serikali inaonesha kwamba tunatumia asilimia 5 tu ya gesi katika bomba husika. Nataka tu Serikali ituambie, Deni la Taifa linakua, tulikopa tukajenga bomba tukajua kwamba tunapata suluhu lakini sasa hivi tunatumia bomba asilimia 5, ni nini kimetokea hapo katikati kilichopelekea kushindwa kulitumia kwa asilimia 95 ? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaambiwa tena kuna mpango Stigler’s Gorge wa kuzalisha umeme. Sasa mtuambie bomba la gesi limekwamia wapi katika uzalishaji wa umeme na hii Stiegler’s Gorge inaanzia wapi ili kama Taifa tuwe na taarifa, maana tunaona tunapelekwapelekwa tu. (Makofi)

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la Mheshimiwa Halima Mdee, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilitekeleza mradi mkubwa huu wa ujenzi wa bomba la gesi la Mkoa wa Mtwara. Kama alivyoeleza kwenye swali lake, kwa sasa matumizi ya kusafirisha gesi kwa kupitia bomba hili kwa mwaka huu unaoendelea imefika lita za ujazo milioni 175 kutoka milioni 145 za mwaka 2016/2017, ni wazi ongezeko linatokana na mahitaji makubwa.
Mheshimiwa Spika, naomba nimthibitishie tulipokuwa tunajenga bomba hili na ahadi tulizotoa kwa wana Mtwara, ahadi zile ni sahihi kwa sababu kuna miradi mbalimbali ambayo inayoendelea. Kwa mfano, Mtwara peke yake tunajega mradi wa kuzalisha umeme wa megawatts 300 kwa kutumia gesi asilia ya Mkoa wa Mtwara. Sambamba na hilo, pia kuna mpango wa kujenga mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia Somanga Fungu, kwa kuzalisha megawatts 330 kwa kutumia gesi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yoyote lazima izalishe umeme kwa vyanzo mbalimbali, huwezi kutumia gesi asilia peke yake ukatosheleza mahitaji ya nchi nzima. Ndiyo maana tunazalisha umeme kwa kutumia maji na gesi. Sasa hivi zaidi ya asilimia ya 50 megawatts zinazozalishwa zinatumia gesi. Kwa hiyo, ni wazi kwamba gesi ambayo iligundulika Mtwara imeleta tija katika uzalishaji wa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama tunavyofahamu umuhimu wa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vingine, Serikali imetafakari, kwa sababu lengo la Serikali ni kuzalisha umeme wa bei nafuu na kumfikia mtumiaji kwa bei nafuu. Ndiyo maana Serikali imekuja na mradi wa Stiegler’s Gorge utakaozalisha megawatts 2,100. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimewahi kusema ndani ya Bunge lako Tukufu kwamba uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji una unafuu zaidi, unatumia shilingi 36 ukilinganisha na gesi ambayo ni shilingi 147. Kwa nchi inayotarajiwa kujenga viwanda nchi nzima na kazi inayoendelea lazima tuzalishe umeme kwa wingi. Kwa kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ni kuzalisha megawatts 5,000 mradi wa Stiegler’s Gorge ndiyo wakati wake muafaka. Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)