Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Livingstone Joseph Lusinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Primary Question
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani juu ya wanyama waharibifu hususan tembo ambao wamesambaa hovyo katika Jimbo la Mtera na kufanya uharibifu mkubwa pamoja na kuua watu?
Supplementary Question 1
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kuuwawa kwa Ndugu Emmanuel Ernest wa Ilolo na Stefano Ndalu wa Nhinyi na Amani Joseph Sita wa Mvumi Mission kujeruhiwa vibaya na kupata malipo kidogo sana, je, ni lini sasa Serikali itaruhusu vijiji viweze kumiliki silaha kwa ajili ya kujilinda na wanyama hao wakali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, pesa aliyoitaja Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa imelipwa kwa watu 27 ukiigawanya ni sawasawa na shilingi 278,518. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kuwatangazia Watanzania kwamba katika nchi yetu tembo wana thamani kubwa kuliko uhai wa watu? Ahsante. (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu maswali hayo, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Livingstone Lusinde kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kufuatilia na kuwatetea wananchi wake. Kutokana na kazi yake ndiyo maana anajulikana kama kibajaji yaani kwa mambo makubwa anayoyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kuwapa pole wale wananchi wote ambao wameathirika ama wameuwawa na wanyama wakali, nawapa pole sana. Niseme tu kwamba hili suala alilolileta na kupendekeza kwamba tutoe silaha kwa wananchi na hasa katika vijiji kuweza kumiliki silaha, basi pale tutakapokuwa tunapitia sheria, pamoja na kanuni hizi tutaliangalia kama hilo litawezekana ili kusudi tuone kama linaweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili alilouliza ni kwamba kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za mwaka 2011 ndiyo vinatoa viwango vile vinavyostahili. Nataka niseme kwamba tunachotoa siyo fidia, ni kifuta machozi na kifuta jasho. Ndiyo maana imeandikwa kabisa kwamba kifuta jasho kama binadamu ameuwawa ni shilingi1,000,000, kama amejeruhiwa ni shilingi 500,000, kama ni mazao yana viwango vyake kufuatana na kilometa. Kwa hiyo, hivi viwango vipo kwa mujibu wa sheria, lakini pale tutakapokuwa tunapitia tutavihuisha na kuona kama kuna haja ya kuvirekebisha ili kusudi vikidhi mahitaji ya wakati uliopo.
Name
Zaynab Matitu Vulu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani juu ya wanyama waharibifu hususan tembo ambao wamesambaa hovyo katika Jimbo la Mtera na kufanya uharibifu mkubwa pamoja na kuua watu?
Supplementary Question 2
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na napongeza majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilitaka kujua, je, ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kuhakikisha inatoa pilipili nyingi ili kuweza kuchoma na kukimbiza tembo hao kwenye maeneo wanayoishi watu hasa ukizingatia kwamba kwanza kuchoma moto misitu ni kuharibu mazingira?
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichosema ni kwamba katika maeneo yale yanayozunguka hifadhi zetu au yale ambayo yapo jirani na hifadhi zetu tunajaribu kuwahamasisha wananchi kwamba wapande pilipili na pia pale ambapo pana kinyesi cha tembo tunakichukua kile tunachoma. Nataka niseme kwamba tutaangalia namna na tutazungumza mikakati ambayo tumeiweka katika kuhakikisha kwamba pilipili zinatosha katika maeneo hayo hasa pale tutakapowasilisha bajeti yetu hapo tarehe 21 na 22 Mei.
Name
Julius Kalanga Laizer
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Primary Question
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani juu ya wanyama waharibifu hususan tembo ambao wamesambaa hovyo katika Jimbo la Mtera na kufanya uharibifu mkubwa pamoja na kuua watu?
Supplementary Question 3
MHE. JULIUS K. LAIZER. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo hili la tembo katika nchi yetu limekuwa likiwasababishia Watanzania umaskini mkubwa sana na mkakati wa Wizara hauoneshi kama kuna jitihada nzuri ya kushughulikia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nauliza swali hili jana usiku tembo wamevamia mashamba ya wananchi zaidi ya ekari 20 na kumaliza kabisa na ni kilomita zaidi ya 20 kutoka eneo la hifadhi. Je, Serikali ina makakati gani wa haraka katika kipindi hiki cha mvua na cha mazao yetu ili kusaidia wananchi kuwaondoa tembo hao waache kuharibu mazao yetu?
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na matukio ya tembo katika maeneo mengi hapa nchini na hii imetokana na kuimarika kwa uhifadhi katika maeneo mengi na hivyo tembo wameongezeka. Pale ambapo pametokea tatizo la namna hiyo tunaomba tuwasiliane haraka ili kusudi askari wetu wa doria waweze kwenda na kuchukua hatua na kuwafukuza tembo hao ili warudi katika hifadhi pale ambapo wanastahili.
Name
Eng. Edwin Amandus Ngonyani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Primary Question
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani juu ya wanyama waharibifu hususan tembo ambao wamesambaa hovyo katika Jimbo la Mtera na kufanya uharibifu mkubwa pamoja na kuua watu?
Supplementary Question 4
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Tatizo la Mtera halina tofauti kabisa na tatizo la kata nzima ya Likuyu Sekamaganga na hususan Kijiji cha Mandela. Walioathirika walishafanyiwa tathmini muda mrefu na hakuna dalili ya kuwalipa hicho kifuta jasho na kifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itatoa hicho kifuta jasho na kifuta machozi kwa wale walioathirika katika Vijiji vya Mandela, Likuyu Sekamaganga, Mtonya pamoja na majirani zao wa Mgombasi?
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na matukio mengi katika lile Jimbo la Tunduru na maeneo mengine pamoja na kile Kijiji cha Mandela. Naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba matukio haya ya wanyama waharibifu ni mengi sana katika nchi yetu kwa sasa hivi. Hili inatokana na kwamba uhifadhi umeimarika na wanyama wameongezeka lakini pia kuna changamoto nilizozisema nilipokuwa najibu swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kuna matukio zaidi ya 3,509 ambapo wananchi wamepatwa na matatizo mbalimbali. Jumla ya fedha ambazo zinadaiwa mpaka sasa hivi katika maeneo na wilaya mbalimbali ni zaidi shilingi milioni 828. Kwa hiyo, kazi tunayoifanya sasa hivi ni kutafuta hizi fedha ili kuhakikisha kwamba hao wananchi wote walioathirika na wanyamapori na wanyama waharibifu basi waweze kupata kifuta jasho na kifuta machozi kinachostahili. Baada ya kupata fedha hizo tutafanya hivyo mara moja. (Makofi)